Maendeleo bora mara zote kuna elimu bora imesukwa nyuma yake

By Yasmine Protace , Nipashe
Published at 01:58 PM Aug 21 2025
Wananchi waliopo maeneno ya pembezoni wapewe kipaumbele katika elimu sekta zote
Picha: Mtandao
Wananchi waliopo maeneno ya pembezoni wapewe kipaumbele katika elimu sekta zote

MTU anapoenda masomoni, anahitaji elimu na ujuzi ambazo mara zote, zinaenda kama jozi moja

Hiyo humkamilisha mtu awe mtoto au katika elimu ya utu uzima, jibu likibaki palepale kwamba kuna dhana ya kuwekezwa ujuzi anayesoma mahali aliko.

Tafsiri inayochukua nafasi ni kwamba,huyo mtu anapomaliza masomo yake, aweze kujiendeleza kimaisha kupitia ujuzi huo.

Kumeshuhudiwa watoto wengi wanapomaliza shule au vyuo, baadhi yao wanakaa nyumbani wakisubiri matokeo,ili wapate mwelekeo kwa hatua inayofuata.

Huwa kuna wengine kulingana na mazingira ya malezi, pia picha za uchumi wanakoishi, wanapomaliza shule huenda mbali kufanya kazi za ndani wakisaka kujiingizia kipato wajikimu maisha yao.

Lakini kama watoto wanakuwa na ujuzi ambao wameupata kutoka shule au vyuoni, ni kwamba wanapomaliza masomo yao, daima watajishughulisha kupitia maarifa waliyoyapata shuleni, hali itakayowasaidia wasikae vijiweni.

Pia, ujuzi unawafanya watoto kujiajiri na kuacha kukaa vijiweni maana wana jicho la kutambua na stadi ya kumudu nini cha kukifanya. 

Vilevile huko huko shuleni, kuna ya ziada kwamba dhana ya kuwa na elimu ya maisha shuleni, inatoa maana pana zadi kwa kusaidia wanafunzi wanapofanya majukumu ya uzalishaji mali.

Hapo nina maana wanafunzi wanatengeneza vitu vingi ambavyo awali havikupatikana mitaani. Walikuwa hawajaingia katika mfumo wa kujiinua kipato na kufanya shule kuingia gharama kubwa kutafuta, watu wa kupamba.

Nakumbuka Hayati, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, akaipa elimu kipaumbele katika mfumo wake wa maendeleo, akiamini kuwa nyenzo inayowavusha Watanzania kutoka waliko.

Ni mada inayodumu hadi sasa, ikiendelezwa na mkuu wa shule ya sekondari mojawapo kwenye mahafali yanayomhusu mwaka huu, akitamka: 

"Tunawafundisha wanafunzi kupika mapishi ya aina mbalimbali, ikiwamo upambaji na kutengeneza sabuni na viungo vya chai. Lengo la kufanya hivyo ni kuwajenga wanafunzi juu ya kuweza kujiajili na kujiongezea kipato."

Akaongeza kuwa wanafunzi wanaohitimu elimu ya msingi na sekondari, wanalazimika kukaa nyumbani huku akisubiri matokeo na wao shule walipobaini hilo, wakaona ni vyema wakiwaandalia elimu ya maisha kuwakomboa kimaisha.

Kwa mujibu wa mkuu huyo wa shule, ni kwamba wanajamii tunaporudi na kuona watoto wetu wanakosa mwelekeo wa nini cha kufanya, ni ishara mahali hapo kuna matatizo na elimu haijafanya kazi yake vilivyo.

Najua kumeshafanyika maboresho mengi ya kitaaluma na bado kuna mahitaji ya nini kifanyike yanashughulikiwa.

Pia, tunafahamu kuna hatua kubwa zinachukuliwa katika kuboresha mitaala ya nchi, moja ya mitazamo ni kuziba pengo tajwa, hali kadhalika kuwaongezea uwezo na uelewa wale wanaosoma.

Najua ni kazi ngumu na si ya kupata majibu ya leo, bali inaangukia mchakato wa aina fulani. 

Katika nyendo zake Hayati Mwalimu Nyerere, alitenda yote, kila mradi uliendana na elimu nyuma yake, mathalan katika mipango ya elimu, pia kukawapo afya.

Mwalimu Nyerere hata kuna wakati akachukua hatua kuandaaa maelekezo ya elimu kupitia vitabu vyake kama vile cha Ujamaa (Kiswahili) na Ujamaa Essay cha Kizungu.

Hotuba zake hakuacha kando nadharia taaluma na ndio maana tukasikia katika hotuba mathalan za kilimo, akinena kama “mpunga tunapanda nchi moja moja.”

Kusheheni kwa ngazi za maendeleo nchini kwa kasi, mfano baada ya miaka 10 ya uhuru makubwa kufikiwa, kuna uhusiano wa moja kwa moja na msaada wa sekta ya elimu leo hii.