TAARIFA iliyochapishwa hivi karibuni kwenye tovuti ya Shirika la Afya Duniani, zinaeleza kwamba takriban wasichana milioni 16 wenye umri wa kati ya miaka 15 hadi 19 hujifungua kila mwaka.
Pia wengine 2,000,000 walio chini ya umri wa miaka 15 kadhalika nao hujifungua kila mwaka, WHO ikifafanua kuwa asilimia 95 ya mimba hizo hutokea katika nchi za kipato cha chini na cha kati, hususan miongoni mwa jamii maskini, zisizo na elimu na hasa za vijijini.
Bara la Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara lina viwango vya juu zaidi vya mimba za utotoni duniani, huku hali hiyo ikichangiwa na ndoa za binti, ukosefu wa elimu ya afya ya uzazi, na huduma duni za afya.
Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizo Kusini mwa Jangwa. Ni wazi kwenye idadi hiyo ya mimba za utotoni itakuwa imo. Hivyo ipo haja nasi kuchukua hatua makini ili kuwanusuru watoto ambao kwa umri huo ni wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.
Kutokana na taarifa hiyo, WHO imekuja na mwongozo mpya wa kimataifa kuzuia mimba za utotoni na kuboresha afya ya wasichana, kwa kutoa elimu kwao na kwa wavulana kuhusu uzazi wa mpango.
Mwongozo huo unaletwa kama hatua muhimu katika kukabiliana na changamoto hiyo inaoyakumba mamilioni ya wasichana duniani na kusababisha wakatishe ndoto zao katika elimu.
Ninadhani mikakati kama vile elimu ya kina ya afya ya uzazi kwa vijana, upatikanaji wa huduma rafiki za afya, na ushirikishwaji wa jamii katika kubadili mila potofu zinazochangia uwepo wa mimba.
Hivyo, ni vyema pia kuwapo juhudi za makusudi za kutoa njia mbadala ambazo zinatekelezeka ili kukabiliana na ndoa za utotoni kwa kuimarisha elimu ya wasichana wajitambue na kujua haki zao.
Njia hiyo itawafanya walio katika hatari ya kupata mimba kuweza kuziepuka, kwa kuwa watakuwa wamejengewa uelewa na kuwa makini dhidi ya vitendo vinavyoweza kusababisha wapate mimba.
Kinachotakiwa ni usawa na haki ili wasichana wabaki shuleni, waweze kutimiza ndoto zao kupitia elimu. Hivyo, suala la wao kufikiwa na elimu ya uzazi wanakuwa huru kufanya maamuzi sahihi kuhusu maisha yao.
Akizungumza katika uzinduzi wa Ripoti ya Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria Tanzania ya mwaka 2022, Rais Samia Suluhu Hassan, anaitaja mikoa inayoongoza kwa mimba za utotoni.
Akikariri ripoti hiyo, anasema mikoa inayoongoza mimba za utotoni kuwa ni Songwe asilimia 45, Ruvuma asilimia 37, Katavi asilimia 34, Mara asilimia 31 na Rukwa asilimia 30.
Rais anaitaja mikoa ya Dodoma, Kigoma, Tabora na Shinyanga kuwa imefanikiwa kupunguza mimba za utotoni, na kwamba ni vyema kuipongeza na pia kujifunza mbinu ambazo imetumia kupunguza tatizo.
Mbali na mikoa aliyoitaja kuongoza kwa mimba za utotoni, anabainisha kuwa Dar es Salaam nayo haiko nyuma, bali mimba za aina hiyo zimeongezeka kutoka asilimia 11.9 hadi kufikia asilimia 18.1.
Kwa ripoti hiyo, ni wazi kila mmoja ana wajibu wa kulinda maisha ya watoto kwa kutimiza wajibu wa kusimamia malezi bora ambayo yatawawezesha kuwa salama bila vikwazo vya mimba.
Pamoja na hayo, ni vyema pia viongozi ambao mikoa yao ina idadi kubwa ya mimba za utotoni kuchukua hatua mbalimbali za kudhibiti mimba ikiwamo kufahamu chanzo cha tatizo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED