KESHO ni maadhimisho ya sherehe za Nane Nane na bila shaka wakulima wametumia fursa hiyo kujifunza na kupata maarifa ya kilimo ili kuongeza tija na uzalishaji kupitia wataalamu mbalimbali wanaopatikana kwenye maonesho hayo.
Hayati Julius Kambarage Nyerere, Rais wa Kwanza wa Tanzania alikuwa na kaulimbiu ya kilimo ni uhai na ndio maana serikali imeendelea kuwekeza nguvu katika kuboresha sekta hiyo.
Serikali imewekeza nguvu kubwa katika kuboresha sekta hiyo, hivyo maonesho hayo sio mahali pa kupita tu, bali ni darasa wazi kwa kila mmoja anayetaka kuboresha shughuli zake za kilimo.
Kadhalika, yamekusanya wataalamu wa kilimo, watafiti, na kampuni za pembejeo za kilimo ili kutoa elimu na teknolojia mpya zinazoweza kubadilisha maisha ya wakulima.
Matumizi ya mbegu bora, mbolea, na mbinu za kisasa ndio njia pekee ya kukabiliana na changamoto za kilimo zinazowakabili.
Maonesho hayo pia yamewakutanisha wajasiriamali mbalimbali ambao wameonesha bidhaa zenye ubora na viwango hali inayoonesha kuna jitihada kubwa za kupenya kwenye masoko ya ndani na nje ya nchi.
Ubunifu mkubwa ulioneshwa na wanazalisha bidhaa mbalimbali umeongeza thamani na ubora zaidi.
Maadhimisho haya hukutanisha wakulima wakubwa na wadogo kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania ambao hubadilishana uzoefu na kupata elimu ya kilimo bora.
Sherehe hizo hutoa fursa kwa wakulima wadogo kujifunza kutoka kwa wakubwa katika lengo la kukifanya kilimo nchini kuwa na uzalishaji bora.
Sherehe hizi hubadili mandhari ya maonesho na kufanya kuonekana kuwa kijani kutokana na mazao yanayostawishwa kwa kuzingatia njia bora za kilimo.
Kilimo cha kisasa na kile cha asili kinatofauti kubwa. Cha asili kilikuwa kikizingatia mbegu za asili ambazo pamoja na mazao yake kuwa na ladha nzuri, lakini hayatoi mazao mengi.
Kwa kilimo cha kisasa ambacho kinatumia mbegu za kisasa zinazozalishwa kisasa, zinatoa mazao mengi na katika sehemu ndogo ya ardhi na kwa muda mfupi.
Kumekuwa na masomo ya mashamba darasa ambayo huonesha jinsi kilimo cha kisasa kinavyosaidia kuzalisha mazao mengi na kwa muda mfupi hali inayosaidia kukabiliana na tatizo la njaa.
Sikukuu ya Nane Nane huonesha pia ufugaji wa kisasa kuanzia wa kuku hadi wanyama na tofauti kubwa huonekana kati ya ule wa asili na wa sasa.
Kwa ujumla maonesho ya Nane Nane hutoa fursa kubwa ya wakulima kujifunza mpaka kwenye ufugaji wa samaki ambao kwa sasa umepamba moto na kutoa matokeo bora.
Wakulima hufundishwa jinsi ya kufuga kwa kutumia eneo dogo, ambalo hutoa mazao mengi na kuleta faida kubwa kwa mfugaji.
Kuna utalaamu wa kufuga samaki kwa kutumia matangi ya maji ambayo hukatwa katikati na kuokoa mtu kutumia eneo kubwa.
Ufugaji huu pia humsaidia mtu asiyekuwa na nafasi ya kutosha kwenye eneo lake kuendelea kufaidi matunda ya ufugaji na kupata kipato kinachomwezesha kumudu maisha ya kila siku.
Kwa wakulima na wafugaji siku ya Nane Nane ni muhimu kwao kuendelea kupata ujuzi na kubadilishana uzoefu kwa wenzao waliopiga hatua na kufikia nafasi nzuri.
Kilimo kinalipa na kinaweza kubadili maisha ya mtu bila kutegemea ajira kutoka serikalini au kwenye kampuni binafsi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED