Ziwa Tanganyika liko hatarini, madhubuti zichukuliwe

Nipashe
Published at 12:16 PM Sep 11 2025
Ziwa Tanganyika jinsi linavyoonekana kutoka angani
Picha: Wikipedia
Ziwa Tanganyika jinsi linavyoonekana kutoka angani

ZIWA Tanganyika, moja ya maajabu ya asili barani Afrika na hazina ya kipekee ya kibaiolojia duniani, sasa linapiga kelele za kuomba msaada.

Wavuvi wanarudi mikono mitupu, wafanyabiashara wanahesabu hasara, na walaji wa kawaida wanashindwa kumudu bei ya samaki waliowahi kuwa chakula cha kila siku.

Hali ni mbaya. Na kama taifa, hatuwezi kuendelea kufumbia macho jambo hili. Makala maalum iliyochapishwa na gazeti hili jana imebeba ushuhuda mzito.

Kwa karne nyingi, ziwa hili limekuwa uti wa mgongo wa kiuchumi na kijamii kwa wakazi wa maeneo ya Kigoma, na hata nchi jirani kama Burundi, Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC). 

Hii si tu kwa sababu ya wingi wa samaki, bali pia kwa nafasi yake katika ajira, biashara, lishe na utamaduni wa jamii zinazolizunguka.

Lakini sasa, vyanzo mbalimbali vinaonesha wazi kuwa uhai wa Ziwa Tanganyika uko shakani. Mabadiliko ya tabianchi yamevuruga hali ya hewa ya kawaida ya ziwa hilo, na kusababisha samaki kupungua katika baadhi ya misimu. 

Hali hii inazidishwa na uvuvi haramu, matumizi ya zana hafifu au zisizoruhusiwa kisheria, pamoja na ongezeko la watu wanaotegemea ziwa hilo kwa maisha yao ya kila siku.

Wakati wavuvi wanalalamika wazi kuwa wanarudi kutoka ziwani bila hata ndoo mbili za samaki, serikali na wadau wa sekta hii lazima waone dalili hizi kama tahadhari ya moto unaowaka chini kwa chini. 

Kupungua kwa rasilimali samaki kuna maana kudidimia kwa kipato cha kaya, kushuka kwa lishe ya wananchi, na kutoweka kwa maisha ya jadi ya uvuvi.

Bei ya samaki imepanda kwa kiwango kisichoelezeka. Sangara kutoka Sh. 60,000 hadi Sh. 80,000, kambale hadi Sh. 25,000, na dagaa hadi Sh. 60,000 kwa kilo. Bei hizi ni zaidi ya uwezo wa mwananchi wa kawaida na zinatishia usalama wa chakula kwa familia nyingi.

Lakini cha kusikitisha zaidi ni kwamba bado tunaendelea kutumia takwimu za zaidi ya miaka 30 iliyopita kujua wingi wa samaki katika ziwa hili. Jambo hili ni sawa na kuendesha gari kwa kutumia kioo cha nyuma. 

Tanzania inahitaji kufanya tathmini mpya ya kina kuhusu hali ya samaki, maeneo yao ya mazalio na athari za mabadiliko ya tabianchi katika mifumo ya maisha ya viumbe wa ziwani.

Ni kweli kuwa serikali imeanza kuchukua hatua, kama vile kupumzisha ziwa kwa vipindi maalum na kuanzisha ufugaji samaki kwa vizimba. Hizi ni hatua chanya, lakini bado hazitoshi. 

Kuna haja kuwa na mkakati wa kitaifa unaohusisha serikali kuu, serikali za mitaa, wanavijiji, taasisi za utafiti na mashirika ya kimataifa. 

Mkakati huo unapaswa kuwa na vipengele vinavyolenga kudhibiti uvuvi haramu kwa ufanisi zaidi. Sheria za uvuvi lazima zisitekelezwe kwa nguvu na uwazi. Wale wanaotumia nyavu haramu na vifaa visivyo rafiki kwa mazingira lazima wachukuliwe hatua kali.

Ni muhimu pia serikali na sekta binafsi wawekeze kwenye vifaa vya kisasa kama 'fish finders', ambavyo vinaweza kusaidia wavuvi kuvua kwa tija zaidi na kwa njia endelevu.

Mkakati huo unapaswa kuhusisha kufanya utafiti wa mara kwa mara. Bila takwimu sahihi, hatuwezi kupanga kwa ufanisi. Utafiti mpya kuhusu bayonuai ya Ziwa Tanganyika unapaswa kufanywa kila miaka miwili.

Mkakati pia ujikite katika kutoa elimu kwa jamii kuhusu uvuvi endelevu. Elimu kwa wavuvi kuhusu madhara ya uvuvi usio endelevu ni msingi wa mabadiliko ya tabia na mtazamo wa muda mrefu.

Kukuza ufugaji samaki kwa mbinu za kisasa pia kunapaswa kupewa kipaumbele. Ufugaji samaki una nafasi kubwa ya kupunguza shinikizo kwa ziwa, lakini unahitaji msaada wa kifedha na kitaalamu il ulete tija.

Ziwa Tanganyika si tu urithi wa Kigoma, bali ni sehemu muhimu ya urithi wa Taifa. Likiwa na zaidi ya spishi 1,500 za viumbe hai. Asilimia 40 ya spishi hizo hazipatikani kokote duniani. Ni lazima tuchukulie tishio hili kama jambo la kitaifa.

Kwa sasa, ziwa hili linaendelea kuumia kwa ukimya. Lakini muda si mrefu, kimya hicho kinaweza kubadilika kuwa kilio cha kizazi kijacho kitakachouliza: "Mlikuwa wapi wakati Ziwa Tanganyika likifa?"

Jibu letu linapaswa kuwa: Tulisimama, tukachukua hatua, na tukaliokoa.