Msanii maarufu wa muziki wa Bongofleva mwenye ladha ya R&B na Afro-pop, Christian Bella, amepewa rasmi uraia wa Tanzania baada ya kuishi nchini kwa muda mrefu na kutimiza masharti yote ya kisheria.
Taarifa hiyo imetolewa jijini Dar es Salaam na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene, leo Alhamisi, Desemba 18, 2025, katika maadhimisho ya Siku ya Wahamiaji Duniani.
Akizungumza katika hafla hiyo, Simbachawene alisema Tanzania ina idadi kubwa ya wahamiaji, na baadhi yao wamekuwa wakipewa uraia baada ya kufuata taratibu zilizowekwa kisheria.
“Sasa anakwenda wapi? Amekwisha fika. Ameoa hapa, ana watoto hapa na atapata wajukuu hapa. Anafanya kazi vizuri, hana makosa, amefuata utaratibu na muda wote alioishi hapa amelipa malipo stahiki, siyo wengine wanaolanda-landa tu,” amesema Simbachawene.
Waziri huyo alibainisha kuwa uraia unaweza kufutwa endapo mhusika hatatii masharti, akisisitiza kuwa Serikali hufanya uchunguzi wa kina kabla ya kutoa uraia kwa mtu yeyote.
“Hatuwezi kumpa uraia mtu ambaye ni hatari au anayekuja kuwa hatari. Ndiyo maana kuna mchakato wa ‘vetting’ kabla ya mtu kupewa uraia,” aliongeza.
Awali, Christian Bella alikuwa raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), lakini ameishi Tanzania kwa miaka mingi akijishughulisha na shughuli za kisanii, huku akichangia kukuza tasnia ya muziki nchini.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED