Ligi yetu iwe bora zaidi msimu huu

Nipashe
Published at 11:32 AM Sep 15 2025
Mpira
Picha: Mtandao
Mpira

MSIMU mpya wa Ligi Kuu Tanzania bara wa 2025/26 unatarajiwa kufungua pazia lake keshokutwa Jumatano ya Septemba 17, mwaka huu.

Ligi hiyo inaanza baada ya mchezo wa Ngao ya Jamii utakaopigwa kesho kati ya Mabingwa watetezi Yanga dhidi ya Simba, mchezo utakaopigwa uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Bodi ya Ligi, KMC na Dodoma Jiji ndizo zitakazo fungua pazia hilo, zitakapokwaana kwenye Uwanja wa KMC Complex, kabla ya Coastal Union kuivaa Prisons, siku hiyo hiyo.

Alhamsi kutakuwa na michezo mingine miwili, ambapo Mashujaa FC, itakuwa nyumbani kwenye uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma, ikiikaribisha, JKT Tanzania, kabla ya Namungo kucheza na Pamba Jiji.

Sisi Nipashe tunatarajia ligi ya msimu huu kuwa na ushindani mkubwa zaidi, baada ya timu zote 16 kufanya usajili wa nguvu kwa kuboresha vikosi vyao wakati wa dirisha la usajili wa wachezaji.

Pamoja na ushindani ambao tunautarajia kwenye Ligi hiyo, pia tunawaasa waamuzi kuchezesha mechi zote kwa kutumia kanuni na sheria zilizoweka ili mwisho wa msimu tuweze kupata bingwa kwa uhalali.

Tunasema hivyo, kutokana na ukweli kwamba, baadhi ya waamuzi msimu uliopita walikuwa na makosa mengi yaliyosabisha baadhi ya timu kushinda au kupoteza michezo yao.

Tunaamini kwamba, Bodi ya Ligi Kuu na Shirikisho la soka Tanzania, TFF, zitakuwa makini katika kuhakikisha kwamba, zinasimamia vizuri sheria na kanuni zake, kwa ajili ya ubora wa Ligi hiyo.

Pia TFF na Bodi ya Ligi zinatakiwa kuwasimamia waamuzi hao kwa umakini mkubwa na kutoa adhabu inayostahili kwa wale wote ambao wataonekana kufanya makosa ambayo yanaweza kuzuilika.

Hiyo inamaana kwamba, kama vyombo hivyo vinavyosimamia mchezo huo vitakuwa makini katika majukumu yake, ligi yetu itakuwa bora na bingwa wake atapatikana kihalali bila kuwa na malalamiko kutoka kwa timu nyingine.

Tunasema hivyo, kwa saabu bingwa wa Ligi atakuwa mwakilishi wa Tanzania kwenye michuano ya kimataifa, hivyo akipatikana yule ambaye ‘amebebwa’ atashindwa kufanya vizuri katika mashindano hayo.

Pia tunatarajia wachezaji kuonesha vipaji vyao na thamani zao kwenye klabu walizosajiliwa ili kuinogesha ligi hiyo.

Kiwango kitakachooneshwa na wachezaji hao pia kitawasaidia kuweza kujitangaza kimataifa na hivyo kupata nafasi ya kutakiwa na timu kutoka nje ya mipaka ya Tanzania.

Pia ubora wa wachezaji hao utamsadia kocha wa timu ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars), Hemed Morocco kuwa na wakati mzuri wa kuchagua wachezaji bora wa kuiwakilisha nchi.

Ligi yetu ikiwa bora na kuzalisha wachezaji bora, maana yake hata timu ya Taifa nayo itakuwa bora, kwani kocha atakuwa na uwanda mpana wa kuchagua wale walio bora kabisa.

Hivyo, tunatumaini wachezaji kujipambania vya kutosha na kuzisaidia timu zao katika kuwania ubingwa wa Ligi hiyo kwa msimu huu.

Tunazitakia kila la heri timu zote kwenye ligi hiyo na tunaamini, zitaonesha kiwango bora pamoja na burudani nzuri kwa mashabiki wake.