Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mkoa wa Tabora imekamilisha ujenzi wa daraja la mawe lenye urefu wa mita 60.3 katika barabara ya Sasu–King’wangoko–Seleli, Wilaya ya Kaliua, hatua inayolenga kuboresha miundombinu ya usafiri na kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa eneo hilo.
Akizungumza kuhusu mradi huo, Meneja wa TARURA Mkoa wa Tabora, Mhandisi Lusako Kilembe, amesema ujenzi wa daraja hilo umegharimu shilingi milioni 526.7 zilizotokana na ufadhili wa Benki ya Dunia kupitia mradi wa RISE, unaolenga kuondoa vikwazo vya miundombinu hususan katika maeneo ya vijijini.
Mhandisi Kilembe amesema daraja hilo linashika nafasi ya pili kwa urefu kati ya madaraja ya mawe nchini, likitanguliwa na daraja la aina hiyo lililopo Wilaya ya Busega, Mkoa wa Simiyu, lenye urefu wa mita 80.
“Ujenzi wa daraja hili umeokoa shilingi bilioni 1.27, kwani endapo tungejenga daraja la kawaida la zege na nondo tungetumia takribani shilingi bilioni 1.8. Daraja hili linatarajiwa kuchochea kwa kiasi kikubwa uchumi wa wananchi,” amesisitiza.
Ameeleza kuwa utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 95, ambapo kazi za ujenzi zinatekelezwa na kampuni ya M/S Mgalang’ombe Co. Ltd ya Mkoa wa Tabora, na unatarajiwa kukamilika kikamilifu mwishoni mwa mwaka huu.
Aidha, amesema ujenzi wa daraja hilo ni sehemu ya mkakati wa Serikali ya Awamu ya Sita wa kuhakikisha barabara zinapitika mwaka mzima, kupunguza changamoto za usafiri hususan kipindi cha mvua, kurahisisha usafirishaji wa mazao, kukuza biashara, pamoja na kuboresha upatikanaji wa huduma za kijamii zikiwemo afya na elimu.
Mhandisi Kilembe ameongeza kuwa mradi huo utaimarisha mawasiliano kati ya Mikoa ya Tabora na Shinyanga, hatua itakayosaidia kuharakisha maendeleo ya wananchi wa maeneo husika.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED