MAZISHI na kumbukizi za Mwanamapinduzi wa Kenya na Afrika Raila Odinga (80), yamelipa bara hili funzo kuwa upinzani si uadui na ni lazima kujifunza uhimilivu na uvumilivu wa kisiasa unaotangazwa na Rais wa Kenya William Ruto.
Kiongozi huyo wa Kenya alimshuhudia mbele ya Wakenya na dunia kuwa mpinzani wake mkuu wa kisiasa Odinga ni rafiki, mwalimu, ndugu kiongozi mwelekezi na mtu wa kukimbilia wakati wa shida na raha.
Rais Ruto anamwelezea Waziri Mkuu wa zamani wa Kenya Baba Odinga kuwa ni rais wa wananchi, hivyo anastahili heshima na maziko anayopewa Rais wa Taifa na ndivyo alivyozikwa Jumapili nyumbani kwenye shamba la wazazi wake huko Bondo.
Kiongozi huyo anasema anapotangaza maziko ya heshima kama apewayo rais wapo waliompinga wakisema hakuwa rais hivyo hakuyastahili, lakini Ikulu ya Kenya akampa heshima hiyo.
Ukiangalia kilichotokea Nairobi Jumapili na mlolongo mzima wa upinzani Kenya na uhusiano wake na ikulu unaoonyesha kuwa ni utekelezaji wa Falsafa ya R4 inayotangazwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, inayojikita kwenye maridhiano (Reconciliation), ustahamilivu (Resilience), mageuzi (Reforms) na kujenga upya taifa (Rebuilding).
Afrika inajua ni kwanini mifumo ya vyama vingi inakwama na ni kitu gani kinachokwamisha ushindani na kuyumbisha vyama vya kidemokrasia ambacho kimojawapo ni kukosekana R4 zinazoleta maridhiano, uhimilivu na uvumilivu, mageuzi na ujenzi mpya usioangalia yaliyopita.
Uwanja wa vyama vingi Afrika una mengi ya kujifunza kutoka kwa Dk. Ruto. Vyama tawala vimepata somo kwa Dk. Ruto pia kuwa ni lazima kuendelea kufurahiana na kuheshimiana hata kama ni wapinzani kupitia R ya maridhiano. Ndicho ambacho Raila naye alitaka watu kujifunza kuwa na maridhiano na kusahau yaliyopita.
Ni kwasababu Raila alirejea na kuanza siasa baada ya kuwekwa kizuizini na Rais Daniel Arap Moi kwa miaka minane bila kufunguliwa mashtaka. ‘Baba Raila aliachiwa mwaka 1991 ikimaanisha kuwa alitupwa kizuizini mwaka 1980 na kutokana na kushinikiza mageuzi wakati wa enzi ya udikteta wa Moi. Aliteswa ndani ya vyumba vya Nyayo House, inayodaiwa kuwa ilikuwa kiboko kwa wapinzani wa Moi.
Uhusiano wa Dk. Ruto na Odinga umeonesha kuwa upinzani unatakiwa kupewa nafasi kufanya kazi kwa uhuru zaidi lakini pia upinzani nao usiikwamishe serikali kufanyakazi na kuhakikisha kila mmoja iwe serikali au upinzani kila upande unakubalika kwa wananchi kwa misingi ya maamuzi yao, kufuata sheria na kusimamia haki.
Ruto anaonesha kuwa walioko madarakani kuna walichojifunza kwa wapinzani (resilience) ndiyo maana anasema Raila ni mwalimu wake mkuu akimtaja kuwa ni ‘academy ya siasa’na kwamba yeye ni zao la shule ya uhandisi wa kisiasa ya Odinga, akisema anazungumza naye mara moja baada ya kutangazwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ya Kenya kuwa ndiye Rais, akimtafuta na kumuomba ushauri.
Anasema mambo hayakuishia hapo changamoto za kisiasa zilipoibuka na miswada ya fedha ikakwama anakutana na Baba Odinga kushirikiana naye kwenye kupanga safu ya viongozi mawaziri akimtaja Waziri wa Fedha wa Kenya John Mbadi kuwa ni changuo la ‘Baba’ ili kulijenga upya taifa lililojeruhiwa na kubaki na makovu ndiyo ‘R’ ya rebuliding au kujenga upya.
Dk.Ruto anaonesha kuwa walio kwenye upinzani pamoja na wanaoshika madarakani wana nafasi kubwa zaidi ya kuunganisha nguvu na kuwezesha zaidi mifumo ya kiuongozi inayoridhiana na kwa ujumla anazigusa R4 za Falsafa ya Rais Samia kwa hali ya juu ambayo inaonekana inatakiwa itawale Afrika.
Ruto anaonesha kuwa mamlaka makubwa waliyo nayo marais, bunge na taasisi nyingine za umma yanahitaji kufanya kazi kwa misingi lakini yanatakiwa kufahamu kuwa bila kuwa na upinzani madhubuti, tena wa karibu unaoanzia kutikisa kwenye uchaguzi wa rais, wabunge na madiwani huenda zisifanikiwe sana na kuonesha ulazima wa kushirikiana.
