KATIKA karne hii ya maendeleo ya sayansi na teknolojia ya tiba, jamii imejenga imani kubwa kwa dawa na vifaa tiba kama silaha kuu dhidi ya magonjwa.
Vidonge, sindano, vipimo vya ujauzito na vifaa vingine vinavyoonekana visivyo na madhara baada ya matumizi, kwa kweli vinaweza kuwa hatari kubwa kwa afya na mazingira ikiwa havitashughulikiwa ipasavyo.
Tatizo hili, linalonyemelea kimyakimya, limegeuka kuwa bomu la kiafya na kimazingira linalosubiri kulipuka katikati ya makazi yetu.
Ripoti maalum tuliyochapisha jana na leo kuhusu kadhia hii, inaonesha wazi kuwa mji mkuu wa Dodoma, kitovu cha serikali na maendeleo ya kisasa, unakumbwa na changamoto kubwa ya utupaji holela wa mabaki ya dawa na vifaa tiba. Picha za watoto wakicheza na sindano zilizotumika au kutumia vidonge vilivyopitwa na muda kama vitu vya kuchezea ni ushahidi wa kusikitisha unaodhihirisha jinsi jamii ilivyo kwenye hatari kubwa, huku ikiwa na uelewa mdogo au kutofahamu kabisa.
Kisheria, Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya Mwaka 2004 imeshajieleza bayana: dawa na vifaa tiba vilivyopitwa na muda ni taka hatarishi, na vinapaswa kuteketezwa kwa njia maalum.
Hata hivyo, hali halisi mitaani ni kinyume cha sheria hii. Mabaki haya yanazagaa kwenye madampo ya taka za kawaida, vichochoroni, na hata ndani ya nyumba zetu, bila utaratibu maalum wa uteketezaji.
Tatizo halipo tu kwenye utupaji ovyo. Utafiti wa kitaaluma umebaini kuwa asilimia 70 ya kaya zinahifadhi dawa majumbani, huku asilimia 96 ya dawa hizo zikiwa hazitumiki tena.
Ni jambo la kawaida sasa kukuta familia nyingi zikihifadhi dawa za zamani kwa "matumizi ya baadaye", hali ambayo si tu inaleta hatari ya matumizi mabaya ya dawa, bali pia inasababisha uchafuzi wa mazingira endapo dawa hizo zitamwagika au kutupwa kiholela.
Wataalamu wa afya na mazingira wanatoa onyo kali kuhusu tabia hii. Dawa ni kemikali zenye sumu zinazoweza kudhuru viumbe hai, kuchafua maji, kuharibu udongo na hata kuchochea usugu wa vimelea vya magonjwa dhidi ya dawa.
Vilevile, vifaa tiba kama sindano na vipimo vilivyotumika vinaweza kusambaza magonjwa hatari kama, homa ya ini, Virusi vya Ukimwi (VVU) na kipindupindu ikiwa vitagusa watu bila kinga.
Jambo la kusikitisha zaidi ni kwamba, licha ya kuwapo mamlaka kama Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), ofisi za afya za jiji, na vyombo vya habari, bado elimu kwa wananchi kuhusu hatari hizi ni finyu mno.
Wananchi kama Michael James wa Chang’ombe au Mwamvua Twalibu wa Maili Mbili, kwa kauli zao, wanaonesha jinsi walivyo mbali na uelewa wa sheria na madhara ya kiafya kuhusu mabaki ya dawa na vifaa tiba.
Ni wazi kuwa tatizo hili haliwezi kutatuliwa kwa ukaguzi wa vituo vya afya pekee au kwa mikakati ya kifupi. Kinachohitajika ni mkakati wa kitaifa, wenye nguvu na wa kudumu wa elimu kwa umma.
Kampeni za uhamasishaji kupitia redio, runinga, mitandao ya kijamii na mikutano ya hadhara lazima ziimarishwe. Shule, taasisi za dini, na viongozi wa kijamii pia wanapaswa kuhusishwa kikamilifu ili kufikisha ujumbe huu kwa kila mwananchi.
Vilevile, ni wakati sasa wa serikali kuanzisha mfumo wa kitaifa wa ukusanyaji na uteketezaji mabaki ya dawa na vifaa tiba kutoka katika kaya.
Kama tunavyokusanya taka ngumu na plastiki, basi lazima tuwe na mifumo rasmi ya kuchakata taka hizi hatarishi. Bila hivyo, juhudi zote za kulinda afya ya jamii na mazingira zitaendelea kuwa sawa na kujaribu kuzuia mafuriko kwa kutumia ungo.
Nipashe tunatoa wito kwa mamlaka zote husika; Wizara ya Afya, NEMC hadi serikali za mitaa kuchukulia suala hili kwa uzito wa kipekee. Ni lazima tutambue kuwa mabaki ya dawa na vifaa tiba si tu taka, bali ni sumu inayoweza kuathiri vizazi vya sasa na vijavyo.
Tukishindwa kuchukua hatua sasa, tutakuwa tumewatelekeza wananchi wetu katika hatari isiyoonekana, lakini yenye madhara makubwa na ya muda mrefu. Mazingira salama ni afya ya taifa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED