WACHEZAJI 22 waliochaguliwa kupitia mchakato wa kutafuta vipaji vya mpira wa miguu katika mikoa ya Mbeya, Arusha, Mwanza na Dar es Salaam, watakaoiwakilisha timu ya mabingwa ya Safari Lager mwaka huu imetangazwa.
Kwa mujibu wa taarifa ya klabu hiyo, timu hiyo itakutana na klabu ya Yanga katika fainali ya Kombe la Safari Lager Julai 26, mwaka huu, kwenye uwanja wa KMC Dar es Salaam.
Ilisema kombe lilianzishwa kwa lengo kuu la kuibua na kukuza vipaji vya soka vya vijana nje ya mfumo wa klabu za kitaalamu.
“Mashindano yalikuwa wazi kwa wachezaji wenye umri kati ya miaka 18 hadi 24 na yalifanyika kwa mfumo wa bonanza chini ya usimamizi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF),” imesema sehemu ya taarifa hiyo.
Klabu hiyo imesema imeshirikiana na makocha wabobezi pamoja na wawakilishi wa jamii kuwachambua wachezaji, na kufanikiwa kupata timu iliyotambulishwa kama Safari Champions iliyochaguliwa kwa kuzingatia uwezo wa kiufundi na ushiriki wa mashabiki kupitia tovuti maalum.
“Lengo letu katika hili halikuwa tu kuandaa mashindano. Tulitaka kuunda tukio litakalobadili namna vipaji vya soka vinavyogunduliwa na kusherehekewa. Vijana hawa hawakusajiliwa walionekana. Na makocha, mashabiki, na jamii zao. Hii ni timu iliyojengwa na watanzania,” imesema.
Aidha, ilielezwa kuwa klabu ya Yanga imeungana na timu hiyo kama sehemu ya juhudi za pamoja za kuendeleza soka la nyumbani.
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga Ally Kamwe amesema wanajivunia kuwa sehemu ya simulizi inayorudisha mpira kwa watu.
"Huu si mchezo wa kawaida tunaupokea kwa mikono miwili tunaamini katika nguvu ya soka kwa kuunganisha vizazi,” amesema Kamwe.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED