Wakati umefika kusimamia kisheria biashara ya vyakula

Nipashe
Published at 03:54 PM Sep 16 2025
Miji mikubwa mlo wa barabarani kama huu ni kawaida
Picha: Mtandao
Miji mikubwa mlo wa barabarani kama huu ni kawaida

KATIKA toleo letu la jana, tulikuwa na sehemu ya pili ya ripoti ya biashara ya vyakula vinavyouzwa mitaani jijini Mwanza, hali inayozidi kudhihirisha ukweli mchungu kwamba sheria pekee hazitoshi. Kinachokosekana ni nia ya kweli ya utekelezaji.

Taarifa zinaonesha wazi kwamba licha ya kuwapo marufuku ya kitaifa iliyotolewa na Waziri wa Afya mwaka 2015, na pamoja na Sheria Ndogo za Afya za Jiji la Mwanza za Mwaka 2024, biashara ya vyakula mitaani inaendelea kushamiri, bila kuzingatia masharti ya usafi na afya ya umma.

Kwa miaka 10 sasa, wananchi wamekuwa wakila vyakula vinavyopikwa na kuuzwa kwenye mazingira yasiyokuwa salama pembezoni mwa barabara, mbele ya maduka, chini ya miti, na mara nyingine hata karibu na maeneo ya uchafu. 

Vyakula hivi havina ulinzi dhidi ya inzi, vumbi, au hata joto kali linalochochea kuharibika kwake. Ni hatari inayoonekana wazi, lakini inaachwa iendelee.

Kwa mtazamo wa kisheria na kiafya, hali hii ni kushindwa kwa mifumo yetu ya usimamizi. Sheria zipo, lakini hakuna msimamo thabiti wa utekelezaji. 

Halmashauri inatoa miongozo, lakini haichukui hatua stahiki za kuhakikisha inatekelezwa. Hii inatia shaka, kama si dalili ya kupuuzia usalama wa maisha ya wananchi.

Ofisa Afya wa Kata ya Igogo jijini Mwanza, Chilonge Hamis, anatoa mfano hai wa jinsi ambavyo elimu tu haitoshi. Anasema wafanyabiashara huachwa wakiuza mihogo iliyokaangwa asubuhi, wakiibeba kwa kutumia vikapu kutwa nzima, hadi jioni. 

Ni wazi kuwa ushauri haupo kwa ajili ya kufurahisha, bali una lengo la kuzuia milipuko ya magonjwa kama kipindupindu, typhoid na maradhi ya tumbo, ambayo yote ni ya kuepukika kama kungekuwa na nidhamu katika usimamizi wa afya ya jamii.

Nipashe tunakubaliana kwamba tatizo la ajira ni kubwa, na kweli kuna wananchi wanaoingia katika biashara hii kwa sababu hawana njia nyingine ya kujipatia kipato. 

Hili ni suala la kijamii ambalo linahitaji majibu ya kitaasisi kama vile kuanzisha vituo maalum vya mamalishe vilivyo rasmi, vyenye vibali, na vinavyotunzwa kwa viwango vya usafi vinavyokubalika. 

Serikali za mitaa zina uwezo na mamlaka ya kufanya hivyo, badala ya kuacha kila mtu afanye anavyoona inafaa kwa kigezo cha “kutafuta riziki”.

Wakati umefika sasa kwa mamlaka kutofumbia macho biashara haramu za chakula, kwani si tu zinahatarisha afya ya watu, bali pia zinawadhalilisha wafanyabiashara waliowekeza katika migahawa halali na wanaofuata sheria.

Haiwezekani mfanyabiashara anayelipa kodi, anayepimwa afya, anayefuata masharti ya mazingira, ashindane katika soko moja na mtu anayechoma nyama mbele ya duka kwenye karatasi ya nailoni iliyojaa vumbi.

Ofisa Afya wa Jiji la Mwanza, Audiphace Sabbo, anasema sasa marufuku inaanza kutekelezwa rasmi, na tunampongeza kwa msimamo huo.

Hata hivyo, isiwe kauli tu, bali tunahitaji kuona utekelezaji wa vitendo. Maagizo haya yasigeuke kuwa porojo kama mengine yaliyopita.

Wananchi wanahitaji kuona tofauti: kwamba sasa chakula hakitauzwa ovyo mitaani, kwamba wauzaji wanazingatia mavazi ya usafi, na kwamba mazingira ya biashara yanakaguliwa mara kwa mara.

Katika nchi inayoheshimu utawala wa sheria, hakuna sababu ya kuruhusu watu kuuza chakula kwa njia ya kiholela, kinyume cha sheria, kwa kisingizio cha “kutafuta maisha.” 

Kama hali hii itaendelea kufumbiwa macho, basi tunatengeneza bomu la kiafya linalosubiri kulipuka, tena katika jamii masikini isiyokuwa na uwezo wa kugharamia matibabu ya maradhi haya yanayoepukika.

Kwa hiyo, Nipashe tunatoa rai kwa Halmashauri ya Jiji la Mwanza kusimamia sheria zake kwa nguvu zote, bila ubaguzi wala huruma kwa wanaokiuka masharti ya afya.

Vilevile, tunatoa rai kwa Serikali Kuu kupitia Wizara ya Afya, kushirikiana na halmashauri katika kutoa rasilimali na mafunzo kwa maofisa afya ili watekeleze wajibu wao kikamilifu.

Nipashe pia tunatoa rai kwa wananchi kutambua kuwa afya ni jukumu la pamoja. Si sahihi kununua au kula chakula kisicho salama kwa sababu tu ni rahisi au karibu.

Afya ya jamii si anasa, ni haki ya msingi. Tusiruhusu biashara kiholela ya chakula kuwa chanzo cha vifo visivyo na sababu. Sasa ni wakati wa kuchukua hatua.