Anachokionesha Ruto kwa Odinga kisaidie kwa wapinzani wa Afrika kujua kuwa ni wanahusika moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja kwenye kufikia mabadiliko ya katiba, ya uchumi, siasa, jamii na yoyote mengine kwa lengo la kuimarisha demokrasia kwenye mabunge, kubadili sheria na kusaidia serikali kufanya kazi kwa ufanisi zaidi ili kuwaletea watu maendeleo.
Upinzani unatakiwa kutaja changamoto, kukosoa kwa njia ambazo katiba inaziruhusu na kushirika, kusimamia haki, utawala wa kisheria, usawa na demokrasia ili kufikia maendeleo ya kweli. Rais Ruto anawaonyesha wapinzani na viongozi wa Afrika kuwa kwenye siasa hakuna adui wala rafiki wa kudumu kwenye ulingo huo ambao viongozi wengi wa Afrika wanatetereka.
Aidha, anawapa somo kuwa katika siasa ni wazi kuwa ni lazima wasisahau walipotoka, ndicho pia Ruto anachotaka watu wakifahamu , akisema 1997 Ruto alichaguliwa kwa mara ya kwanza kuwa mbunge wa Eldoret Kaskazini wakati huo Odinga naye akiwachaguliwa tena kuwa mbunge wa Lang'ata lakini pia akiwa amepoteza urais kupitia chama cha National Development Party (NDP), anasema baada ya hapo wawili hao wanapata fursa ya kukutana na kuongeza mshikamano wa kibunge na kuanzia bungeni wakawa na uwanja mpana wa siasa, hivyo usiwasahau waliokuinua na kukufikisha kileleni kwenye siasa hata kama wamegeuka kuwa wapinzani wako. .
VIMBWANGA VYA RAILA
Alikuwa mbunifu kwenye siasa na katika kampeni zake hasa za uchaguzi mkuu alifurahisha kwa kuweka ucheshi, nyimbo, vitendawili na wakati mwingine akitumia mbinu ya kutangaza kandanda na kuchangamsha sana wafuasi wake na wafuatiliaji wa kampeni zake kutoka maeneo mbalimbali ya Afrika hasa Afrika Mashariki.
Gazeti pekee la Kiswahili nchini Kenya la Taifa Leo, lisema alianza kwa vitendawili maarufu hadi kubuni matangazo akifananisha uchaguzi na mechi ya soka kati ya chama chake na washindani, Raila alibadilisha mikutano ya kisiasa kuwa ya kusisimua.
Katika kila mkutano mkubwa, umati ulisubiri atoe kitendawili nao ulijibu, tega Kisha kitendawili kilifuata, mara nyingi kikiwa na maana ya kisiasa. Mfano mwaka wa 2017, katika mojawapo ya matamshi yake ya kukumbukwa, alitumia methali, kelele za chura haziwezi kuzuia ng’ombe kunywa maji. Si hivyo tu, Juni 25, 2017 akiwa Busia, alitumbuiza umati kwa kitendawili kilichobeba kejeli kali ya kisiasa:“Kitendawili… Tega Alikimbia usiku uchi akachoka akalala fo fo fo. Alipoamka asubuhi alipata aibu kubwa. Yeye ni nani? Mmeshindwa. Mnipatie mji, eti Busia? Huyo ni mchawi, huyo ni Jubilee. Miaka nne wamelala fofofo.” Linakumbusha Taifa Leo.
Mbali na kuchekesha, vitendawili vyake vilijaa ujumbe kuhusu siasa, uvumilivu na matumaini. Raila alielewa jinsi mpira wa miguu ulivyo na mvuto kwa Wakenya. Mwaka wa 2017, aligeuza hotuba zake za kisiasa kuwa maelezo ya mechi. Umati ulifurahia aliposema:“Uhuru ameanza, amempatia Ruto, Ruto anampatia Duale… Kindiki amepiga shuti, mpira umeenda nje.Mpira unarudi kwa Weta, anampa Isaac Rutto, amechenga William Ruto hadi ameanguka. Mpira bado unaenda mbele…Musalia Mudavadi anapewa, anachenga Duale, anampatia Kalonzo, Kalonzo anampa Raila… GOOOAAAL.
Kaulimbiu ya Raila ya mwaka wa 2022.Inawezekana, iliibua matumaini. Ilionekana kwenye mabango, fulana na nyimbo. Alipoitumia pamoja na leo ni leo,” alizidisha ari miongoni mwa wafuasi wake kwamba ushindi ulikuwa karibu.Mwaka 2013, Raila alitumia kauli “Punda amechoka” kuonesha kuchoshwa kwa wananchi na ufisadi na uongozi mbaya. Kabla ya kuanza kampeni zake, Raila alianza kwa tamko maarufu. Hayaaa alipotamka neno hili, umati ulitulia mara moja, ukisubiri kauli muhimu. Kwa wafuasi wake, lilikuwa ishara kwamba jambo la maana linafuata.
Kwa Raila, siasa hazikuwa tu kuhusu kura, bali kuhusu kuwasiliana. Maneno yake yaliwafikia watu wa kawaida. Alizungumza lugha yao, alicheza nyimbo zao, na alielewa matumaini yao. Alitoa siasa kwa viongozi na kuirudisha kwa wananchi. Anapozikwa nyumbani kwao Bondo ucheshi, busara na kauli zake zitabaki kuwa sehemu ya historia ya siasa za Kenya, linasema Taifa Leo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED