Stars itumie michuano ya CECAFA kujipa kwa CHAN

Nipashe
Published at 09:08 AM Jul 21 2025

Baadhi ya wachezaji wa timu ya taifa, Taifa Stars
Picha: Mtandao
Baadhi ya wachezaji wa timu ya taifa, Taifa Stars

TIMU ya taifa, Taifa Stars, kesho inatarajia kushuka dimbani jijini Arusha kwenye uwanja wa Karatu kucheza mchezo wake wa kwanza wa michuano ya CECAFA 4 Nations dhidi ya Senegal, baada ya kumaliza kambi yake nchini Misri.

Stars ilirejea nchini juzi kutoka Misri ambako iliweka kambi kwenye mji wa Ismailia, ikiwa ni sehemu ya kujiandaa na michuano ya Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani, CHAN.

Michuano hiyo ya CECAFA 4 Nations, inatarajiwa kuanza kupigwa leo hadi Julai 27, ikizishirikisha nchi ambazo ni wenyeji wa CHAN, Tanzania, Kenya na Uganda, pamoja na timu alikwa, Senegal, lengo ikiwa ni kuzipa mazoezi kabla ya fainali hizo.

Ratiba inaonesha kuwa timu ya taifa ya Kenya, Harambee Stars, leo itafungua michuano hiyo kwa kukipiga dhidi ya timu ya Uganda, mechi zote zinatarajiwa kupigwa Uwanja wa Karatu.

Ratiba inaonesha, Stars itacheza dhidi ya Senegal kesho, kabla ya kurejea tena dimbani Julai 24 kucheza dhidi ya Kenya na kumalizia mechi yake ya mwisho dhidi ya Uganda, Julai 27.

Wakati michuano ya CHAN ambayo ina jumla ya timu 19, huku Stars ikiwa Kundi B na timu za Burkina Faso, Afrika ya Kati, Madagascar na Mauritania, pazia lake litafunguliwa Agosti 2, kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Kundi A, lina timu za Angola, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Kenya, Morocco na Zambia, huku Kundi C, likiundwa na timu za Algeria, Guinea, Niger, Afrika Kusini na Uganda.

Timu za Congo Brazaville, Nigeria, Senegal na Sudan, zinaunda Kundi D.

Kabla ya kuanza kwa michuano hiyo ya CECAFA, kocha wa Stars, Hemed Morocco alisema kwamba, mashindano hayo hayajaja wakati mwafaka kutokana na kuingiliana na maandalizi yao kuelekea CHAN.

Kocha huyo alionesha wasiwasi kuwa wachezaji wanaweza kuwa na fatiki kuelekea mchezo wa ufunguzi wa CHAN dhidi ya Burkina Faso, Agosti 2, kwani watakuwa wamecheza michezo kadhaa ya michuano hiyo ya CECAFA siku chache kabla ya ufunguzi wa CHAN.

Morocco alisema hiyo ni michuano mizuri, lakini haikuja kwenye wakati sahihi, kwake yeye ingekuja wiki mbili zilizopita ingekuwa vyema sana ili kuwaweka sawa wachezaji wake kuelekea CHAN.

Alisema watacheza mechi tatu ndani ya siku tano au sita, halafu wanakwenda kucheza mchezo mgumu, Agosti 2, na kubainisha kuwa wachezaji watakuwa na ugumu fulani hasa kwenye fatiki.

Pamoja na kwamba, maneno ya kocha Morocco yanaweza kuwa na ukweli kwa upande mmoja, lakini sisi tunaona mashindano haya ya CECAFA ni sehemu nzuri ya kujipima kwa Stars.

Tunasema hivyo kutokana na ukweli kwamba, Stars ikiwa nchini Misiri kwenye kambi yake haikupata mechi yoyote kubwa yenye ushindani kwa ajili ya kupima utimamu wa wachezaji wake.

Hivyo, Nipashe tunaona kwamba, Stars inaweza kutumia mashindano hayo ya CECAFA kama sehemu ya mwisho kwa maandalizi yao ya CHAN ambapo watakuwa na timu zenye ushindani mkubwa.

Tunaamini kwamba, kwa kuanza kucheza na miamba ya Afrika, Senegal kwenye mashindano hayo, kunaweza kuimarisha utimamu wa wachezaji wake.

Pamoja na hayo, pia mashindano hayo yanaweza kusaidia kujua ni wapi ambapo panatakiwa kuelekeza zaidi nguvu kabla ya kuanza kwa CHAN na pia kurekebisha mapungufu yatakayojitokeza.

Hii ni kwa sababu Stars kwenye CHAN itakutana na timu zenye wachezaji wenye uwezo wa hali ya juu, hivyo kujiweka sawa, na CECAFA kinaweza kuwa kipimo sahihi kwao, hasa ikizingatia kuwa timu zote zilizopo kwenye mashindano hayo, pia zipo kwenye CHAN.