Taifa Stars ijipange kwa Afcon 2027

Nipashe
Published at 01:45 PM Aug 25 2025
Taifa Stars
Picha: Mtandao
Taifa Stars

BAADA ya timu ya Taifa (Taifa Stars) kutolewa kwenye michuano ya wachezaji wanaocheza ligi za ndani, CHAN, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, aliwataka wachezaji kutohusinika na kusononeka, badala yake wajipongeze kwa soka safi waliloonesha kwenye mashindano hayo.

Taifa Stars iliaga michuano hiyo baada ya kufungwa bao 1-0 na Morocco katika mechi ya hatua ya robo fainali iliyochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam Ijumaa.

Majaliwa aliwaambia wachezaji hao anaamini kutokana na uwezo walionesha katika michuano hiyo, kikosi hicho kina nafasi ya kufanya vizuri zaidi kwenye fainali za AFCON mwaka 2027.

Alisema pamoja na kupoteza mchezo huo, lakini uwezo ambao kikosi cha Stars ilichonacho sasa, hakuna timu yoyote Afrika inayoombea kukutana nayo.

"Wala msione kufungwa, ndiyo mwisho wa mchezo wa mpira wa miguu, hapana, nataka niwahakikishie wachezaji bado mna nafasi ya kufanya vizuri zaidi huko mbele katika michuano ya AFCON 2027, nendeni, tuendelee kuimarisha timu yetu.

“CHAN ni michezo ya timu za taifa inayoruhusiwa kuchezwa na wachezaji wa ndani tu, hapa hatujawaleta ndugu zetu wanaocheza klabu zingine nje ya nchi, hiki ni kipimo kikubwa sana kwetu.

Kila hatua kwetu ni funzo. Huko tulikotoka sisi tulikuwa kichwa cha mwendawazimu, kila timu ya taifa ilipokuwa inacheza na timu ya nje tulikuwa tunafungwa tu kila mwaka, kila mchezo, kila mashindano, leo hii Tanzania siyo ya kuijaribu, tumefikia hatua nzuri, naamini baada ya michezo hii TFF inaifanya timu hii kuendelea na michezo mingi ya kujipima nguvu ili kuwaimarisha wachezaji wetu," alisema.

Pia alisifu benchi la ufundi la timu hiyo ambalo liko chini ya Kocha Mkuu, Hemed Suleiman 'Morocco', akisema kwa sasa Watanzania wameacha kasumba ya kuamini zaidi walimu kutoka nje ya nchi.

Kauli hiyo ya Waziri Mkuu Majaliwa tunaiunga mkono kwa asilimia zote 100, kwa sababu kushindwa kwa wakati huu kutumike kama darasa la michuano ijayo ya AFCON 2027.

Ikumbukwe kwamba, CHAN ya safari hii imeandaliwa kwa ushirikiano wa nchi tatu, yaani Tanzania, Kenya na Uganda na hivyo hivyo, AFCON 2027 itaandaliwa katika nchi hizo.

Kitakachoongezea tu kwenye AFCON 2027 ni miji itakayochezewa mechi za mashindano hayo, mabapo itakuwa 10 kwa nchi zote tatu.

Kwa Tanzania miji ya Dar es Salaam, Arusha, Dodoma na Zanzibar ndiyo yakayoanda, huku nchini Kenya itachezwa katika miji ya Nairobi, Eldoret and Kakamega na Uganda kwenye miji ya Kampala, Lira na Hoima.

Wito wetu sasa, tunaona ni wakati muafaka zaidi kwa benchi la ufundi, kutathmini kile kilichotokea kwenye CHAN na kufanyia kazi kila aina ya mapungufu yaliyoonkena kwa ajili ya kujipanga. 

Tunaamini baadhi ya wachezaji waliokuwepo kwenye CHAN huwenda wasiwepo kwenye AFCON 2027 kutokana na umri au kiwango, hivyo basi Shirikisho la soka Tanzania, TFF, kwa kushirikiana na benchi la ufundi, wanatakiwa kutumia muda uliobaki kwa ajili ya kuimarisha kikosi hicho.

Kwa hatua iliyofikia Stars ya robo fainali ni nzuri, lakini tunaamini inaweza kufanya vizuri zaidi kwenye AFCON 2027, kwa kutumia uzoefu walioupata kwenye CHAN.