Vijana TEHAMA ni fursa isiwe uraibu

By Sabato Kasika , Nipashe
Published at 01:07 PM Aug 19 2025
Vifaa vya kiteknolojia
Picha: Mtandao
Vifaa vya kiteknolojia

KATIKA dunia ya leo ya sayansi na teknolojia, matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mwasiliano (TEHAMA), yamechukua nafasi kubwa kurahisisha kazi na mambo mengine muhimu ya kiuchumi, tiba, kilimo, viwandani na kwa ujumla uzalishaji na utoaji huduma.

TEHAMA imefanya mawasiliano kuwa rahisi popote duniani, kwani inawezekana kuzungumza na marafiki na familia kupitia simu, barua pepe, ujumbe mfupi na mitandao ya kijamii, pia kupata habari mbalimbali kutoka pande zote dunia kwa urahisi na kwa muda mfupi.

Vilevile, teknolojia hiyo imewafanya watu kuwa na ufanisi zaidi katika kazi zao, kwa kutumia programu za kompyuta imekuwa rahisi kukamilisha kazi kwa haraka na kwa ufanisi zaidi.

Aidha, TEHAMA imefungua fursa nyingi za elimu, wanafunzi wanaweza kujifunza chochote wanachotaka mtandaoni popote walipo na wanweza kuongeza uelewa ambao hawakuwa nao awali kupitia njia hiyo.

Kwa mfano zipo baadhi ya kozi ambazo zimekuwa zikifundishwa vyuoni, lakini kwa sasa wanafunzi wanaweza kuzipata mitandaoni kwa urahisi na kujisomea iwapo watakuwa na nia hiyo.

Lakini teknolojia imekuwa na changamoto kwa baadhi ya vijana rika mbalimbali, kwani imekuwa ni kawaida kwao kutumia muda mwingi kwenye simu, kompyuta na mitandao ya kijamii kwa mambo yasiyo ya muhimu kwa maendeleo yao.

Pamoja na hayo, wakati mwingine teknolojia inaweza kuwa hatari ikiwa itatumiwa vibaya, kwani taarifa binafsi za mtu zinaweza kudukuliwa, hivyo suala la umakini katika matumizi teknolojia ni la muhimu.

Vijana ni nguvukazi ya taifa, hivyo, ni vyema wajengwe katika misingi ambayo itawafanya wawe viongozi wa baadaye, lakini pia wazee busara wa baadaye watakaotegemewa na taifa kwa ushauri.

Mchango wao vinahitajika katika uhai wa taifa, lakini kinyume cha hapo, nchi inaweza kukosa viongozi makini wa baadaye na kuwa na wazee wa baadaye wasio na manufaa kwa nchi yao kutokana na teknolojia.

Kimsingi, vijana wanatakiwa kuchangia katika maendeleo ya nchi yao lakini hali ilivyo, inaonesha kuwa huenda wakakosekana viongozi wa baadaye na kupata wazee ambao itakuwa vigumu kuchota busara kwao.

Hiyo inatokana na ukweli kwamba baadhi yao wamekuwa ni waraibu wa mitandao kwa mambo yasiyofaa, wasiofuatilia mambo ya muhimu yanayoendelea katika nchi yao.

Kundi hilo ndilo ambalo kama nilivyoeleza kuwa hushinda kwenye mitandao ya kijamii, kuandika mambo ambayo hayana umuhimu na pia wanafuatilia mambo yasiyo na maana kwao wala kwa taifa lao.

Vijana wanatakiwa kuwa sehemu ya maendeleo kwa nchi yao badala ya kushinda kwenye mitandao ya kijamii wakifanya vitu ambavyo ni sawa na kupoteza muda bila sababu za msingi.

Kwa ujumla ni kwamba, teknolojia inaweza kutumika kwa malengo mema au mabaya, hivyo ni vyema kuitumia kwa umakini kwa ajili ya kupata mambo muhimu na sio ambayo hayafai.

Vijana wakiendelea kushinda kwenye mitandao ya kijamii na kuandika mambo ambayo hayana maana badala ya kuitumia kama fursa ya kujiendeleza kielimu na vitu vingine muhimu, wanaweza 'kupotea'.

Sina maana kwamba mitandao ya kijamii ni mibaya. Nilishaeleza faida na hasara zake. Jambo la muhimu ni kujua ni namna gani wanaitumia. Lakini ukweli ni kwamba ina faida na hasara.

Katika mazingira hayo, ni vyema vijana waelekeze nguvu zao kutumia mitandao kwa faida, ambazo kimsingi zinaweza kuwasaidia kwa mambo mengine ikiwamo hata kupata ajira au kujiajiri.