WAJUMBE wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wanajukumu kubwa la kuchagua wagombea watakaokiwakilisha chama chao kwenye majimbo na udiwani.
Kuna vyama vingine vya siasa ambavyo pia kwa sasa vipo kwenye mchakato wa kupata wagombea wao, hivyo mpambano katika uchaguzi utakuwa wa shika nikushike.
Uamuzi wa wajumbe wa vyama vyote hivyo ni wa muhimu kwa kuwa watakayempitisha ndiye atakayekwenda kusimama kwenye jimbo kwa ajili ya kuwawakilisha wananchi bungeni.
Kila chama ambacho kinaingia kwenye mchakato wa Uchaguzi Mkuu, lengo lake ni kupata mgombea atakayekiwakilisha chama chake vema ili kupata kiongozi bora.
Wajumbe kazi yao ni kusikiliza sera zinazotolewa na wagombea na jinsi wanavyojinadi na kupima kama wanafaa kuwa viongozi wazuri. Kuna wagombea ambao wamejitokeza kwa mara ya kwanza na kuna wale ambao wamejitokeza kwa zaidi ya mara moja kwenye uchaguzi uliopita.
Cha msingi ni kuangalia uwezo wa kila mgombea nguvu yake iliko. Kuna wagombea ambao ni wazuri wa kujieleza, lakini linapokuja suala la utekelezaji ni tatizo na matokeo yake wananchi huanza kulalamika.
Wagombea wengine si waongeaji, lakini vitendo vyao vinashawishi kumfanya achaguliwe kuwa kiongozi. Hata hivyo, kuna suala la watu kujisahau, anapopata uongozi tu, kila kitu alichokiahidi kinawekwa pembeni na kusubiri kipindi chake kinapokaribia kwisha ndipo anajitokeza kwa wananchi kuwashawishi wamchague tena.
Ushindani wa ndani wa vyama hasa chama talawa (CCM) ni mkubwa, ni kama wagombea wanapambana na wagombea wa vyama vingine.
Mgombea anapopita kwenye hatua ya kupitishwa kwenye chama chake ili kuwa mwakilishi wa jimbo, anakuwa amepitia mtihani mkubwa wa kupimwa na kukubalika.
Malalamiko katika kila mchakato wa uchaguzi ni lazima yajitokeze, uchaguzi ni uchaguzi, hata uwe wa kuwa kiongozi wa kaya ni lazima kutakuwa na mizengwe ya hapa na pale.
Jana ilikuwa siku rasmi ya Chama Cha Mapinduzi ya upigaji kura za maoni katika majimbo mbalimbali nchini. Ushindani wa vigogo wa chama hicho waliokuwa wakichuana kuwania jimbo ulifikia kilele chake kwa wajumbe kufanya uamuzi wa wanayemtaka awawakilishe.
Mchuano ulikuwa mkali na baadhi ya wagombea ukiwapima mizani ilikuwa inalingana, hivyo kazi ya kuangalia mzani huo umeegemea wapi ni ya wajumbe.
Utaratibu uliowekwa na chama katika kuwapata wagombea, uliridhiwa na wanachama wote ndio maana hata wale walioshindwa kupenyeza katika mchujo wa awali waliridhia na kukubali matokeo.
Wakati mchakato ukifanyika lazima kunakuwa na kambi za wapambe wanaomsapoti mgombea wao, lakini kazi ya kupiga kura inapomalizika na kumpata aliyepitishwa, kambi hizo huvunjwa na wanachama wote hubaki kuwa kitu kimoja kumuunga mkono yule aliyepitishwa.
Ukomavu wa chama na wanachama huonekana hapa, wa watu kuondoa tofauti zao na kutengeneza nguvu moja ya kutafuta ushindi.
Staili hii pia inatumiwa na vyama vingine na ndio maana mara nyingi uchaguzi humalizika kwa amani na kama kuna tofauti yoyote humalizwa kwa masikilizano na hali hubaki kuwa tulivu.
Kitu cha msingi ambacho wajumbe wanatakiwa kuwa nacho makini ni kujiepusha na kishawishi chochote cha rushwa. Kwa sababu rushwa ni adui wa haki na siku zote mtu anayetumia pesa kuingia madarakani, atahakikisha anazirudisha kwa kutumia madaraka yake
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED