Makocha wa Afrika waigombea Simba

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 11:59 AM Dec 16 2025
news
Picha Mtandao
Makocha wa Afrika waigombea Simba

WAKATI mabosi wakiendelea na mchakato wa kusaka mrithi wa Dimitar Pantev, makocha mbalimbali wameendelea kuwasilisha maombi Msimbazi akiwamo Mkurugenzi wa Ufundi wa TS Galaxy ya Afrika Kusini, Nermin Basic, imefahamika.

Habari kutoka Afrika Kusini zinasema kocha huyo raia wa Bosnia naye ametuma maombi ya kazi kwa mabosi wa Simba na tayari ameanza kujadiliwa kuchukua nafasi hiyo ya kuwaongoza Wekundu wa Msimbazi.

Chanzo chetu kinasema Basci anapewa kipaumbele sawa na Steve Barker, kocha wa zamani wa Stellenbosch FC, ambaye sasa anaifundisha AmaZulu inayoshiriki Ligi Kuu ya Afrika Kusini.

Kwa mujibu wa magazeti na blogu za michezo Sauzi, zinasema mkurugenzi huyo ndiye ana nafasi kubwa zaidi ya kutua Simba na kumfunika Barker ambaye hatua za mazungumzo zilikuwa zinaendelea vizuri.

"Kwa sasa kuna takribani makocha wanne ambao Simba wanawapa kipaumbele zaidi. Wawili wanatoka Afrika Kusini. Mkurugenzi wa Ufundi wa TS Galaxy na Steve Barker. 

Pia kuna mmoja kutoka Algeria, aliyewahi kuifundisha US Monastir, kama sikosei. Mkurugenzi wa Ufundi wa TS Galaxy ndiye chaguo namba moja. Yeye ndiye kipaumbele chetu kwa sasa,” kilieleza chanzo hicho kwa jarida la Soccer Laduma la Afrika Kusini jana.

Basic ambaye kwa sasa ndiye Mkurugenzi wa Ufundi wa TS Galaxy, pia amewahi kukinoa kikosi cha US Monastir.
 Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema makocha 240 wamepeleka maombi ya kutaka kuifundisha Simba ambayo imefungwa michezo yote miwili ya hatua ya makundi kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ambayo wamecheza.

"Mara baada ya kuachana na Pantev viongozi wapo katika mapitio ya maombi mbalimbali ya watu ambao wameomba wenyewe, pamoja na makocha ambao tunawaangalia sisi wenyewe walikuwa katika timu nyingine barani Afrika.

Tunategemea na kukusudia hadi kufikia Desemba 28, kikosi kitakaporejea mazoezini, tayari tuwe tumekamilisha kulisuka benchi zima la ufundi.

Nichukue nafasi hii kuwaambia wanachama na mashabiki wa Simba wasiwe na wasiwasi, tunafanya kazi kwa ukamini ili tupate kocha mzuri atakayekuja kuinufaisha Simba,viongozi wanafanya tathimini, wanapitia rekodi, wasifu na sifa muhimu ili kujiridhisha kabla ya kufanya maamuzi, awe ni mwalimu mzuri, atakayekuja kufanya kazi ya kupendeza ndani ya klabu ya Simba," Ahmed alisema.

Baadhi ya makocha wanaotajwa kupeleka maombi, yumo aliyewahi kuifundisha Yanga kwa muda mfupi, Romain Folz, Erick Tinkier, Msauzi, aliyewahi kufundisha Orlando Pirates, Cape Town City, SuperSport United, Mzambia Honor Janza, aliyewahi kuiongoza Taifa Stars na Namungoa na Nikodimos Papavasiliou 'Nikki', ambaye kwa sasa anaifundisha Ghanzil El Mehalla ya Misri.

Wengine ni Amine El Karam, Mmorocco na  kocha wa zamani wa RS Berkane na Hubert Velud, kocha aliyekuwa akiziongoza USM Alger (Algeria), AS FAR na Etoile du Saleh (Morocco) na TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.