Waandaaji wa mbio za hisani za ‘Rombo Marathon- 2025’ wametambulisha aina ya mbio zitakazobeba ujumbe wa mwaka huu, yaani ‘trail run’ ambazo wakimbiaji wake, watatembea msituni na kukimbia msituni.
Akizungumzia maandalizi ya mbio hizo leo Desemba 19, 2025, Mkuu wa Wilaya ya Rombo, Raymond Mwangwala, amesema mbio hizo za mwaka huu ni tofauti na miaka mingine, kwa sababu mbio hizo zitatumia siku tatu.
“Siku ya kwanza, itakuwa ni siku ambayo itakuwa tunaiita before party. Before party tumeshaandaa, kutakuwa kuna matenty (mahema), kuna eneo la vinywaji, kuna eneo la ndafu, kuna eneo la nyama choma, ambayo usiku wake, watu watakaa na wataifahamu Rombo, wataielewa kwa kupitia siku hiyo.
“Rombo Marathon, ni sehemu pekee ya kuja kupumzika, kwa sababu unaweza ukaja na familia yako. Itakuwa ni marathon, ambayo unafika unapumzika siku ya kwanza, siku ya pili sasa, ndio siku ambayo tunakimbia.
…Mkishakimbia hiyo siku ya pili, mnapata fleva za tofauti. Kwanza unauona Mlima Kilimanjaro kwa pembeni, lakini unaviona vijimito vinavyotiririka lakini unauona msitu. Ni mbio ambazo tunasema ni ‘trail run’ ambayo unatembea msituni, unakimbia msituni.”
Kwa mujibu wa Mwangwala, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika mbio hizo za Rombo Marathon zitakazofanyika Disemba 23 katika eneo lenye miinuko mikali na msitu wa asili wa Rongai, unaosifika kuwa nyani wa aina nne.
Mbio hizo zitakazowahusisha wakimbiaji kati ya 1,200 mpaka 1,700 walioingia mkoani Kilimanjaro ‘kuhiji’ sikukuu za mwisho wa mwaka za Krismasi na mwaka mpya.
Joseph Katembo, ambaye ni Mjumbe wa Kamati ya Ufundi ya Maandalizi ya Mbio za Rombo Marathon, amesema wakimbiaji wa mbio hizo ni Watanzania, lakini akitaka kuja mtu kutoak nje ya nchi,analazimika kuja na vibali vinavyomtambulisha ametokea nchi gani.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED