KLABU ya Mashujaa FC, imetangaza kumsajili straika wake wa zamani, Ismail Mgunda, aliyetokea klabu ya AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, baada ya kuitumikia kwa miezi minne.
Taarifa iliyotolewa jana na klabu hiyo, inasema kuwa imemrejesha tena mshambuliaji wake huyo baada ya kumaliza mkataba wake wa muda mfupi na timu hiyo. "Karibu tena nyumbani Mgunda,"ilisomeka sehemu ya taarifa ya klabu hiyo.
Mchezaji huyo anakuwa wa kwanza kutambulishwa na klabu hiyo, ambayo ipo kwenye hatua za mwisho wa usajili kwa wachezaji inayowaona inawafaa kwa msimu ujao wa mashindano.
Mgunda, aliondoka nchini Januari mwaka huu, kipindi cha dirisha dogo la usajili kuelekea nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kujiunga na timu hiyo.
Aliondoka nchini akiwa amepachika mabao manne, huku bao moja akilifunga kwa kichwa nje ya boksi, ambalo linabaki kwenye kumbukumbu kuwa ni bao pekee msimu huu kufungwa hivyo ambapo mengi ya kujitwisha hufungwa ndani ya eneo la hatari.
Meneja wa timu hiyo, Athumani Amiri, amesema kuelekea msimu ujao, benchi la ufundi limeelekeza kusajili mastraika wenye uwezo mkubwa kwani rekodi zinaonesha kuwa ndilo eneo ambalo liliwaangusha msimu uliopita.
"Tunaendelea na usajili, maeneo ambayo tumeyatilia mkazo zaidi msimu huu kwenye usajili, ambayo hatukufanya vizuri msimu ujao ni eneo la ushambuliaji. Hili lilikuwa tatizo sana msimu uliopita kwa klabu yetu ya Mashujaa," alisema meneja huyo.
Wachezaji wengine mabao wanadaiwa kuwa wamejiunga na timu hiyo na huenda wakatangazwa wakati wowote ni kiungo, Samuel Onditi na beki wa kati, Mohamed Mussa, wote kutoka, Kagera Sugar, winga machachari, Selemani Bwezi wa KenGold, iliyoshuka daraja, winga na kiungo mshambuliaji, Salum Kihimbwa na Fountain Gate, pamoja na straika, Mudathir Said wa Mbeya City.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED