TIMU ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, imetuheshimisha wabongo. Hivyo ndivyo unavyoweza kusema baada ya kufanikiwa kufika hatua ya robo fainali ya michuano ya Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN), inayoendelea hapa nchini, Kenya na Uganda.
Pamoja na kutolewa Ijumaa iliyopita kwa bao 1-0 dhidi ya timu ya taifa ya Morocco, lakini ilicheza soka safi na kilichotokea ni kwa sababu chache tu za kukosa kutumia nafasi zilizopatikana.
Stars imetolewa kuheshima kwa kufunga bao 1-0 kwa tabu na timu ya Morocco, moja ya vikosi ambavyo huko nyuma nilitabiri kuwa vitaleta shida kwenye michuano hii.
Ni kwa sababu kama ilivyo Stars, ni moja ya timu inayotumia wachezaji wengi wa Ligi Kuu ya ndani.
Ilikuwa na wachezaji wengi wa RS Berkane, Wydad Casablanca, Raja casablanca na wachache wa FAR Rabat.
Mchezaji aliyefunga bao pekee kwenye mchezo wa Ijumaa, Oussama Lamlioui, ndiye alifunga bao la pili kwenye mchezo wa fainali ya kwanza kati ya Simba dhidi ya RS Berkane uliochezwa nchini Morocco, Mei 17, mwaka huu, timu hiyo ya Tanzania ikipoteza mabao 2-0.
Oussama ndiye kinara wa mabao kwenye michuano hii ya CHAN inayoendelea, akiwa ameshapachika mabao manne mpaka sasa.
Hapa unaweza kuona kuwa Stars ilicheza na timu ya aina gani. Haikucheza na timu ya kawaida kawaida tu.
Ikumbukwe kuwa Morroco ni moja kati ya timu mbili ambazo zimetwaa michuano hii mara nyingi zaidi kuliko nchi zingine.
Morocco na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo zimetwaa michuano hii mara mbili kila moja.
DR Congo ilitwaa taji hilo, 2009 na 2016, wakati Morocco ikifanya hivyo, 2018 na 2020.
Kwa hili inaonesha kuwa kama Stars isingepita njia ya Morocco, ingeweza kufika hatua hata ya fainali.. Hata mechi iliyochezwa ilikuwa na kiwango cha fainali.
Niwapongeze wachezaji wa Stars kwa kupambana kiasi cha kupoteza mechi kwa heshima. Imepoteza kwa timu bora kabisa Afrika.
Niwapongeze wachezaji kwa kuliongoza Kundi B kwa mara ya kwanza kwenye historia ya michuano hiyo, ikifanya hivyo bila kupoteza mchezo wowote.
Pongezi pia ziende kwa Kocha Mkuu, Hemed Morocco, na wasaidizi wake, Juma Mgunda, Jamhuri Kihwelo 'Julio' kwa kukinoa kikosi hicho na kuonekana kuwa tishio kwenye fainali hizo.
Pongezi kubwa ziende kwa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, chini ya Profesa Palamagamba Kabudi na Naibu wake, Hamisi Mwinjuma, ambaye walikuwa bega kwa bega na wachezaji, benchi la ufundi pamoja na Shirikisho la Mpira wa Miguu Nchini (TFF), kuhakikisha kila kitu kinaenda sawa hadi Stars ilipofikia. Hata baada ya Stars kutolewa, lakini wanaendelea kuhakikisha michuano hiyo inafanyika kwa hali ya ile ile ya usalama, amani na utulivu kwa timu zilizobaki kama mwenyeji wa michuano hiyo.
Pongezi za kipeke kabisa ziende kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa kuhakikisha michuano hii inafanyika hapa nchini, pamoja na kuwapa hamasa wachezaji, benchi ya ufundi kwa kutoa zawadi ya pesa ya 'goli la mama', pale timu inapopata ushindi, lakini si hivyo tu, kutoa pesa kwa ajili ya motisha kabla hata mechi haijachezwa.
Ikumbukwe kuwa kabla ya mchezo dhidi ya Morocco, Rais aliwapa wachezaji pamoja na benchi la ufundi kiasi cha Sh. Milioni 200 kwa ajili ya kutoa hamasa hali iliyowafanya wachezaji kupambana hadi tone la mwisho la damu.
Juhudi zote hizi zilizooneshwa kuanzia Rais na serikali yake, pamoja na wadau wote wa soka, imewafanya hata Shirikisho la Soka Afrika (CAF), kutojutia kuileta michuano hii hapa nchini, wakiona kabisa pia AFCON 2027, itafanyika pia kwa mafanikio makubwa.
Nikirudi kwa kile kilichofanywa na Stars, nina uhakika kuwa AFCON inayokuja tukiunganika na wachezaji wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi, tutafanya vizuri zaidi. Hongera Serikali, Hongera Stars, imetuheshimisha.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED