Ligi Kuu yatoa wageni 13 timu za taifa Afrika

By Faustine Feliciane ,, Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 03:44 PM Mar 23 2025
 Ligi Kuu yatoa wageni 13 timu za taifa Afrika
Picha: Mtandao
Ligi Kuu yatoa wageni 13 timu za taifa Afrika

WAKATI kikosi cha timu ya taifa jana kikiwasili Morocco tayari kwa mchezo wa kufuzu kombe la Dunia dhidi ya timu ya taifa ya nchi hiyo, Ligi Kuu Tanzania Bara imetoa wachezaji 13 kwenye timu za taifa mbalimbali Afrika.

Kwa mujibu wa takwimu na rekodi za gazeti hili, jumla ya nchi tisa za Afrika zilizotaja wachezaji wao wa timu za taifa, baadhi ya wachezaji wanaocheza Ligi Kuu Tanzania Bara wameitwa kwenye timu zao.

Nchi hizo zilizoita wachezaji kutoka Ligi Kuu Tanzania Bara ni Uganda, Kenya, Zambia, Guinea, Mali, Zimbabwe, Burundi, Gambia na Sudan.

Yanga ndiyo timu iliyotoa wachezaji wengi zaidi, ikiwa na wachezaji sita wa kigeni waliokwenda kwenye vikosi vyao vya taifa, zikifuatiwa na timu za Simba, Azam na Pamba Jiji ambazo zimetoa wachezaji wawili, Tabora United ikitoa mchezaji mmoja.

Michuano hiyo ya kufuzu Kombe la Dunia, imekuwa ikiendelea tangu katikati ya wiki, mpaka wiki endi hii.

Wachezaji ambao wanatoka klabu ya Yanga ni Duke Abuya aliyeitwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Harambee Stars ya Kenya, inayojiandaa na mchezo wa kufuzu dhidi ya Gambia na Gabon, mechi za Kundi F.

Clatous Chama na Kennedy Musonda, walioitwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Zambia ambacho kipo Kundi E pamoja na timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars na Khalid Aucho ambaye ameenda kujiunga na Uganda Cranes, iliyo Kundi G, ikicheza dhidi ya Msumbiji na Guinea.

Wengine ni Djigui Diarra, aliyeitwa kwenye kikosi cha Mali ambacho kiko Kundi I, kikitarajia kucheza dhidi ya Comoro na Africa ya Kati, na Prince Dube, ambaye ameitwa na timu ya Zimbabwe kwenda kucheza mechi ya kufuzu fainali za Kombe la Dunia kutoka Kundi C, ambayo ilitarajia kucheza dhidi ya Benin na Nigeria.

Simba imetoa wachezaji wawili ambao ni Steven Mukwala, aliyeitwa na Uganda Cranes na golikipa namba moja wa timu hiyo, Moussa Camara, aliyekwenda kuidakia timu ya Guinea iliyo Kundi G, iliyotarajiwa kucheza dhidi ya Somalia na Uganda.

Azam, imetoa wachezaji wawili ambao ni golikipa namba moja wa timu hiyo, Mohamed Mustafa, akienda kwao Sudan ambayo itacheza dhidi ya Sudan Kusini na Senegal mechi za Kundi B.

Gibril Sillah, akienda kuichezea Gambia, iliyo Kundi F iiliyotarajiwa kucheza na Shelisheli pamoja na Kenya.

Pamba Jiji pia imetoa wachezaji wawili ambao ni Mathew Tegisi, aliyeitwa Kenya na Shasir Nahimana aliyeitwa kwenye kikosi cha Burundi ambayo nayo ipo Kundi F ikitarajiwa kucheza dhidi ya Ivory Coast na Shelisheli.

Tabora United imetoa mchezaji mmoja,Banele Sikhondze, aliyeitwa na timu yake ya taifa ya Eswatini ambayo tayari mchezo wake wa kwanza imesuluhu nyumbani dhidi ya Cameroon na inatarajiwa pia kucheza dhidi ya Mauritius, mechi za kusaka tiketi ya kucheza Kombe la Dunia, kanda ya Afrika kutoka Kundi D.