Tuna imani na Taifa Stars, libakisheni kombe nchini

Nipashe
Published at 05:24 PM Aug 04 2025
Mabao ya Taifa Stars yamefungwa na Abdul Suleiman ‘Sopu’ na Mohamed Hussein ‘Zimbwe Jr’. Michuano hiyo inafanyika kwa mara ya kwanza katika nchi za Tanzania, Kenya na Uganda
Picha: Mtandao
Mabao ya Taifa Stars yamefungwa na Abdul Suleiman ‘Sopu’ na Mohamed Hussein ‘Zimbwe Jr’. Michuano hiyo inafanyika kwa mara ya kwanza katika nchi za Tanzania, Kenya na Uganda

TIMU ya Taifa ya Tanzania, maarufu kama Taifa Stars, imeanza vyema kampeni yake ya michuano ya Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN), baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Burkina Faso.

Mchezo huo wa kundi B ulipigwa usiku wa Jumamosi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, ambao ndio ulikuwa wa ufunguzi rasmi wa michuano hiyo inayofanyika kwa ushirikiano wa nchi tatu, Tanzania, Kenya na Uganda. 

Michuano hiyo iliyofunguliwa rasmi Jumamosi, inashirikisha timu 19 na itaendelea hadi Agosti 30, mwaka huu. Ikumbukwe, baada ya Fainali hizi za CHAN, Afrika Mashariki itakuwa tena mwenyeji wa Fainali kubwa za Mataifa ya Afrika (AFCON) za mwaka 2027 ambapo Shirikisho la Soka Afrika imeziteua tena Tanzania, Kenya na Uganda kuwa wenyeji wa fainali hizo. 

Stars itarejea tena uwanjani Jumatano saa 2:00 usiku, kucheza mchezo wa pili wa Kundi B, dhidi ya Mauritania. Kundi hilo pia lina timu za Afrika ya Kati na Madagascar ambalo kituo chake ni Dar es Salaam, likicheza Uwanja wa Mkapa. 

Mbele ya umati wa mashabiki waliokuwa wakishangilia kwa sauti kubwa, Taifa Stars walitawala sehemu kubwa ya mchezo huo. 

Ushindi huu umekuwa wa kihistoria kwa Tanzania, kwani ndio mara ya kwanza kuwahi kushinda mchezo wa ufunguzi wa CHAN, baada ya kupoteza michezo miwili iliyopita katika mashindano mawili yaliyopita. 

Bao la kwanza lilifungwa kwa mkwaju wa penalti na Abdul Sopu muda mfupi kabla ya mapumziko. 

Penalti hiyo ilipatikana baada ya Clement Mzize kuangushwa kwenye eneo la hatari na beki wa Burkina Faso, Franck Aimé Tologo kufuatia pasi ya kiungo, Mudathir Yahya Abbas. 

Katika kipindi cha pili, beki Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ alihakikisha ushindi kwa Stars kwa kufunga bao la kichwa katika dakika ya 71, na kuamsha shamrashamra kwa mashabiki. Matokeo haya yanaiweka Tanzania katika nafasi nzuri kwenye kundi hilo. 

Baada ya ushindi huo, Nipashe tunaamini kwamba, Stars ina nafasi nzuri ya kufuzu hatua ya mtoano na baadae kutinga fainali na kupambana kuhakikisha kombe hilo linabaki hapa nchini. 

Tunasema hivyo kwa sababu ya kiwango bora kilichooneshwa na kikosi cha Stars kwenye mchezo huo, kwani wachezaji walitumia vizuri maelekezo ya benchi la ufundi linaloongozwa na kocha Mkuu, Hemed Morocco. 

Wachezaji walionekana kutulia na kutumia vizuri maelekezo ya kocha na hivyo tunaamini mchezo utakaofuata, Stars watakuwa kwenye kiwango bora zaidi na kujihakikishia ushindi. 

Hii ina maana kwamba, kikosi hicho kimejifua vya kutosha katika maandalizi yake na hivyo kuwa na uelewano mzuri wa wachezaji dimbani. 

Pamoja na hilo tunawataka wachezaji wetu kujituma zaidi, kwani hiyo ni sehemu ya kuonesha vipaji vyao na kujiuza kwa timu nyingine hasa za Ulaya, kwa sababu mashindano hayo yanatazamwa na mawakala wengi wa soka duniani. 

Huku lengo kuu la CHAN likiwa ni kutoa jukwaa la kipekee kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani kuonesha vipaji vyao, hivyo tunaona hiyo ni fursa nzuri zaidi kwao. 

Ni fursa ya kujulikana barani Afrika na kwa wasajili wa kimataifa, huku ikisherehekea msingi wa soka la Afrika. Hivyo, sisi tunawatakia kila la heri Stars na tunawataka kuhakikisha wanaipigania nchi na kulibakisha kombe hapa nchini. 

Kila la heri Taifa Stars.