Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, ametoa mchango wa Shilingi Milioni 20 kwa timu ya taifa ya soka, Taifa Stars, kufuatia ushindi muhimu wa bao 1–0 walioupata dhidi ya Mauritania katika mchezo wa pili wa fainali za mataifa ya Afrika CHAN.
Ushindi huo, uliopatikana kupitia mlinzi wa kulia Somari Kapombe baada ya pasi safi kutoka kwa Iddi Nado, umeimarisha nafasi ya Tanzania kufuzu kwa fainali za AFCON 2025 zitakazofanyika nchini Morocco.
Akizungumza wakati wa makabidhiano yaliyofanyika jijini Dar es Salaam, Chalamila alisema mchango huo ni sehemu ya kutambua juhudi na nidhamu ya timu hiyo pamoja na kuhamasisha kuendelea kwa ubora na ushindi zaidi.
Alisisitiza kuwa mchango wake unaunga mkono dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kukuza michezo na maendeleo ya vijana nchini kote.
"Rais Samia ameonyesha mfano bora kwa kuiunga mkono Taifa Stars, na mimi najivunia kuwa sehemu ya dhamira hii ya kitaifa. Hii si kuhusu mpira tu, bali ni heshima kwa maono ya Rais kuhusu michezo kama nyenzo ya mshikamano na fursa kwa vijana," alisema Chalamila.
Awali, Rais Samia aliahidi kutoa Shilingi Milioni 5 kwa kila bao litakalofungwa na Taifa Stars katika mechi za kufuzu, hatua iliyoongeza ari kwa wachezaji na kuhamasisha ushabiki mkubwa wa umma kwa timu hiyo.
Kwa sasa, timu inaendelea kunufaika na wimbi la hamasa ya kitaifa wanapoendelea kupambana kufuzu kwa mashindano hayo ya bara.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED