Wanaoanzisha migogoro kwenye taasisi za umma wasionewe haya

Nipashe
Published at 02:28 PM Aug 28 2025
Wananchi ni nguzo muhimu kwa maendeleo
Picha; Mtandao
Wananchi ni nguzo muhimu kwa maendeleo

MASHIRIKA na taasisi za umma ziliundwa kwa ajili ya kutoa huduma kwa wananchi pamoja na kuzalisha kwa faida na hatimaye kutoa gawio kwa serikali. Pia taasisi hizo zinapaswa kujitegemea kwa maana ya kuhakikisha zinawalipa wafanyakazi stahiki zao bila kutegemea ruzuku kutoka serikali kuu kwa ajili ya uendeshaji na matumizi ya kiutawala.

Kutokana na ukweli huo, taasisi hizo za umma chini ya Ofisi ya Msajili wa hazina, zimekuwa zikisisitizwa kufanya kazi na kutoa huduma za ubora wa hali ya juu kwa wateja kwa ajili ya maendeleo yao na kuchangia pato la taifa kwa ujumla. 

Licha ya dhima hiyo, taasisi nyingi zimekuwa zikishindwa kutekeleza wajibu na kupata hasara kila mwaka. Hata viongozi wakuu, akiwamo Rais samia Suluhu Hassan, wamekuwa wakitoa maelekezo mbalimbali kuhusu utendaji kazi wao. Kutokana na kushindwa kuleta tija, kumekuwa na mabadiliko ya mara kwa mara ya watendaji wakuu kwa kuwaondoa wale walioshindwa na kuteuliwa wapya. 

Sababu nyingine inayofanya mashirika na taasisi za umma kushindwa kutekelezwa wajibu na kuleta tija na ufanisi ni migogoro ya ndani ambayo chanzo kikuu kimekuwa baina ya watendaji wakuu na bodi za wakurugenzi hasa wenyeviti. 

Juzi, akifunga kikao kazi cha viongozi wa taasisi kwa maana ya watendaji wakuu na wenyeviti wa bodi, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Dotto Biteko, alieleza anavyoumizwa na tabia. Aliweka bayana kwamba baadhi ya watendaji wakuu wa taasisi na mashirika ya umma, wanavutana na wenyeviti wao wa bodi badala ya kufanya kazi kwa upendo na kutanguliza maslahi ya taifa.

Kutokana na mwenendo huo, ameonya na kuelekeza viongozi hao waache tabia hiyo mara moja na  watakaporejea katika maeneo yao ya kazi wabadilike na kuchapa kazi huku upendo na umoja miongoni mwao vikitawala. Dk. Biteko pia aliwakumbusha viongozi hao kuwa kiongozi bora hatapimwa kwa maneno na mipango bali hupimwa kwa vitendo na matokeo.

Ni wazi kwamba migogoro katika sehemu za kazi imesababisha mashirika mengi ya umma kufungwa kwa kuwa kila uchao, viongozi na vyama vya wafanyakazi wamekuwa wakivutana na kufanya kulegalega kwa uzalishaji na utoaji huduma. Katika miaka ya 1990 na kurudi nyuma, lilikuwa jambo la kawaida sana kusikia wafanyakazi wamemfungia milango kiongozi mkuu na manejimenti yake. 

Kwa sasa, kumekuwa na malumbano ya ndani kwa ndani na mivutano baina ya menejimenti zikiongozwa na watendaji wakuu kwa upande mmoja na wenyeviti wa bodi kwa upande mwingine. Hali hiyo kwa kiasi kikubwa imesababisha kurudi nyuma kwa maendeleo badala ya kufanya taasisi kuwa na tija na ufanisi.

Kama alivyoonya Naibu Waziri Mkuu Biteko, ni vyema sasa viongozi wa taasisi wakajielekeza katika uzalishaji na utoaji wa huduma wenye tija badala ya kuendelea na malumbano ambayo katu hayajengi bali yanabomoa misingi ya kuanzishwa kwa taasisi hizo. 

Katika baadhi ya mashirika na taasisi, wenyeviti wa bodi za wakurugenzi wamekuwa wakifanya kazi kama watendaji kwa kutaka wapewe ofisi na Kwenda kila siku kazini wakati sheria inawataka kusimamia sera na mipango kama inatekelezwa ipasavyo. Hali hiyo imesababisha kuwapo kwa migogoro. 

Wakati umefika sasa kwa serikali kutokuwaonea haya watendaji na viogonzi wa bodi wanaoendekeza migogoro ndani ya taasisi kwa maslahi binafsi. Kila mtu anapaswa kuwajibika kwa nafasi yake badala ya kuingilia majukumu ya upande mwingine na hiyo ndiyo sababu kubwa ya kuwapo kwa migogoro hiyo. 

Pia viongozi hao wa taasisi watambue kuwa kuendekeza migogoro na kusababisha kukosekana kwa tija na ufanisi na hatimaye kutokuwapo kwa matokeo chanya ya kimaendeleo ni sawa na uhujumu uchumi na kuikosesha serikali mapato, hivyo hawana budi kuchukuliwa hatua kali ikiwezekana kufikishwa katika vyombo vya sheria.