Kamati Maalum ya Afya yaundwa kuelekea AFCON

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 12:41 PM Apr 15 2025
Washiriki wa kombe la AFCON
Picha: Mtandao
Washiriki wa kombe la AFCON

MAANDALIZI ya michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) itakayofanyika nchini mwaka 2027 yanashika kasi katika nyanja zote muhimu.

Naibu Waziri wa Afya, Dk. Godwin Mollel, ameliambia  Bunge jijini Dodoma leo  kuwa Kamati maalum ya Afya imeundwa wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge  Cecilia Daniel kuhusu mikakati ya serikali wa kuboresha huduma za afya mkoani Arusha, ikizingatiwa mkoa huo ni miongoni mwa wenyeji wa mashindano hayo kimataifa.

Dk. Mollel amesema kamati hiyo, itahakikisha miundombinu ya afya inaimarishwa kulingana na  mahitaji ya mashindano hayo ya kimataifa, ili kutoa huduma bora kwa wageni na wananchi wakati wa mashindano.

Ameongeza kuwa Sserikali imewekeza katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa Mt. Meru kwa zaidi ya Sh. bilioni tatu, ikiwa ni hatuo juhudi za kukuza tiba utalii na kuboresha upatikanaji wa huduma za afya katika mkoa wa Arusha.

Mashindano ya AFCON 2027, yanatarajiwa kuvuta maelfu ya wageni kutoka mataifa mbalimbali barani Afrika, huku serikali ikiweka mikakati madhubuti kuhakikisha maandalizi yote muhimu, yakiwamo ya kiafya, yanakamilika kwa wakati.