Wastaafu ujumbe muupate na muuzingatie

Nipashe
Published at 12:22 PM Aug 06 2025
Wazee
AI
Wazee

WAFANYAKAZI wanapofikia umri wa kustaafu, mategemeo yao ni mapato wanayoyapata kwenye mafao yao yaweze kuwasaidia kuishi maisha mazuri mpaka siku zao za kuishi duniani zitakapotimia.

Baadhi yao wanapokuwa kazini huchelewa kujipanga kimaisha mpaka kipindi cha kustaafu kinapofika ndipo hushtuka wakati jua limeshazama kujipanga.

Na katika muda huo ndio wanapochanganyikiwa kutokana na kile anachokusudia kukifanya, ikiwamo ujenzi wa nyumba ya kuishi kutotosha na matokeo yake huingia kwenye mtego wa matapeli.

Kipindi cha kupokea mafao ndicho kinachotumiwa sana na matapeli kuwarubuni wastaafu ili fedha zao wapate kuziiba.

Matapeli ni wajanja huwafuatilia wastaafu hao na wanakuwa na uhakika wakiwarubuni watafanikiwa kuwanasa.

Kujipanga mapema ni jambo muhimu sana katika maisha kwa sababu mtu anajiwekea utaratibu mzuri wa kuishi bila kuwasumbua watu wengine.

Mtu anapofikia umri wa utu uzima ananyemelewa na maradhi mbalimbali na mafao yake yatamwezesha kujiweka katika maisha yatakayomwondoa kwenye manyanyaso kutoka kwa ndugu au jamii inayomzunguka.

Kwa kuepuka kuingia kwenye mtego huo, Wizara ya Fedha imewaasa wastaafu wanaolipwa mafao na Hazina kujiepusha na jumbe kwa njia ya simu zinazotumwa na watu wasiojulikana zikiwaelekeza kutuma fedha ili kuhakikiwa.

Hiyo ni njia moja inayotumiwa na matapeli hao kutapeli fedha za wastaafu kwa kuwalaghai kutuma taarifa zao kwenye simu.

Uhakiki wa taarifa za wastaafu hufanywa na Hazina na vile vile hakuna uboreshwaji wa pensheni za wastaafu kwa mtu mmoja mmoja.

Kwa mujibu wa Wizara ya Fedha, imekuwa ikipokea malalamiko kadhaa kutoka kwa wastaafu kuombwa fedha kupitia mitandao ya simu ili wafanyiwe uhakiki na kurekebishiwa viwango vya pensheni, ambazo wizara hiyo imetahadharisha kuwa taarifa hizo sio sahihi na kwamba hakuna gharama zozote anazotozwa mstaafu anayehudumiwa na Hazina.

Wizara ya Fedha kwa utaratibu wake inalipa mafao ya kustaafu na mirathi kwa watumishi waliostaafu wakiwa katika ajira yenye masharti ya kudumu na malipo ya uzeeni kwa waliokuwa hawachangii kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ambao walistaafu kabla ya tarehe 30 Juni, 2004.

Kadhalika, hakuna gharama zozote zinazohitajika Wizara ya Fedha kwa ajili ya kushughulikia mafao ya uzeeni na imesisitiza wastaafu kupuuza jumbe hizo kwa njia ya simu ya mkononi kwa kuwa wanaofanya hivyo ni matapeli.

Mstaafu yeyote anayepokea mafao kutoka Hazina anatakiwa kutoa taarifa kituo chochote cha polisi kilicho karibu naye anapoombwa fedha kwa ajili ya kupata huduma yoyote ya ofisi za Wizara ya Fedha.

Aidha, wananchi wametakiwa kutuma maoni, maswali au madai au kufika Ofisi ya Hazina ndogo mkoa anaotoka.

Wastaafu wanaotakiwa kuchukua tahadhari sio tu wanaopokea mafao yao kutoka Hazina, bali hata wale wanaopokea kutoka kwenye mifuko ya hifadhi ikiwamo ya NSSF na PSSSF.

Baadhi ya wastaafu wanaopokea mafao yao ya mkupuo, kutokana na kutojipanga huanza kuzitumia vibaya na wengine kuishia kwenye mtego wa matapeli.

Ndio maana baadhi ya taasisi zimeanza kutoa mafunzo ya kuwaandaa wafanyakazi wanaokaribia kustaafu kuanza kujipanga ili wasiingie kwenye mtego huo.

Kama mtu atakuwa hajajipanga ni bora mafao yake akayahifadhi mahala salama ambapo ni benki na hata kuwekeza kwenye hisa ambazo zitamwezesha kutunza mafao yake.