Waziri wa Madini, Antony Mavunde, ametangaza kufutwa kwa leseni za utafiti wa madini ambazo hazijaendelezwa kwa muda mrefu, hatua inayolenga kuzipangia matumizi mapya na kuwawezesha wachimbaji wadogo kushiriki kikamilifu katika sekta ya madini nchini.
Amesema uamuzi huo unalenga kuongeza ushiriki wa Watanzania katika sekta ya madini na kuhakikisha rasilimali za taifa zinawanufaisha wananchi wengi zaidi.
Akizungumza leo na wachimbaji wadogo wa Mwakitolyo namba tano katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Waziri Mavunde amesema Serikali imechukua hatua hiyo baada ya kubaini uwepo wa leseni nyingi za utafiti zilizomilikiwa na watu binafsi lakini hazikuendelezwa, hali iliyosababisha maeneo makubwa ya ardhi kubaki bila tija.
Mavunde ameeleza kuwa wiki mbili zilizopita Wizara ya Madini ilifuta jumla ya leseni 74 za utafiti wa madini zenye ukubwa wa hekta 700,000 nchi nzima. Amesisitiza kuwa leseni hizo sasa zitapangwa upya na kutolewa kwa wachimbaji wadogo ili waweze kufanya shughuli za uchimbaji kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu zilizopo.
“Serikali hii inalenga kuona wachimbaji wadogo, hususan vijana na akinamama, wanapewa fursa halali za kushiriki kikamilifu katika sekta ya madini. Hatutaki kuona ardhi inashikiliwa bila kuendelezwa huku wananchi wakikosa ajira na kipato,” amesema Mavunde.
Aidha, Waziri Mavunde amewataka wachimbaji wadogo kuzingatia sheria, kanuni na miongozo ya uchimbaji salama, ikiwemo kulinda mazingira, kutumia teknolojia sahihi pamoja na kuchangia mapato ya Serikali kupitia ada na tozo mbalimbali.
Ameongeza kuwa Serikali itaendelea kutoa elimu na usaidizi wa kitaalamu kwa wachimbaji wadogo ili kuwajengea uwezo zaidi, huku akiwatahadharisha kuacha tabia ya kuvamia leseni za watu wengine na kuanzisha shughuli za uchimbaji holela, akibainisha kuwa vitendo hivyo husababisha migogoro na vurugu zisizo na tija.
Kwa upande wake, mmoja wa wachimbaji wadogo wa Mwakitolyo namba tano, Albert Bahame, amempongeza Waziri Mavunde kwa kuchukua uamuzi huo, akisema utawasaidia kupata maeneo halali ya uchimbaji na kupunguza migogoro ya ardhi pamoja na migongano na wamiliki wa leseni kubwa.
Hatua ya kufutwa kwa leseni hizo inaelezwa kuwa sehemu ya mkakati mpana wa Serikali wa kuimarisha usimamizi wa sekta ya madini, kuongeza uwazi na kuhakikisha rasilimali za madini zinatumika kwa maendeleo ya wananchi na taifa kwa ujumla.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED