Mkazo uwekwe utoaji elimu ya afya vijijini

Nipashe
Published at 02:04 PM Sep 25 2025
Miundombinu bora huboresha huduma
Picha: Mtandao
Miundombinu bora huboresha huduma

VIFO vinavyotokana na magonjwa sugu kama saratani, kifua kikuu, virusi vya ukimwi na kisukari vimekuwa vikiongezeka siku hadi siku, hivyo kugharimu maisha ya watanzania wengi ambo ni nguvu kazi ya taifa. Mbali na vifo hivyo, vingine ni vile vya uzazi na watoto chini ya miaka mitano.

Kutokana na kuongezeka kwa vifo hivyo, serikali ilichukua hatua kwa kusogeza huduma za afya kwa wananchi. Katika kufanikisha hilo, serikali iliandaa Mpango wa Maendeleo ya Afya ya Msingi ambao Pamoja na mambo mengine, ulilenga kujengwa kwa vituo vya kutolea huduma za afya katika maeno mbalimbali ya nchi. 

Chini ya mpango huo, iliazimiwa kwamba kuwe na zahanati katika kila kijiji, kituo cha afya katika kila kata na hospitali ya wilaya au halmashauri katika makao makuu ya wilaya au mamlaka ya serikali za mitaa. Kwa upande wa mikoa, iliazimiwa kuwe na hospitali za rufani na katika kanda kuwe na hospitali za rufani za kanda kwa lengo la kupunguza mlundikano wa wagonjwa katika ngazi za kitaifa na kikanda. 

Kwa ujumla, mpango huo ulifanikiwa kwa kiasi kikubwa kwa sabau hivi sasa kila Kijiji kina zahanati na takriban halmashauri zote nchini zina hospitali  zilizosheheni huduma mbalimbali kama afya ya mama na mtoto, maabara za kiasa, dawa na vifaa tiba. Pia serikali kila mwaka imekuwa ikijitahidi kuajiri wahudumu wa afya katika hospitali na zahanati kulingana na  mahitaji maalum.

Kuwapo kwa huduma hizo katika ngazi husika, kumepunguza kwa kiasi kikubwa vifo hivyo ambavyo vilikuwa mzigo mzito na vilikuwa vikigharimu maisha ya wajawazito wakati wa kujifungua na vile vya Watoto chini ya miaka mitano. 

Kwa mujibu wa takwimu za serikali kupitia Wizara ya Afya, vifo vya watoto vimepungua kwa asilimia 35 kutoka 67 kati ya Watoto 1,000 hadi 43 kwa 1,000. Aidha, vifo vitokanavyo na uzazi vimepungua kutoka 556 kwa 100,000 hadi 101 kwa 100,000 kutoka mwaka 2016/17 hadi 2022/23. 

Takwimu hizo zinaonesha mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kuzuia na kudhibiti vifo hivyo hatimaye kufanya nguvu kazi hiyo ya taifa, kwa maana ya wajawazito kuwa stahimilivu sambamba na kujenga afya njema ya Watoto ambayo ni nguvukazi bora ya miaka ijayo.    

Pamoja na mafanikio yaliyoainishwa, bado kuna tatizo katika maendeleo ya afya ya jamii kwa ujumla kutokana na kuongezeka kwa vifo vya magonjwa sugu kama vile maradhi ya moyo, shinikizo la juu la damu, saratani hasa ya shingo ya kizazi na tezi dume. Vifo hivyo kutokana na wataalamu wa afya, kwa kiasi kikubwa, vinasababishwa na watu wengi kuchelewa kufika kwenye vituo vya tiba na kufanyiwa uchunguzi mapema ili kama wanabainika kuwa na tatizo waanze matibabu mara moja. 

Kuwapo kwa sababu hiyo, ni vyema sasa hatua zikachukuliwa ili kupunguza athari. Kwa mantiki hiyo, elimu ya afya inapaswa kuwa ajenda kuu ya kupunguza vifo vitokanavyo na magonjwa sugu ambayo kwa sasa yamekuwa tishio kwa kugharimu maisha ya watu.  Ni muhimu kwa wadau wote wa afya kuwa na programu za elimu ya afya kwa kuwaeleza wananchi kuhusu magonjwa hayo sugu. 

Serikali imejitahidi kutoa elimu kuhusu udhibiti wa magonjwa mbalimbali ikiwamo kuendesha programu za afya hasa kwa kinamama wanaohudhuria kliniki. Elimu kama hiyo inapaswa kufanywa na wadau wote na kasi iongezwe katika maeneo mbalimbali hasa vijijini ambako wengi wanakumbwa nayo kwa kuchelewa kufika kwenye vituo vya afya.