Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mipango na Uwekezaji), Profesa Kitila Mkumbo, amesema kwamba msingi wa kufanikisha Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 ni ujenzi wa viwanda, na njia bora ya kufikia malengo hayo ni kupitia kongani maalum za viwanda.
Profesa Mkumbo amesema hayo Desemba 10, 2025, wakati wa ziara ya siku moja katika Kongani ya Viwanda ya Kwala, Kibaha. Ameongozana na Waziri wa Viwanda na Biashara Judith Kapinga, Waziri wa Maji Jumaa Aweso, Naibu Waziri wa Nishati Salome Makamba pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge.
Amesema kupitia Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi (TISEZA) kwa kushirikiana na Halmashauri, kongani za viwanda 34 tayari zimesimamiwa na kuanzishwa, hatua inayolenga kurahisisha upatikanaji wa huduma muhimu kwa wawekezaji kama maji, umeme na miundombinu ya usafiri.
Baada ya kukagua viwanda katika eneo hilo, Prof. Mkumbo amesema lengo la ziara hiyo lilikuwa ni kutathmini maendeleo ya uzalishaji na kusikiliza changamoto zinazowakabili wawekezaji ili zipatiwe ufumbuzi wa haraka.
Amezitaja changamoto zilizobainishwa kuwa ni uhaba wa umeme, upungufu wa maji, na hitaji la kituo cha reli ya Mwendokasi (SGR) katika eneo la kongani. Serikali, amesema, tayari imechukua hatua ambapo katika wiki mbili zijazo kongani hiyo itapatiwa ongezeko la megawati 4 za umeme, huku suluhu ya kudumu ikifanyiwa kazi kupitia kituo cha umeme cha Chalinze.
Kuhusu maji, Waziri wa Maji Jumaa Aweso ametoa maelekezo ya kuharakisha mradi wa maji wenye thamani ya Sh bilioni 25 ambao utapelekea huduma ya uhakika katika eneo la viwanda la Kwala.
Aidha, Profesa Mkumbo amesema suala la ombi la kituo cha SGR tayari lipo katika utekelezaji kufuatia maelekezo ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, na Mkuu wa Mkoa wa Pwani amelipatia kipaumbele maalum.
Akiangazia maendeleo ya uwekezaji, Prof. Mkumbo amepongeza juhudi za Kongani ya Sino Tan – Kwala Industrial Park – kwa kuwa na kiwanda kikubwa cha uzalishaji vifaa vya umeme wa jua (solar power) na kiwanda cha chuma, ambavyo ni vya kwanza kwa ukubwa na aina yake nchini.
Amesema viwanda hivyo vitachochea ukuaji wa uchumi na kuongeza ajira kwa Watanzania, ikiwa ni matokeo ya uwekaji wa mazingira rafiki ya uwekezaji yanayoendelea kusimamiwa na Rais Samia.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Sino Tan Industrial Park, Janson Huang, amesema wanapanga kujenga zaidi ya viwanda 200, ambapo 20 tayari vimejengwa, lakini changamoto za umeme, maji na kituo cha reli zimeathiri kasi ya ukuaji wao. Kwa sasa wanapata megawati 50 pekee dhidi ya mahitaji ya megawati 70, na wanahitaji takriban lita milioni 1.5 za maji kwa siku.
Hata hivyo, Huang ameishukuru TIC kwa msaada mkubwa wanaotoa katika kufanikisha miradi hiyo na kuahidi kuendelea kuongeza viwanda pindi changamoto za huduma muhimu zitakapopatiwa ufumbuzi.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED