Ukatili huu mbona unazidi?

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 01:06 PM Aug 27 2025
Njiwa ni ishara ya amani
Picha: Mtandao
Njiwa ni ishara ya amani

KUMEKUWA na matukio mengi kwenye jamii mijini na vijijini yanayohusisha wanaume na wanawake kufanya maamuzi kwa sababu ya hasira, chuki au kukaa na vinyongo moyoni.

Matokeo yake wahusika wanajikuta wakitumbukia katika maamuzi magumu na ya kikatili kama mauaji ya wenza wao, watoto au wenyewe kujitia kitanzi.

Huenda wengi wamekuwa wakidhani ni udhaifu kusema matatizo yao binafsi na yale yanayowahusisha wenza wao na hapo ndipo kesi za mauaji zinapoleta simanzi kwenye mioyo yao na Watanzania wengine.

Matokeo yake hawatafuti ushauri na nasaha na kama wanavyosema mwanzo wa ngoma ni lee, mauaji haya yalianza kama kipele ila sasa ni jipu linalohitajika kutumbuliwa kwa upasuaji mkubwa hospitalini.

Katika siku za hivi karibuni, ripoti na taarifa kuhusu kuenea kwa vitendo vya mauaji yanayohusishwa na wivu, chuki na makosa kwenye mapenzi zimezua taharuki, mjadala lakini pia hofu.

Siku za nyuma hayakusikika sana matukio hayo, ila kwa sasa yameonekana kushamiri. Swali la kujiuliza ni hili ni kwanini mauaji haya? Je nini kinachoendelea kwenye jamii?

Kumekuwa na matukio ya kujiua, wanawake na wanaume wakijinyonga, lakini pia wanaume kuuwa wake na wapenzi wao, watoto lakini pia kinamama kuua waume zao, kisa hisia za kuwapo harufu ya usaliti kwenye uhusiano au ndoa inaponukia.

Hili huenda linatokana na wanaume na wanawake kushindwa kuongea matatizo yao kwa wanasihi au watu wa karibu ama wataalum wa saikolojia kwa kuogopa aibu, kutoa siri za ndani na mambo kama hayo.

Yapo madai kuwa wanaume ndiyo wanadaiwa zaidi kuhusika na mauaji hayo, lakini hata kina mama wapo.

Kumekuwa na mifano kadhaa wa kadha, ya vitendo hivi mfano mkoani Shinyanga hivi karibuni wapenzi walihitilafiana mmoja akamua mwenzake kwa kumchana na wembe.

NI mwanadada Pendo Medusela (37), mkazi wa Manispaa ya Shinyanga, anayeshikiliwa na polisi kwa tuhuma za kumuua mpenzi wake, Timothy Magesa (35), kwa kumkata kwa wembe sehemu mbalimbali mwilini kutokana na madai ya kutofautiana kwenye mapenzi.

Tukio hili ni kama limeibua upya mjadala wa masuala ya mauaji kutokana na madai ya kuwapo wivu wa mapenzi na mmoja wao ambaye ni mwanamke aliyesema kuwa alipigiwa simu na kuonywa na mwanamke mwenzake kuwa aachane na mpenzi wake wa kiume.

Aidha, Jeshi la Polisi mkoani Songwe lilieleza tukio la mauaji ya mke na mume raia wa Kongo waliouawa kwa kupigwa na kuchomwa moto na wananchi katika Kijiji cha Chafuma, Wilaya ya Momba wiki iliyopita  Agosti 22, mchana kwa madai ya kumwua mama mwenye nyumba wao na kumzika.

Polisi ilisema wanandoa hao walidaiwa kuhusika na mauaji ya mwenye nyumba Simwaka mwanamama  mwenye miaka 80, kumzika bafuni na kuanza kuuza mazao yake .

Inaelezwa kuwa Agosti 22, wanakijiji  walianza kumtafuta bibi huyo na kugundua kaburi la siri bafuni kwake , lakini pia taarifa zilienea kwamba wanandoa hao na wapangaji wake waliuza baadhi ya mazao yake, jambo lililoibua hasira na kuwaripoti serikalini kwa hatua zaidi na mwisho ikiwa ni kuwaua kikatili.

Mauaji ya watoto ni mambo yaliyotikisa mwaka jana, na hivi ni baadhi ya visa, vilivyoripotiwa, Julai 15 mkoani Dodoma, kuliripotiwa tukio la mtoto Sumaiya Issa, kutekwa; Julai 7, Mbagala jijini Dar es Salaam, mtoto Nusra Omari alikutwa ameuawa na baadhi ya viungo kunyofolewa; Julai 17 mkoani Dodoma, mtoto Theresphora Mwakalinga alikutwa amefariki dunia na baadhi ya viungo vyake vimenyofolewa.

Ukitazama kwa undani vitendo hivi vya mauaji ni suala la kisaikolojia zaidi, maana mtu anakuwa na imani kwamba akimuua mwenzake atafaidika. Kuua hakufanyiki kwa ghafla ni mtiririko wa matukio yanayoenda kupanga hadi kuamua mauaji.

Hivyo basi ili kuepukana na haya yote ni vyema kama wapenzi wakikaa na kutengeneza namna yao ya kuishi, wakubaliane walivyo na madhaifu yao na kukubaliana yale ambayo wanatofautiana.

Wapenzi mpe uhuru mwenzio aishi maisha ayapendayo lakini si kvunjiana heshimuni kushiriki ngono na wengine au ulevi kupindukia cha msingi ni kulinda mambo mliyokubaliana ili kuepuka mafarakano.

Na pia serikali ifanye uchunguzi kwanini watu wanawaua watoto? Utafiti ujibu na ziwekwe sheria na adhabu kali zaidi kwa watu watakaojihusisha na vitendo hivi maana usipoziba ufa utajenga ukuta.