VINARA wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba wamesema wamejiandaa vyema kwenda 'kuizima' na 'kuondoa ukubwa' ambao Tabora United 'imejivika' kuelekea mechi ya ligi hiyo itakayochezwa keshokutwa kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mkoani, Tabora.
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, aliliambia gazeti hili jana kikosi chao kiko tayari kumaliza tambo za Tabora United kwa kuwaonesha wao bado ni timu ya daraja la kati.
Ahmed alisema majigambo hayo yote yanayotokea sasa ni kwa sababu mabingwa watetezi, Yanga na Azam FC walikubali kufungwa na Tabora United, vinginevyo yasingekuwepo.
Alisema kikosi chao kitaondoka jijini, Dar es Salaam kesho kuelekea Tabora tayari kwa mchezo huo ambao unasubiriwa kwa hamu na mashabiki na wadau wa soka nchini.
"Sisemi Tabora United ni timu mbaya, ila imekuwa na kiburi, mdomo na kujiamini kwa sababu ya kuzifunga Yanga na Azam, sasa tutakwenda kuwaonesha sisi sio hao ambao wamewafunga, sisi ni 'levo' nyingine kabisa, tunakwenda kuwaonesha wao ni timu ya daraja la kati na bado haina ukubwa huo inaojipa," alisema Ahmed.
Aliongeza wachezaji wa Simba wako imara kuhakikisha wanapata ushindi katika mechi hiyo na kumaliza maneno, tambo na vijembe vinavyoendelea nje ya uwanja, kabla dakika 90 za kupambana dimbani.
Tabora United itashuka uwanjani ikiwa na ahadi ya kupewa bonasi ya Sh. Milioni 50 kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora endapo itaifunga Simba katika mchezo huo.
Katika mechi ya keshokutwa, huenda Tabora United ikamkosa straika wake tegemeo, Heritier Makambo, ambaye anatumikia adhabu ya kuoneshwa kadi tatu za njano na winga, Yacouba Songne, ambaye ni majeruhi.
Pia kuna taarifa wachezaji wapya wa Tabora United waliosajiliwa kipindi cha dirisha dogo bado hawajapata vibali vya kufanya kazi nchini na kama mchakato huo hautakamilika, nyota hao pia wana hatihati ya kucheza mchezo huo.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Tabora United, Charles Obini, alisema kuelekea mechi dhidi ya Simba, yapo baadhi ya mambo wameyatatua na mengine yapo nje ya uwezo wao.
"Ni kweli, Makambo ana kadi tatu za njano, hawezi kucheza mchezo huo, Yacouba Songne yeye alikuwa majeruhi, ameanza mazoezi lakini kucheza kwake itategemea na kocha atakavyoona kama atakuwa amepona vizuri, hawezi kulazimisha kama hakuwa vyema.
Kuhusu wachezaji wapya, wote tayari tumewalipia vibali, tunachosubiri ni leseni tu, tukipata watacheza," Obini alisema.
Aliongeza kikosi chao kimejiandaa kucheza mechi hiyo dhidi ya Simba kama wanavyojiandaa na michezo mingine ya Ligi Kuu Tanzania Bara.
"Tunajiandaa kama tunavyojiandaa na timu nyingine, hakuna mechi spesho eti kwa sababu tunacheza na Simba, maandalizi yetu ni yale yale tu kama tulivyojiandaa dhidi ya Yanga, KenGold, JKT Tanzania, Azam na timu nyingine, morali iko juu na tuna imani matokeo yatakuwa mazuri.
Vijana wanajiandaa vizuri, wachezaji wetu wageni nao wako vizuri, naamini mechi itakuwa nzuri kulingana na mipango yetu, sisi hatuna presha, tunajua mpira una matokeo matatu, tunaenda kucheza ili kupambana, litakalotokea sawa tu, hata tulipoenda kucheza dhidi ya Yanga hakuna aliyetegemea tutashinda, wenye presha ni Simba," Obini alisema.
Katika mechi iliyochezwa Agosti 17, mwaka jana, kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam, Simba ikishinda mabao 3-0, yaliyofungwa na Che Fondoh Malone, Velentino Mashaka na Awesu Awesu Tabora United ilimkosa Makambo, Songne na wachezaji wengine ambao taratibu za usajili zilikuwa hazijakamilika.
Baada ya kusogezwa mbele kwa Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN), hadi Agosti 2, mwaka huu, Ligi Kuu Tanzania Bara inarejea rasmi kuanzia kesho kwa Yanga kuwakaribisha Kagera Sugar kwenye Uwanja wa KMC Complex.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED