CHAN 2025 kuanza kesho: Kocha Morocco-Tupo tayari kucheza na timu yoyote

By Shufaa Lyimo , Nipashe
Published at 03:34 PM Aug 01 2025
Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Hemed Suleiman 'Morocco',
Picha: Mpigapicha Wetu
Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Hemed Suleiman 'Morocco',

Mashindano ya Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) yanatarajiwa kuanza rasmi kesho , Agosti 02, 2025, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, ambapo Tanzania (Taifa Stars) itamenyana na Burkina Faso katika mchezo wa ufunguzi utakaoanza saa 2:00 usiku.

Tanzania inakuwa mwenyeji wa mashindano haya kwa mara ya kwanza katika historia, kwa kushirikiana na Kenya na Uganda kama waandaaji wenza wa michuano hiyo ya Afrika.

Mchezo wa kesho unatarajiwa kuwa na ushindani mkali, huku makocha wa timu zote mbili wakieleza matarajio yao ya kuanza mashindano kwa ushindi.

Morocco: “Tupo Tayari, Tuna Kikosi Imara”

Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Hemed Suleiman 'Morocco', amesema kikosi chake kiko tayari kwa mchezo huo baada ya maandalizi ya muda mrefu, akieleza kuwa amekuwa akifuatilia mfumo wa uchezaji wa Burkina Faso na kuwa na imani ya kupata ushindi.

“Tupo tayari kukutana na timu yoyote katika mashindano haya kutokana na aina ya kikosi nilichonacho. Tumefanya maandalizi ya kutosha na wachezaji wote wako fiti,” amesema Morocco.

Kocha huyo ameongeza kuwa michezo ya kirafiki waliyocheza kabla ya mashindano imesaidia kupunguza presha kwa wachezaji, hasa chipukizi waliopo kwenye kikosi hicho.

“Wachezaji chipukizi wameonyesha kiwango kizuri na kushirikiana vyema na wazoefu. Tunaamini tunaweza kufanya vizuri na kuacha kombe nyumbani,” amesisitiza.

Kwa upande wa afya ya wachezaji, Morocco amesema hakuna majeruhi mkubwa isipokuwa Clement Mzize, ambaye ana majeraha ya kawaida yanayomruhusu kuendelea na mazoezi huku akisubiri tathmini ya mwisho kutoka kwa daktari wa timu.

Aidha, amewataka mashabiki wa soka nchini kujitokeza kwa wingi kuisapoti Taifa Stars ili kuwapa wachezaji nguvu ya kupambana zaidi.

1

Manula: “Tutapambana Kulinda Heshima ya Nyumbani”

Mchezaji wa kikosi cha Taifa Stars, mlinda mlango Aishi Manula, akizungumza kwa niaba ya wachezaji wenzake, amesema lengo kuu ni kukusanya pointi nyingi katika hatua za mwanzo ili kujiweka vizuri katika kundi lao.

“Tunajivunia kucheza kwenye ardhi ya nyumbani. Tutapambana kuhakikisha tunashinda michezo yetu ya mwanzo,” amesema Manula.

Amesema mashindano ya CHAN ni makubwa kuliko mashindano yoyote yaliyowahi kufanyika nchini, na kwamba ni jukwaa muhimu kwa wachezaji chipukizi kujitangaza mbele ya mawakala na mashabiki kutoka sehemu mbalimbali za Afrika.

Burkina Faso: “Tupo Tayari Licha ya Changamoto”

Kwa upande wake, Kocha Mkuu wa Burkina Faso, Issa Balbone, amesema kikosi chake kiko tayari kwa mchezo huo licha ya kuchelewa kufika nchini.

“Najua Tanzania ina wachezaji wengi wazuri, lakini nasi tupo tayari. Tumekuja kushindana na malengo yetu ni moja — ushindi,” amesema Balbone.

Mchezaji wa timu hiyo, Patrick Ilalo, amesema hawana wasiwasi na mechi ya leo licha ya kuwa Tanzania ni mwenyeji wa mashindano.

“Tumejipanga kuhakikisha tunaiheshimisha nchi yetu. Tutafuata maelekezo ya benchi la ufundi ili tufikie lengo la kubeba Kombe la CHAN,” amesema Ilalo.