Ulaji usiofaa tishio kwa kizazi kipya, tuchukue hatua sasa

Nipashe
Published at 01:11 PM Aug 19 2025
Mlo kamili huimarisha afya
Picha: Mtandao
Mlo kamili huimarisha afya

TAARIFA iliyotolewa na wataalamu wa lishe kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), inatoa taswira ya kutisha kuhusu mwelekeo wa kiafya wa kizazi kipya cha Watanzania – vijana na watoto – kutokana na kuongezeka kwa ulaji usiofaa.

Ulaji wa vyakula vyenye mafuta mengi, sukari nyingi na chumvi kupita kiasi umeanza kuwa chanzo kikuu cha magonjwa yasiyoambukiza kwa kundi ambalo awali lilionekana kuwa salama.

Hali hii si tu inatishia ustawi wa afya ya jamii bali pia inahatarisha nguvukazi ya taifa kwa siku zijazo. Kizazi chenye afya hafifu leo ni mzigo kwa familia, taifa na mifumo ya huduma za afya kesho.

Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) za mwaka 2024 zinaonesha kuwa asilimia 70 ya vifo vyote duniani vinatokana na magonjwa yasiyoambukiza kama vile kisukari, shinikizo la damu, saratani na magonjwa ya moyo.

Kinachotia wasiwasi zaidi ni kwamba magonjwa haya kwa sasa yameanza kuwaathiri vijana na hata watoto wadogo, tofauti na ilivyokuwa awali ambapo yaliambatana zaidi na uzee.

Tatizo haliko kwenye upatikanaji vyakula, bali ni katika tabia na mitindo ya maisha. Katika baadhi ya jamii, hata vijijini ambako vyakula vya asili vinapatikana kwa wingi, watu wengi wameanza kupendelea vyakula vya haraka (fast foods), vyenye sukari nyingi, mafuta mengi na visivyo na virutubisho vya kutosha. 

Vyakula hivi huuzwa kwa wingi mitaani, kwenye maduka na hata shuleni bila udhibiti wa kutosha. Hali hii inahatarisha kizazi kilicho shuleni sasa na kizazi kijacho.

Vijana wengi wa mijini na hata baadhi ya watoto, wameingia katika maisha ya kukaa muda mrefu bila kufanya mazoezi ya mwili, wakishinda mbele ya runinga, simu au kompyuta, wakila bila mpangilio. 

Hii imechangiwa pia na kupungua kwa fursa za michezo shuleni na maeneo ya wazi ya kuchezea watoto, kutokana na ukuaji holela wa miji.

Kwa mujibu wa Mhadhiri Msaidizi kutoka SUA, Hasna Bofu, hali hii imechochewa pia na upungufu wa elimu ya lishe kwa jamii. Elimu ya lishe haipaswi kuwa ya wataalamu wa afya peke yao, bali inatakiwa kufundishwa shuleni kuanzia shule za msingi, ijumuishwe kwenye kampeni za kitaifa kama suala la kitaifa.

Tunasema, hii siyo kazi ya Wizara ya Afya pekee. Wizara ya Elimu, TAMISEMI, Wizara ya Habari na hata Serikali za Mitaa, zina wajibu wa kushirikiana kuhakikisha elimu ya lishe inawafikia watu wote – mijini na vijijini. 

Mafanikio ya serikali katika kupunguza utapiamlo kutoka asilimia 38 hadi 31 ni hatua ya kupongezwa, lakini kama anavyosema Dk. Hadijah Mbwana wa SUA, juhudi hizo haziwezi kufaulu kikamilifu bila kushughulikia mabadiliko ya tabia za ulaji.

Ni wakati sasa wa serikali kuanzisha na kusimamia kampeni ya kitaifa ya lishe bora, kama ilivyofanya kwa kampeni za chanjo, malaria na Ukimwi. 

Kampeni hizo zinaweza kuhusisha vipindi vya redio na televisheni, machapisho shuleni, semina kwa wazazi na walimu, na hata mabalozi maarufu wa lishe bora.

Pia ni muhimu kwa mamlaka zinazohusika kudhibiti biashara ya vyakula visivyo na ubora, hasa vinavyouzwa karibu na shule. Hatua madhubuti zichukuliwe kuhakikisha watoto hawanunui bidhaa hatarishi kama soda, pipi nyingi na vyakula vya kukaangwa mara kwa mara.

Sambamba na hayo, miundombinu ya michezo iimarishwe katika shule na mitaa ili kuwahamasisha watoto kushiriki mazoezi. Walimu wa michezo warejeshwe shuleni kwa nguvu mpya, si kwa sababu ya michezo pekee bali kwa afya ya taifa.

Ni wajibu wa kila mzazi, mlezi na mwalimu, kuhakikisha watoto wanapewa lishe inayofaa kwa ukuaji na maendeleo yao ya kimwili na kiakili. Taifa lenye watoto na vijana wenye afya ni taifa lenye matumaini ya maendeleo ya kweli.