Tusimamie haki, tukatae ukatili na kujichukulia sheria mikononi

Nipashe
Published at 02:00 PM Aug 13 2025
Tusimamie haki, tukatae ukatili na kujichukulia sheria mikononi
Picha: Mtandao
Tusimamie haki, tukatae ukatili na kujichukulia sheria mikononi

TUKIO la kusikitisha lililotokea jijini Mwanza hivi karibuni, ambapo mwili wa kijana Dickson Yusuph, dereva bodaboda mwenye umri wa miaka 24, ulikutwa bila kichwa kando ya barabara ya Nyegezi–Luchelele, limezua maswali mazito kuhusu hali ya usalama, maadili ya kijamii na mwelekeo wa taifa katika kushughulikia migogoro ya kijamii na kihisia.

Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi, vijana wawili waliotajwa kwa majina ya Oscar Emmanuel na Edwin Bujuel walikiri kuhusika na mauaji hayo ya kinyama wakidaiwa kuchukua hatua hiyo kutokana na wivu wa kimapenzi. 

Katika kile kilichofuata kama mlolongo wa mauaji, wananchi wenye hasira waliwavamia na kuwaua watuhumiwa hao wawili kwa kipigo wakati walipokuwa wakionesha polisi mahali walikoficha kichwa na mali za marehemu.

Kwa upande mmoja, tukio hili linaonesha kiwango cha juu cha ukatili katika jamii yetu, ukiachilia mbali mauaji ya Dickson, pia ni dhahiri kuwa hisia kali za hasira na kutokuwa na imani na mifumo ya haki zimelazimisha wananchi kujichukulia sheria mikononi. Ni hali inayopaswa kulaaniwa kwa nguvu zote.

Ni wazi kwamba, kuondoa uhai wa mtu ni uhalifu mkubwa wa kibinadamu na kisheria. Hakuna sababu yoyote, iwe ni wivu wa kimapenzi au ugomvi wa binafsi, inayoweza kuhalalisha unyama wa namna hii. 

Hii ni ishara ya kuharibika kwa maadili, kushuka kwa thamani ya utu na kuporomoka kwa misingi ya heshima ya maisha ya binadamu.

Pili, na kwa masikitiko makubwa zaidi, ni hatua ya wananchi kuchukua sheria mikononi kwa kuwaua watuhumiwa. Ingawa hasira ya jamii mbele ya tukio la kutisha kama hili inaweza kueleweka kiakili, bado haikubaliki kisheria wala kiutu. 

Tanzania ni nchi ya kisheria. Hata mtuhumiwa wa mauaji ya aina yoyote anastahili kufikishwa mbele ya mahakama na kupewa haki ya kujitetea.

Jeshi la Polisi limetoa taarifa kuwa askari wake walijitahidi kuzuia tukio hilo la kulipiza kisasi bila mafanikio, huku wawili wao wakijeruhiwa. 

Kitendo cha wananchi kuwazidi nguvu askari na kutekeleza hukumu ya umma ni ishara kuwa elimu ya kisheria na imani kwa vyombo vya dola ni finyu katika maeneo mengi. Hili ni tatizo linalopaswa kutazamwa kwa jicho la tatu.

Kwa sasa, ni muhimu kwa serikali kupitia Jeshi la Polisi na vyombo vya haki kuongeza juhudi za kutoa elimu ya uraia kuhusu njia sahihi za kushughulikia migogoro na uhalifu. 

Aidha, mashirika ya kiraia, viongozi wa dini na viongozi wa kijamii wana wajibu mkubwa wa kurejesha maadili ya heshima kwa maisha ya binadamu na kukuza ustaarabu wa kuamini katika mfumo wa haki.

Wakati tukilaani vikali mauaji ya Dickson Yusuph, hatupaswi kufumbia macho ukatili uliofanywa dhidi ya watuhumiwa waliokamatwa. Haki haipaswi kuwa ya kuchagua. 

Kama jamii, tunapaswa kuwa na misimamo ya msingi: tukatae mauaji; tukatae kujichukulia sheria mikononi; tukatae ukatili wa aina yoyote.

Ni wajibu wa vyombo vya dola kuhakikisha kuwa wale wote walioshiriki katika tukio la kulipiza kisasi wanakamatwa na kufikishwa mbele ya sheria. Ni kwa kufanya hivyo tu ndipo tutaimarisha misingi ya utawala wa sheria, utu na usalama wa wote katika jamii yetu.

Zaidi ya hayo, ni wakati wa kufanya tathmini ya kina kuhusu vyanzo vya migogoro ya kijamii inayochochea matukio kama haya.  Tatizo la ukosefu wa ajira, msongo wa mawazo, mmomonyoko wa maadili na ukosefu wa malezi bora vina mchango mkubwa katika kuibuka kwa hisia kali na vitendo vya kihalifu. 

Serikali na wadau wanapaswa kuwekeza zaidi katika huduma za afya ya akili, programu za elimu ya maadili shuleni pamoja na kuweka mazingira bora ya ajira kwa vijana ili kupunguza machungu yanayoweza kupelekea watu kuchukua hatua za kikatili.

Viongozi wa kisiasa nao hawawezi kusalia kimya. Katika majukwaa yao, wanapaswa kutumia nafasi hiyo kuhamasisha amani, uvumilivu na kuheshimu sheria. Badala ya kueneza kauli za kuchochea au kusaka umaarufu kupitia migogoro ya kijamii, viongozi wanatakiwa kuwa sehemu ya suluhisho. 

Ni kwa kushikamana kama taifa, kwa kila mtu kutimiza wajibu wake, ndipo tunaweza kujenga jamii salama, yenye misingi ya haki, utu na maelewano ya kweli