BAADA ya taarifa za kuwahitaji kwa mkataba wa mkopo wachezaji wawili wa Simba, Ladack Chasambi na Awesu Awesu, Mbeya City imepiga hodi Yanga ikitaka kumsajili winga, Farid Mussa, ili kukiimarisha kikosi chao kinachoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara.
Habari kutoka ndani ya Mbeya City zinasema hayo ni mapendekezo ya kocha mpya wa timu hiyo, Mecky Maxime, ambaye anataka kukiongezea nguvu kikosi chake.
Chanzo hicho kilisema Maxime anaamini usajili wa kipindi cha dirisha dogo utawasaidia kuondoa makosa waiyofanya katika michezo iliyotangulia.
“Kocha anaamini anaweza kuwapata wachezaji hao kutoka Simba na Yanga kwa sababu hawapati nafasi za kucheza kwa sasa kufuatia ushindani wanaokutana nao,” kiliongeza chanzo chetu.
Taarifa zaidi zinasema wakati kukiwa na mazungumzo ya kuwachukua Chasambi na Awesu kutoka Simba kwa mkopo, Mbeya City inamtaka Farid ama kwa kumsajili moja kwa moja, au kwa mkopo.
Hii ni mara ya pili kwa Mbeya City kujaribu kumsajili Farid, anayecheza winga ya kushoto wakati mwingine akiwa na uwezo wa kucheza kama beki wa kushoto, ambapo ilitaka kumsajili mwanzoni mwa msimu huu.
"Ni mchezaji tuliyemhitaji tangu dirisha kubwa lililopita ila kuna mambo hayakwenda vizuri na kushindwa kupata saini yake, lengo letu ni kuwapata wachezaji tunaowahitaji mapema ili kuepuka ushindani utakapoanza,” kilisema chanzo hicho.
Naye Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe, amekiri baadhi ya wachezaji wao watatolewa kwa mkopo kipindi cha dirisha dogo ingawa hakuwataja majina.
Kamwe alisema tayari Kocha Mkuu, Pedro Goncalves, ameshawasilisha majina ya wachezaji ambao anataka watolewe kwa mkopo.
"Tayari kocha Pedro ameshawasilisha majina kwenye Ofisi ya Ofisa Mtendaji Mkuu wa klabu. Ameelezea maeneo ambayo anahisi yanatakiwa yaboreshwe ndani ya kikosi chetu, amewasilisha pia majina ya wachezaji ambao anaamini tunatakiwa kuwatoa kwa mkopo ili wakapate changamoto sehemu nyingine," alisema Kamwe.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED