Rushwa ni adui wa haki, usitoe wala kupokea

Nipashe
Published at 11:48 AM Aug 26 2025
Mzani ni ishara ya haki kwa pande mbili
Picha: Mtandao
Mzani ni ishara ya haki kwa pande mbili

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), imeendelea kusisitiza umuhimu wa wananchi kuepuka kuingia kwenye vishawishi vya kutoa na kupokea rushwa katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu ili kupata viongozi bora.

Pia, wanasheria wa taasisi hiyo wametakiwa kuhakikisha wanafuatilia uchaguzi ili kupata viongozi ambao hawatokani na rushwa.

Taasisi hiyo imesisitiza kuwa viongozi kuanzia ngazi ya diwani ni wadau wakubwa wa TAKUKURU kwa kutoa taarifa za rushwa kwenye aina yoyote ya tukio ambalo litaonekana kuwa na viashiria vya rushwa.

Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Crispin Chalamila, amekumbusha kuwa ni jukumu la wanasheria na watumishi wa taasisi hiyo kufuatilia kwa makini uchaguzi mkuu ili viongozi watakaopatikana wawe waliochaguliwa na wananchi.

Kila mtu anatakiwa kufuatilia uchaguzi kwa wivu mkubwa ili kupata wadau wasafi na wanaopendwa na watakaochaguliwa na wananchi, wasiofaa wasipite. Hiyo ni rai ya Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU.

Taasisi hiyo ni wadau muhimu kuhakikisha washindi wanaopatikana ni wale wanaokubalika kwenye jamii.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi mkuu huyo msisitizo wao kwasasa ni kuzuia rushwa na wanaendelea kujiimaarisha kwenye umma kwa kutoa elimu kuzuia rushwa.

 TAKUKURU inatekeleza majukumu yake ya kuufanya uchaguzi ujao usiwe na vitendo vya rushwa kuanzia kwa wananchi wenyewe hadi wagombea. Inahimiza wananchi kuepuka vitendo vya rushwa na kutokubali kuchagua viongozi wanaotoa rushwa kwa sababu hawana msaada wowote kwao kwa kipindi chote cha miaka mitano ijayo. Hizo ni salamu na ujumbe ambao taasisi hiyo imetaka uwafikie wananchi.

Wakati Uchaguzi Mkuu ukikaribia, TAKUKURU imefanya mafunzo, semina na warsha mbalimbali kwa wadau ili nao waende kuelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kufanya uchaguzi kwa umakini kupata viongozi bora wanaowajibika. 

“Rushwa ni saratani kubwa ambayo haiwezi kukabiliwa na sheria au taasisi moja; ni suala la ushirikishwaji wa wadau wote,” Taasisi hiyo inasisitiza.

Rushwa katika uchaguzi ni tishio kwa msingi wa demokrasia kwa kuwa huathiri uamuzi wa wapigakura, huharibu uwazi wa mchakato wa uchaguzi na kuzaa viongozi wasiowajibika.

Rushwa katika uchaguzi si tu kwamba inapotosha mwelekeo wa uamuzi wa wananchi, bali pia hupunguza imani ya wananchi kwa vyombo vya uchaguzi na serikali kwa ujumla. Mbaya zaidi, hujenga mazingira ya uhasama, migawanyiko ya kijamii na kuvuruga amani ya taifa.

Vyama vya siasa kama wadau wa uchaguzi, vina nafasi ya kipekee katika juhudi za kutokomeza vitendo vya rushwa. Ndani ya vyama ndipo panapotoka wagombea, mapambano dhidi ya rushwa kwenye uchaguzi hayawezi kufanikiwa pasipo ushiriki wa kweli na wa dhati kutoka katika vyama vyenyewe.

Taasisi hiyo iko kazini katika suala la rushwa kuelekea Uchaguzi Mkuu ambao kwa sasa zinahesabiwa siku. Vyombo vya habari ni silaha muhimu dhidi ya rushwa wakati wa uchaguzi vinapofanya kazi kwa uadilifu na ujasiri.

Kwa mujibu wa “Mkakati wa Taifa Dhidi ya Rushwa na Mpango wa Utekelezaji wa Awamu ya Tatu 2017-2022 (NASCAP III)”, vitendo vya rushwa vinatafsiriwa kuwa ni kutoa, kupokea au kushawishi moja kwa moja kutolewa au kupokelewa kwa kitu chochote cha thamani kwa maslahi au matumizi binafsi, ili kupindisha utaratibu uliopo katika utoaji wa maamuzi, au kupata faida ya kitu au jambo ambalo hakustahili.
 
 Rushwa ni jambo ambalo limejadiliwa na kuwekewa mikakati katika ngazi mbalimbali za kidunia, kikanda na hata katika nchi moja moja. Kwenye Ajenda 2063 ya Afrika Tuitakayo, Lengo namba 3 inalenga kuwa na Afrika yenye utawala bora, demokrasia, inayoheshimu haki za binadamu, usawa na utawala wa sheria.