Yanga, Simba, Azam na Singida nafasi mnayo

Nipashe
Published at 02:56 PM Sep 22 2025
Uwanja wa Taifa, nyenzo muhimu kwa soka
Picha: Mtandao
Uwanja wa Taifa, nyenzo muhimu kwa soka

WAWAKILISHI wa Tanzania kwenye michuano ya soka inayosimamiwa na Shirikisho la mpira wa miguu Afrika, CAF, wameanza vyema kwenye mechi zao za kwanza kwa kupata ushindi ugenini.

Lakini wao Mlandege FC kutoka Zanzibar ilianza vibaya michuano hiyo kwa kupoteza kule nchini Ethiopia, bada ya kukubali kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa timu ya EIC.

Yanga ambao ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania bara, wao walianza kurusha karata zake kwenye uwanja wa 11 Novembro jijini Luanda nchini Angola, Ijumaa, wakicheza na Wiliete de Benguela ya huko.

Yanga kwenye mchezo huo ilipata ushindi wa mabao 3-0, yakifungwa na Aziz Andabwile, Edmund John na Prince Dube, hivyo kuwaweka kwenye nafasi nzuri katika mchezo wa marudiano Jumamosi ijayo.

Kwa upande wa Simba, walipepetana na Gaborone United na wakaibuka na ushindi wa bao 1-0 Jumamosi usiku, na hivyo pia kujiweka kwenye nafasi nzuri kwenye mchezo wa marudiano Jumapili ijayo.

Mechi hizo za Yanga na Simba zilikuwa za hatua ya awali ya michuano ya Ligi ya mabingwa Afrika, ambapo wanawania kufuzu hatua ya makundi.

Kwa upande wa michuano ya Kombe la Shrikisho, Azam FC ilipata ushindi mabao 2-0 ikiwa ugenini, Sudan Kusini, kwenye uwanja wa Juba, ikicheza dhidi ya Al Mereikh Bentiu, wakati nchini Rwanda, Singida Black Stars nayo ikipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Rayon Sports, kwenye Uwanja wa Nyamirambo, jijini Kigali.

Hiyo inamaana kwamba, timu zetu hizi nne zina nafasi nzuri zaidi ya kuendeleza ushindi kwenye mechi zao za marudiano na kuwa na nafasi nzuri ya kusonga hatua inayofuata, kabla ya kuingia kwenye makundi.

Pamoja na ushindi huo ambao timu hizo ziliupata ugenini, lakini tunazishauri kwamba, zisibweteke, kwani mchezo wa soka, hautabiri na hivyo zinatakiwa kujipanga vizuri zaidi kwa marudiano.

Pia zikumbuke kwamba, zilipata bahati ya kuanza ugenini na kupata ushindi huko, hivyo zimerahisisha kazi kwenye mechi zao za marudiano na hivyo, lazima zijipange vya kutosha.

Tunasema hivyo kutokana na ukweli kwamba, timu walizozifunga sio kwamba hazina viwango bora, bali wao walichanga karata vizuri zaidi na kuweza kupata ushindi huo.

Kama zenyewe ziliweza kupata ushindi ugenini, maana yake hata wapizani wao wanaweza kupindua meza na kupata matokeo mazuri kwenye mechi za marudiano, hivyo timu zetu hazipaswi kujisahau.

Tunaamini mabenchi yote ya ufundi kwa timu hizo yatafanyia kazi mapungufu yaliyoonekana kwenye mechi zao hizo za kwanza ili kujiweka imara zaidi.

Kuanza kwa ushindi kwa timu zetu nne, maana yake ni kwamba, zimetuma salamu nzuri za kiwango cha soka la Tanzania kimataifa, hivyo wito wetu ni kuhakikisha mechi zao za marudiano wasifanye makosa yoyote.

Kwa upande wa Mlandege ya kule Zanzibar, nayo haitakiwi kukata tamaa, kwani kama ikijipanga vizuri ina uwezo wa kupata ushindi kwenye uwanja wao wa nyumbani katika mchezo wa marudiano.

Hivyo basi, sisi Nipashe tunazitakia kila la heri timu zetu ili ziweze kupata ushindi kwenye mechi za marudiano na hatimaye kufuzu kwa hatua inayofuata na baadaye kwenye makundi.