Sheria usalama barabarani irekebishwe kudhibiti ajali

Nipashe
Published at 01:45 PM Jul 18 2025
Sheria usalama barabarani
Picha: Mtandao
Sheria usalama barabarani

AJALI za barabarani zimeendelea kugharimu maisha ya watu, hivyo taifa kupoteza nguvu kazi kwa ajili ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi. Hivi sasa kila uchao habari kuhusu ajali limekuwa jambo la kawaida masikioni mwa Watanzania.

Hivi karibuni kwa mfano, katika mkoa wa Kilimanjaro zimeshuhudiwa ajali kadhaa zilizohusisha mabasi makubwa ya abiria na madogo. Ajali hizo zimesababisha makumi ya watu kupoteza maisha na wengine kujeruhiwa na kupoteza baadhi ya viungo na kuwa watu wenye ulemavu. 

Mbali na ajali hizo, kumekuwa kukitokea matukio kama hayo katika mikoa mbalimbali ambayo pia yamegharimu maisha ya watu. Kwa mantiki hiyo, ajali hizo zimeendelea kuwa janga lingine linaloligharimu taifa kwa sasa kutokana na vifo na watu kupata ulemavu hatua ambayo inachangia kwa kiasi kikubwa kupotea kwa nguvu kazi ambayo ni tegemeo kwa maendeleo ya nchi.  

Sababu ambazo zimekuwa zikitajwa kwamba ni chanzo kikuu cha ajali hizo ni zile zile za miaka nenda rudi na hazijawahi kubadilika. Kila inapotokea ajali, makamanda wa polisi wa mikoa wamekuwa wakizitaja sababu hizo kuwa ni za kibinadamu, kwa  mujibu wa takwimu mpya za mwaka 2024 zilizotolewa hivi karibuni, zinachangia kwa asilimia 97. 1.   

Kwa mujibu wa takwimu hizo zilizotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), sababu zinazotajwa kuwa chanzo cha ajali hizo ni mwendokasi, uzembe wa madereva na uendeshaji hatarishi wa waendesha pikipiki. 

 Zingine ni ubovu wa magari, sababu za kimazingira kama vile miundombinu mibovu ya barabara na moto. Pia suala la madereva kutumia vilevi limekuwa likitajwa kuwa sababu nyingine ya ajali hizo.  

Katika ripoti hiyo, ajali za barabarani 1,520 ziliripotiwa Tanzania Bara kwa kipindi cha mwaka 2024 ikiwa pungufu kwa matukio 21 kulinganisha na ajali 1,541 zilizotokea katika muda kama huo mwaka 2023.  

Aidha, takwimu hizo zinaonesha ajali 1,005 zilikuwa mbaya zaidi na zilisababisha  kusababisha vifo 1,521 mwaka 2024, ikiwa ni ongezeko la vifo 34 kulinganisha na ajali 987 zilizosababisha watu 1,487 kupoteza maisha mwaka 2023.

Ripoti hiyo inabainisha kwamba ajali za pikipiki bado zimeendelea kuwa janga kwa mwaka 2024 kwa kusababisha ajali. Katika mwaka 2024, kulikuwa na ajali za pikipiki 383 sawa na ongezeko la asilimia 2.4 kulinganisha na ajali 374 mwaka 2023. Ajali hizo zilisababisha vifo vya watu 341 na wengine 352 kujeruhiwa.

Kwa ujumla, ajali hizo zimekuwa kama Donda ndugu kwa sababu licha ya watu kuchukuliwa hatua zikiwamo wahusika kutozwa faini, kufungiwa leseni na baadhi ya kampuni zinazomiliki mabasi kufungiwa au kusimamishwa kwa muda, tatizo linazidi kuongezeka. 

Inawezekana wahusika kwa maana ya madereva, wamekuwa hawajali wala kuona adhabu hizo kama mbaya kwao ndiyo maana wamekuwa wakiendelea kufanya makosa yale yale miaka nenda miaka rudi. 

Kwa mtazamo yakinifu, kiwango cha adhabu kinachotolewa ni kidogo ndiyo maana wamekuwa wakirudia makosa yale yale. Dereva anaamua kufanya makosa, mengine yanagharimu uhai wa watu kwa kuwa anajua hata ikitokea ajali atatozwa faini na maisha yatasonga.    

Wakati umefika sasa kwa serikali kufanya marekebisho ya Sheria ya Usalama Barabarani kwa kuipa meno zaidi ili yawang’ate wanaosababisha ajali ambazo sasa zimekuwa pasua kichwa. 

Suala hilo aliwahi kuagiza pia Rais Samia Suluhu Hassan kwamba amechoka kusikia habari za ajali na kusisitiza kama kuna mafundo kwenye sheria husika, ipelekwe bungeni na kufanyiwa marekebisho. Sasa kigugumizi kiko wapi kurekebisha sheria hiyo?