'Wagombea ni hoja, nidhamu, vinginevyo ‘inakula kwenu!’

By Beatrice Moses , Nipashe
Published at 02:21 PM Aug 28 2025
AI
AI
AI

HATIMAYE imetimu wakati ambao hulo nyuma uliitwa ‘tarehe zijazo’ sasa ni leo.

Kipenga cha Tume Huru ya Uchaguzi (INEC), kinachoruhusu kuanza kwa kampeni za wagombea wa urais, ubunge na udiwani kutoka vyama vyama vya siasa tofauti kujinadi kwa sera kuelezea utekelezaji wa ilani utakavyokuwa iwapo watapewa ridhaa na wananchi wenye sifa ya kupiga kura.

Hatua hii ni muhimu kwa kuwa wananchi wagombea ama wanapojieleza au kunadi sera zao, wananchi wanapata nafasi ya kuchakata ili kufanya uamuzi sahihi wa kutumia boksi la kura kuamua wanayeamini kuwa atatekeleza ahadi alizozitoa.

Hapo kuna ya umuhimu wa kujielezea ili ueleweke au uweke ushawishi kwa wananchi. Ni shughuli pevu hasa katika zama hizi za teknolojia, ni vyema wagombea kuhakikisha wanatumia hekima.

Hizo ni katika kuelezea sera zao na siyo kutumia ushawishi wa maneno yasiyo na staha kuwachafua wapinzani wao kumbuka jambo hilo linaweza kukugharimu kukosa nafasi hiyo muhimu unayoisaka.

Nawakumbusha wagombea kwa niaba ya Watanzania wenzangu kwamba, wananchi wanatamani kusikia ilani za vyama husika zina maslahi gani kwao na jinsi zitakavyotekelezwa ili kuleta maendeleo ya taifa kwa ujumla.

Naamini kwamba, kila mgombea mwenye uelewa mzuri na hekima, amejiandaa vizuri kutumia mbinu bora ya kushawishi wananchi kumchagua.

Awe ameaminiwa na chama chake kukiwakilisha na ataeleza hatua za utatuzi wa kero zinazowakabili na utekelezaji ahadi utakavyokuwa na siyo porojo au kashfa kwa wagombea wengine.

Kuna kanuni zimewekwa kama mwongozo ambazo zinalenga kuhakikisha wagombea wote wanazingatia maadili na huo ndiyo uungwana, pia kuweka alama nzuri kwa vijana ambao wanaendelea kujifunza masuala ya siasa.

Hivyo itakuwa ni jambo la fedheha kubwa iwapo kuingia kwenye mgombea kutoka chama fulani hana uwezo wa kujenga hoja isipokuwa kutumia lugha chafu, dhidi ya wagombea wenzake.

Kwa mujibu wa Kanuni za Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani za Mwaka 2025, imebainisha jinsi Mamlaka ya Kamati za Maadili ya Uchaguzi Ngazi ya kitaifa, jimbo na kata katika kutoa adhabu, pamoja na kutaja hatua za kuchukua.

 Baadhi ya kanuni hizo ni pamoja na (a) kuagiza upande uliokiuka maadili kusahihisha kosa au makosa yaliyotendeka na iwapo italazimu kuuomba umma msamaha; (b) kutoa onyo au karipio kwa maandishi; (c) kutangaza jina la chama cha siasa au mgombea aliyekiuka maadili na kueleza kosa au makosa yake kwa njia ya taarifa. 

Inafafanua kuwa, taarifa hiyo itapaswa kutolewa kwa umma kupitia redio, televisheni, magazeti na njia nyingine za mawasiliano.

Pia, (d) kamati inaweza kukisimamisha chama cha siasa au mgombea kuendelea kufanya kampeni za uchaguzi kadiri itakavyoonekana inafaa, yaani kuzuiwa kufanya kampeni za uchaguzi itajumuisha zuio la kufanya mikusanyiko ya aina yoyote inayoashiria kufanya kampeni za uchaguzi.

Katika kipengele (e) kamati inaweza kuzuia chama cha siasa au mgombea kutumia vyombo vya habari au kubandika machapisho ya kampeni kwa muda ambao kamati itaona unafaa; (f) kukitaka chama cha siasa au mgombea kulipa faini kama ilivyoainishwa.

Inaelezwa kwenye kipengele(i) ikiwa ni katika ngazi ya kata, kiasi kisichozidi Sh. 200,000 ambacho kitathibitishwa na kamati ya jimbo; (ii) ikiwa ni katika ngazi ya jimbo, kiasi kisichozidi Sh. 700,000 za ambacho kitathibitishwa na kamati ya kitaifa; (iii) ikiwa ni katika ngazi ya kitaifa, kiasi kisichozidi Sh. 1,500,000) au kwa kadiri kamati itakavyoona inafaa.

Wakati kipengele (g) inaelezwa kuwa kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 135 cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Namba Moja ya Mwaka 2024, adhabu ya kosa la unyanyasaji au ukatili wa kijinsia itakuwa ni kukisimamisha chama cha siasa au mgombea (iii) ikiwa ni katika ngazi ya kitaifa, kiasi kisichozidi Sh 1,500,000 au kwa kadiri kamati itakavyoona inafaa.

Hivyo, wananchi wanatarajia kushuhudia/kushiriki na kukamilisha ratiba ya kampeni za amani hadi ifikapo mwisho wake, kisha kuruhusu Oktoba 29, mwaka huu, kutumika kwa hatua ya kupiga kura kama ilivyopangwa, kisha baada ya hapo kila mgombea atajua hatima ya  mbio zake kama zina matunda mema au amekwama.