TIMU ya Taifa, Taifa Stars, imefanikiwa kufuzu Robo Fainali ya michuano ya mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ligi za ndani, CHAN, baada ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Madagascar katika mchezo wa Kundi B, Jumamosi usiku kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Mabao yote ya Stars yalifungwa na mshambuliaji wa Yanga, Clement Mzize dakika ya 13 na 20, wakati la Madagascar likifungwa na beki Nantenaina Gregasse Razafimahatana dakika ya 34.
Stars sasa inaongoza Kundi B ikiwa na pointi tisa ikifuatiwa na Mauritania yenye pointi nne baada ya timu zote kucheza mechi tatu, kwenye michuano hiyo inayoendelea katika nchi tatu za Tanzania, Kenya na Uganda.
Burkina Faso inafuatia nafasi ya tatu kwa pointi zake tatu na Madagascar ina pointi moja ikiwa nafasi ya nne baada ya timu zote kucheza mechi mbili, wakati Jamhuri ya Afrika ya Kati ambayo imepoteza mechi zote mbili za mwanzo inashika mkia.
Baada ya mechi za leo, Taifa Stars inaendelea kuongoza Kundi B kwa pointi zake tisa ikifuatiwa na Mauritania yenye pointi nne baada ya timu zote kucheza mechi tatu.
Kufanikiwa kwa Stars kutinga Robo fainali kwenye michuano hiyo kwa mara ya kwanza tangu kuanzisha kwake, ni historia kwa soka la Tanzania na sasa inatakiwa kujipanga vizuri katika hatua hiyo.
Stars ambayo inaongozwa na kocha mzawa, Hemed Suleiman ‘Morocco’ tangu katika mchezo wa kwanza wa michuano hiyo, ilionesha kiwango cha kuvutia na hivyo tuna imani kubwa, itafika mbali kama sio kulibeba kabisa taji hilo.
Tunasema hivyo kutokana na ukweli kwamba, Stars inaonekana kubadilika katika kila mchezo, kwani wachezaji wamekuwa wakitumia vyema maelekezo ya benchi la ufundi.
Nipashe tunasema kwamba, Stars ina uwezo mkubwa wa kulibakisha kombe hilo hapa nchini kama itaendelea na morali iliyoonesha katika mechi hizo tatu za hatua ya makundi.
Tunaamini kwamba, hivi sasa benchi la ufundi pamoja na wachezaji watakuwa na muda wa ziada ya kuangalia mapungufu yao na kujipanga vizuri kwenye hatua ya robo fainali.
Tunasema hivyo kwa sababu tunajua hatua ya robo fainali itazikutanisha timu ngumu na hivyo ushindani utakuwa mkubwa zaidi.
Hivyo, lazima benchi la ufundi pamoja na wachezaji wenyewe, waangalia wapi wanapoona kuna mapungufu au udhaifu na kufanyia kazi ili kuhakikisha hatua hiyo inakuwa rahisi kwao.
Tunaamini Stars itafanya kile ambacho Watanzania wamekishuhudia kwenye michezo hiyo mitatu, kwa sababu inapata uungwaji mkono mkubwa na mshabiki na Serikali na wadau wengine.
Kuonesha hilo, katika michezo mitatu waliyocheza na kupata ushindi, wachezaji wa timu hiyo wamekusanya zaidi ya Sh. 200 Milioni kama bonasi ya ushindi wao kutoka kwa Serikali, Wizara ya Michezo na wadau wengine.
Hakuna sababu ya Stars kushindwa kuvuka hatua ya robo fainali na kutinga nusu fainali na baadae fainali yenyewe. Lakini pia tunawakumbusha mashabiki na watanzania kwa ujumla, timu hii bado inatakiwa kuendelea kuungwa mkono ili kufanya vizuri zaidi, kwa wale ambao wana uwezo wa kutoa chochote kama tunavyoona kwa taasisi mbalimbali basi wafanye hivo kuchochea morali na hali ya kupambana.
Siku zote shabiki ni mchezaji wa 12 uwanjani, uwepo wao uwanjani ni hamasa tosha, wachezaji wanaposikia shangwe kutoka jukwaani na makelele ya kuwakumbusha jambo kunaleta hamasa kwao kuona kuna kundi la watanzania wapo nyuma yao.
Tunaitakia kila la heri Taifa Stars kwenye hatua ya robo fainali, tuna imani na nyinyi, fanyeni kweli ili muweze kuingia katika historia ya soka la Tanzania
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED