Stars sasa fanyeni kweli robo fainali

Nipashe
Published at 12:59 PM Aug 18 2025
Stars sasa fanyeni kweli robo fainali
Picha: Mtandao
Stars sasa fanyeni kweli robo fainali

TIMU ya Taifa, Taifa Stars, imetinga kwa kishinda robo fainali ya michuano ya Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani ya nchi (CHAN), ikiongoza kundi lake B kwa pointi 10.

Hiyo ni baada ya kushinda michezo mitatu na kutoka sare mmoja ambao ni wa mwisho kwenye hatua ya makundi dhidi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Hatua inayofuata sasa kwa Stars ni kucheza robo fainali ya michuano hiyo, ambapo kocha wake Mkuu, Hemed Suleiman 'Morocco', amesema wameweza kutimiza malengo yao mawili kati ya matatu waliyojiwekea.

Kwa mujibu wa Morocco wameshindwa kutimiza lengo moja tu ambalo ni kushinda mechi zote za makundi, lakini akasema hayo mawili ya kuongoza kundi na kufuzu robo fainali ni kipaumbele zaidi.

"Tulikuwa na malengo matatu, mawili yalikuwa muhimu sana, moja lilikuwa ni la kuweka rekodi tu. Kwanza ni kutinga hatua ya robo fainali limetimia, pili kuongoza kundi limetimia, kwahiyo utaona yale muhimu tumeyatimiza kwa asilimia 100," alisema Morocco.

Stars ilianza michuano hiyo kwa kuifunga Burkina Faso mabao 2-0, ikashinda bao 1-0 dhidi ya Maritania, ikaitandika Madagascar, mabao 2-1, kabla ya kung'ang'aniwa kooni na Afrika ya Kati.

Morocco akabainisha kuwa sasa wanarudi kwenye uwanja wa mazoezi, ili kujiweka sawa na hatua ya robo fainali, ambayo alisema ni ngumu, lakini wamejipanga.

Hivyo, kwanza tunaipongeza Stars kwa kutinga hatua hiyo ya robo fainali ikiwa ni ya kihistoria, kwani hapo mwanzo haikuwahi kuifikia.

Pili, tunaitaka Stars sasa kwenda kufanya kweli kwenye hatua hiyo ili kujihakikishia nafasi ya kutinga nusu fainali na hatimaye fainali na ikiwezekana kulitwaa kombe hilo.

Tunasema hivyo kutokana na ukweli kwamba, kikosi cha Stars katika michuano hiyo kimeonekana kuwa na kiwango bora kabisa, hivyo tuna imani kubwa kitaweza kufikia malengo yake.

Pamoja na motisha kubwa inayotolewa na serikali kwa kuwaunga mkono wachezaji kuwazawadia fedha kwa kila bao wanalolipata, tunaamini hamasa na ari itakuwa kubwa zaidi kwenye hatua hiyo.

Tunawakumbusha Stars kwamba, wanaipeperusha bendera ya Taifa, hivyo lazima wapambane kwa bidii uwanjani ili kupata matokeo mazuri.

Michuano hii ikiwa inafanyika kwenye ardhi yetu kwa ushirikiano wa Kenya na Uganda, tunaona hiyo ni fursa nzuri kwetu kuweza kulibeba kombe hilo kwa mara ya kwanza.

Ikumbukwe kwamba, Stars inacheza kwenye ardhi yake ikipata sapoti kubwa ya mashabiki, ambao kwa kawaida huitwa ‘mchezaji wa 12’ wana kila sababu kupambania nchi.

Pia ikumbuke kuwa, hatua hiyo itazikutanisha timu zenye kiwango cha juu, baada ya nyingine kutolewa kwenye hatua ya makundi.

Hivyo, tunaamini benchi la ufundi litatumia muda huu kukiandaa kikosi vizuri na kwa kuangalia wapi kuna mapungufu na kuyafanyia kazi.

Pia wachezaji wenyewe, wanatakiwa kuzingatia maagizo ya benchi lao la ufundi kwa kutekeleza kile walichojifunza kwenye mazoezi na kukifanyia kazi wakati wa mechi za hatua hiyo.

Stars ina kila sababu ya kucheza kwa kijiamini, kwani Watanzania wapo nyuma yao kwenye sapoti ili mwisho wa siku tuweze kulibeba kombe hilo.

Pia wachezaji watumie nafasi hiyo kama sehemu ya kujiuza, kwani michuano hiyo inafuatilia na mataifa makubwa ya soka Ulaya na kwingineko.

Hivyo, wakati wanaipambania nchi, pia huo unakuwa wakati wao wa kujitangaza zaidi.

Tunawatakia kila la heri Stars kwenye hatua hiyo ya robo fainali.