CORECU Pwani yawataka wakulima kuchambua korosho kabla ya mnada wa mwisho

By Yasmine Protace , Nipashe
Published at 07:15 PM Dec 19 2025
CORECU Pwani yawataka wakulima kuchambua korosho kabla ya mnada wa mwisho
Picha: Mtandao
CORECU Pwani yawataka wakulima kuchambua korosho kabla ya mnada wa mwisho

Meneja wa Chama Kikuu cha Ushirika wa Korosho (CORECU) Mkoa wa Pwani, Hamis Mantawela, amewataka wakulima wa zao la korosho mkoani humo kuhakikisha wanachambua vizuri korosho zao kuelekea mnada wa mwisho wa msimu huu, ili kuepusha changamoto kwa wanunuzi.

Mantawela ametoa wito huo wakati wa mnada wa sita wa korosho uliofanyika katika eneo la Ikwiriri, mkoani Pwani.

“Mwanzo wa mwezi ujao tunatarajia kufanya mnada wa mwisho wa korosho, hivyo ni jukumu la wakulima kuhakikisha wanachambua vizuri zao lao ili lisilete changamoto kwa wanunuzi,” amesema Mantawela.

Ameeleza kuwa katika mnada wa sita jumla ya tani 345 za korosho zimeuzwa.

Kwa mujibu wa Mantawela, bei za korosho katika daraja la kwanza zilikuwa ni Shilingi 2,110 kwa kilo kwa Misugusugu, Shilingi 2,220 kwa Kibiti na Shilingi 1,910 kwa Rufiji.

Kwa daraja la pili, kilo moja ya korosho iliuzwa kwa Shilingi 1,855 Misugusugu, Shilingi 1,731.59 Kibiti, Shilingi 1,640 Mkuranga na Shilingi 1,874.15 Rufiji.

Ameongeza kuwa hadi kufikia mnada wa nne, zaidi ya Shilingi bilioni 40 tayari zimelipwa kwa wakulima, huku maandalizi ya malipo ya mnada wa tano yakiendelea.

Aidha, amesema ushuru wa vyama vya msingi vya ushirika (AMCOS) wa mnada wa nne tayari umelipwa na kwamba ushuru wa mnada wa tano utalipwa hivi karibuni.

Mantawela amesisitiza umuhimu wa kuendelea kutoa elimu kwa wakulima wanaoendelea kupeleka korosho katika maghala, akiwapongeza wakulima waliopata uelewa ambao wamekuwa wakitoa taarifa mara moja endapo wamewekewa fedha kimakosa.

1

Kwa upande wake, Hassan Mohamed Tunge, kiongozi kutoka Chama cha Msingi cha Ushirika (AMCOS) Kibiti mkoani Pwani, amesema huu ni wakati muhimu kwa wakulima kuhakikisha wanapeleka korosho zao kwenye maghala ya vyama vya ushirika ili ziweze kuuzwa.

Ameeleza kuwa mnada wa mwisho utafanyika mwezi ujao, hivyo mkulima yeyote asiyewasilisha korosho zake kupitia vyama vya ushirika atakuwa amejinyima haki yake mwenyewe.

“Mwezi ujao ni mnada wa mwisho, hivyo wakulima wajitahidi kufikisha korosho zao katika vyama husika ili ziuzwe,” amesema.

Akizungumzia changamoto ya ushiriki mdogo wa wakulima katika minada, Tunge amesema baadhi yao hushindwa kuhudhuria kutokana na kukosa nauli ya kufika maeneo ya minada.

“Kwa mfano, kutoka Kibiti hadi Ikwiriri, nauli ya kwenda na kurudi ni takribani Shilingi elfu 10, jambo ambalo kwa baadhi ya wakulima ni changamoto,” amesema.

Ameongeza kuwa kwa mtazamo wake, vyama vya ushirika vinapaswa kuimarishwa zaidi kwa kuweka televisheni katika ofisi zao ili wakulima waweze kufuatilia minada moja kwa moja na kushiriki kwa kuona mwenendo halisi wa mnada.

2