Bodaboda watakiwa kuanzisha uongozi kuzuia uhalifu

By Shufaa Lyimo , Nipashe
Published at 12:30 PM Dec 22 2025
Bodaboda watakiwa kuanzisha uongozi kuzuia uhalifu
Picha:Mtandao
Bodaboda watakiwa kuanzisha uongozi kuzuia uhalifu

Maafisa usafirishaji kwa pikipiki (bodaboda) wa Mtaa wa Msimbazi Magharibi, Kata ya Tabata jijini Dar es Salaam, wametakiwa kuanzisha uongozi kuanzia ngazi ya mtaa na kata kwa lengo la kutambuana na kuzuia uhalifu unaofanywa na watu wanaotumia vijiwe vya bodaboda kama fursa ya kufanya maovu.

Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Msimbazi Magharibi, Harun Adam, alipokuwa akizungumza na maafisa hao wa usafirishaji.

Adam amesema kuwa hatavumilia kuona vijiwe vya bodaboda vinageuzwa maeneo ya uhalifu au uhuni, akisisitiza kuwa vinapaswa kuheshimiwa kama sehemu halali za kazi.

“Katika mtaa wangu sitaki kuona vijiwe vya bodaboda vinafanywa sehemu ya uhalifu au uhuni, bali viheshimiwe kama sehemu nyingine za kazi,” alisema Adam.

Amesema ni marufuku kwa mtu asiyejihusisha na shughuli za bodaboda kukaa katika vituo hivyo, kwani si maeneo ya kupiga porojo. Ameonya kuwa vituo vitakavyobainika kuwa na tabia hizo vitachukuliwa hatua kali, ikiwemo kufungiwa na kutozwa faini.

Aidha, Adam amesema ameona umuhimu wa kuunda uongozi wa vituo hivyo kutokana na kutambua mchango mkubwa wa waendesha bodaboda katika kurahisisha huduma za usafiri kwa haraka ndani ya jamii.

Ameutaka uongozi wa vituo hivyo kuhakikisha wanakusanya majina ya waendesha bodaboda katika kila kituo na kuyawasilisha kwenye ofisi za Serikali ya Mtaa, hatua itakayosaidia kuimarisha ulinzi na usalama kwa kushirikiana na vyombo vya dola.

Amesema uongozi huo pia utasaidia kubaini na kuwaondoa watu wanaojihusisha na biashara haramu, ikiwemo uuzaji wa dawa za kulevya.

Kwa mujibu wa Adam, hadi sasa jumla ya vituo saba vya bodaboda vimeshasajiliwa kisheria ndani ya Mtaa wa Msimbazi Magharibi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa bodaboda hao, Nasri Mbwilo, amesema wamepokea agizo hilo na wako tayari kuanza kulifanyia kazi mara moja, huku akiwataka waendesha bodaboda kutojihusisha na vitendo vinavyoharibu taswira ya kundi lao.

“Naomba tuendelee kushirikiana ili nasi tupate maendeleo kupitia kazi yetu. Wale watakaokiuka tutawachukulia hatua ili iwe fundisho kwa wengine,” amesema Mbwilo.