Fukwe za Kawe na Rainbow jijini Dar es Salaam zimewahi kuwa maeneo ya furaha, mapumziko na shughuli za kiuchumi kwa maelfu ya wakazi wa jiji, watalii na wajasiriamali wadogo. Leo hii, maeneo hayo yamegeuka kuwa taswira ya huzuni na fedheha.
Kinachotawala sasa si sauti ya mawimbi au harufu ya mihogo ya kuchoma, bali uvundo wa taka, hasa plastiki, ambazo si tu zimeua haiba ya fukwe hizo, bali pia zimeweka hatarini afya ya jamii, uhai wa bahari na kipato cha watu wa kawaida.
Tatizo la taka, hasa plastiki, halipaswi tena kuchukuliwa kama suala la kawaida la kijiji au kata moja. Hili ni janga la kitaifa na la kimataifa.
Kwa mujibu wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP), zaidi ya asilimia 85 ya taka zinazookotwa baharini ni plastiki, huku zaidi ya tani milioni nane za plastiki zikitupwa baharini kila mwaka duniani kote.
Hali hii si tu inahatarisha maisha ya viumbe wa baharini, bali pia inarudi kwetu kwa njia ya samaki tunapokula, maji tunayokunywa, na hewa tunayovuta.
Dar es Salaam peke yake inachangia zaidi ya asilimia 15 ya taka zote nchini. Kiwango kikubwa cha taka hizi huishia kwenye mito na hatimaye baharini.
Ripoti ya Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) inaonesha kuwa hadi tani milioni 20 za taka huzalishwa kila mwaka nchini, hali ambayo inatoa picha ya uzembe wa pamoja – wa mamlaka, wazalishaji na wananchi.
Tunahitaji kuzungumza ukweli: Tanzania inashindwa kusimamia kikamilifu sheria zake za mazingira. Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya Mwaka 2004 inaelekeza wazi kuhusu wajibu wa wazalishaji katika kudhibiti taka wanazozalisha, lakini utekelezaji wake ni hafifu.
Mfumo wa Extended Producer Responsibility (EPR), yaani uwajibikaji wa moja kwa moja wa wazalishaji katika kuchakata na kurejesha taka zao, haujatekelezwa kwa nguvu inayotakiwa.
Ukweli huu unaathiri maisha halisi ya watu. Katika ripoti yetu ya juzi, kijana mvuvi, Toufiq Salmin, anarejea nyumbani na chupa badala ya samaki. Mama mjane Mbonile Francis anaona wateja wakikimbia kutokana na mazingira machafu.
Maelfu ya wajasiriamali walioegemea kwenye utalii wa ndani wanaangamia kiuchumi. Hii si hadithi ya mbali. Ni ukweli unaowaumiza Watanzania wa kawaida kila siku.
Athari za kiafya ni mbaya zaidi. Daktari Wilbroad Kyejo anatoa tahadhari kuhusu plastiki kuvunjika na kuingia katika mfumo wa chakula kupitia samaki. Kemikali zinazopatikana kwenye microplastics kama BPA, phthalates na PCBs zinaweza kusababisha saratani, matatizo ya uzazi, magonjwa ya ngozi na hata madhara ya mfumo wa kinga mwilini.
Tatizo hili pia linachangiwa na kutokuwapo kwa elimu ya mazingira kwa jamii. Shirika la Simply Green linaonesha kuwa asilimia 80 ya taka walizokusanya kwenye fukwe ni plastiki, huku kampuni zinazozalisha bidhaa hizo zikishindwa kuweka mifumo ya ukusanyaji taka baada ya matumizi. Tunahitaji zaidi ya kampeni za usafi wa siku moja. Tunahitaji mabadiliko ya mifumo.
Kwa upande wa serikali, kuna hatua za msingi zimeanza kuchukuliwa, kama vile mkakati wa Mazingira wa 2022-2032 na ushiriki wa kampuni 257 katika kuchakata taka. Hii ni habari njema, lakini bado haitoshi. Kinachokosekana ni utekelezaji madhubuti, usimamizi mkali, na ushirikiano wa dhati kati ya sekta binafsi na umma.
Viongozi wa mitaa na wilaya, kama Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Saad Mtambule, wanaweza kuwa sehemu ya suluhisho kwa kushirikiana na vijana wanaotumia teknolojia na ubunifu katika kuchakata taka. Uwekezaji kwao si tu unatatua tatizo la taka, bali pia unaongeza ajira na kipato miongoni mwa vijana.
Tanzania pia ina nafasi ya kujifunza kutoka kwa mataifa jirani kama Rwanda, ambayo imepiga hatua kubwa katika kudhibiti plastiki.
Nipashe tunaona ni wakati sasa wa kuachana na visingizio. Wazalishaji plastiki lazima wawajibike. Mamlaka za usimamizi wa mazingira lazima zisimamie sheria kwa nguvu zote. Jamii lazima ifundishwe, ihamasishwe na kushirikishwa kikamilifu. Bahari ni maisha. Tusipoilinda leo, kesho yetu itaangamia kimyakimya.
Kama taifa, hatuna muda wa kusubiri. Serikali ianze mara moja kutekeleza mfumo wa EPR kwa kulazimisha wazalishaji plastiki kuwajibika. Elimu ya mazingira ipelekwe hadi ngazi ya shule ya msingi. Sheria zitekelezwe.
Na kila Mtanzania atambue: plastiki unayoitupa leo, inaweza kukuua wewe au mtoto wako miaka mitano ijayo. Fanya uamuzi sahihi leo kwa ajili ya kesho salama.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED