Uchaguzi Mkuu usitumike ‘kuposti’ habari potofu, upotoshaji

Nipashe
Published at 02:03 PM Aug 21 2025
Upigaji kura ni hatua muhimu kupata viongozi
Picha: Mtandao
Upigaji kura ni hatua muhimu kupata viongozi

IKIWA imebaki miezi miwili na siku kadhaa, Watanzania kufanya uamuzi wa kuchagua viongozi wanaowataka kipindi hiki cha kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu kisitumike kusambaza habari potofu, upotoshaji na zenye chuki.

Sasa hivi Watanzania wengi wanamiliki vifaa vya aina tofauti vya mawasiliano ambavyo wengine huvitumia kwa kusambaza habari ambazo huzua mtafaruku ama kuwachafua watu wengine.

Mitandao ya kijamii inatumika sana kwa sasa kusambaza habari hizo na katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi hasa kipindi cha kampeni ndipo mambo mengi ya upotoshaji hujitokeza.

Kuna ambao wanarusha habari potofu kwa kisingizio cha kutojua sheria, lakini hiyo sio sababu ya mtu kutotiwa hatiani kwa kutenda kosa hilo.

Wataalam wa masuala ya mawasiliano wanasema kuwa mtandao unaotumika kusambaza kwa kasi habari za upotoshaji ni wa WhatsApp. Mtu anapokutana na picha mjongeo au picha mnato au habari yoyote husambaza kwenye magrupu mengine ili tu aonekane yeye ni wa kwanza kusambaza habari hiyo bila kujua athari yake.

Ni muhimu kufahamu kuwa wale wanaofanya hivyo bila kujua uhalisi wa habari anayoisambaza anaweza kuishia gerezani.

Wote tunafahamu kuwa matumizi ya teknolojia ya mawasiliano duniani yameleta mafaniko na athari kutokana na watu wanavyoitumia.

Mafanikio yaliyopatikana ni watu kupata fursa nyingi za kujifunza kupitia mitandao hiyo hasa inapotumika vizuri na wengine kutengeneza ajira ambazo zinawapatia vipato.

Teknolojia hiyo pia imesaidia masomo na mikutano kufanyika mitandaoni badala ya kukutana uso kwa uso na kuokoa gharama za watu kusafiri kutoka nchi moja kwenda nyingine.

Hayo ndiyo matumizi mazuri ya teknolojia ambayo yanaleta tija kwa watu na nchi pia.

Hata hivyo, baadhi ya watu wanaitumia vibaya teknolojia hiyo kwa kurusha vitu vinavyozua taharuki na kuchafua watu wengine.

Katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu, watu hutumia mitandao hiyo kuchafua wengine hasa wanapoona wamejitokeza kugombea nafasi ya uongozi.

Waathirika wakubwa kwenye mitandao ni wanawake ambao kutokana na kuchafuliwa huvunjika moyo na kujitoa katika lengo alilokusudia.

Dunia inakwenda na mabadiliko ya teknolojia ni kurahisisha kazi na kupunguza muda unaotumika kwa binadamu kuifanya kazi hiyo.

Pia, wapo wanaotumia picha za matukio ya zamani na kuzitengeneza ili mradi kuwachafua watu na kuwaharibia wasifu wao. Teknolojia hii isitumike kuharibu badala yake itumike kujifunza mambo yenye maendeleo kwa faida yao na taifa.

Mamlaka ya Mawasiliano Nchini (TCRA), imeeleza wazi kuwa inaendeleza jitihada za kupambana na kudhibiti uhalifu mitandaoni, ikiwamo huduma za kifedha kutokana na kuongezeka mifumo mipya ya mawasiliano ya teknolojia.

Kwa nchini Tanzania, wafanyabiashara, wajasiriamali wamerahisishiwa kazi kwa kutumia teknolojia ya mawasiliano ambapo kwa sasa wanaweza kutuma pesa nje ya nchi na kuletewa bidhaa wanazotaka badala ya kusafiri hali inayowapunguzia gharama.

Katika matumizi ya teknolojia hii pia kunahitajika uaminifu wa hali ya juu ndio maana hata TCRA ikiwa ni mdhibiti wa matumizi mabaya ya mawasiliano imekuwa ikiingilia kati kila inapoona mambo hayaendi sawa.

Kuna wanaotumia teknolojia hiyo pia kwa malengo mabaya ya kuwachafua watu wengine kwenye mitandao.

Hali hiyo imekuwa ikishamiri kwenye mitandao ya kijamii kiasi cha kuharibu hali ya hewa na wengine wanaochafuliwa huathirika kisaikolojia.

Duniani mabadiliko ya kiteknolojia hayawezi kuepukika, hivyo ni muhimu wadhibiti wa uhalifu mitandaoni kuwa makini kudhibiti hali hiyo ili kuepuka matumizi mabaya.