RIPOTI ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere ya mwaka 2022/2023 inaonesha kwamba wagonjwa wa afya ya akili wanaongezeka kila mwaka na vifo.
Kwa mujibu wa CAG, kumekuwa na ukosefu wa umakini katika kutambua watu wenye tatizo la afya ya akili, badala yake juhudi za utambuzi zinazingatia makundi mengine, na kwamba huduma za kisaikolojia na kijamii hazijaingizwa kikamilifu katika mipango, bajeti, sera na programu katika ngazi mbalimbali za utawala.
Aidha, mzigo wa matatizo ya afya ya akili miongoni mwa vijana unasababisha mambo makubwa matatu ambayo ni msongo wa mawazo, kujiua ikiwa ni sababu inayoshika nafasi ya pili kwa vifo vya vijana kati ya umri wa mika 15-19 na tatizo linaloongoza ni matumizi mabaya ya pombe na mihadarati.
Mbali na sababu hizo, nyingine ni msongo wa kiwango cha juu, shinikizo la makundi rika na matukio yenye tishio la maisha kama vile majanga, ukatili, unyanyasaji na migogoro katika familia.
Wakati hali ikiwa hivyo, kumekuwapo na biashara ya visu, mapanga na silaha nyingi za asili ambazo ni hatarishi kwa kufanywa hadharani, kwani inaweza kusababisha madhara kwa watu wasio na hatia.
Uuzwaji wa mapanga na visu kiholela mitaani, mtindo ambao kwa sasa unaonekana kama jambo la kawaida, lakini ninadhani unaweza kusababisha madhara makubwa tahadhari zisipochukuliwa.
Wale wanaoshi Dar es Salaam watakuwa wameshudia uuzwaji wa silaha hizo kwenye mkusanyiko wa watu, kitendo ambacho akitokea mwenye tatizo hilo anaweza kusababisha makubwa kwa watu wasio na hatia.
Wakati mwingine wauzaji wa silaha hizo huwafuata madereva, hasa katika katika makutano ya barabara na kuwaonyesha silaha hizo kupitia dirishani kitendo ambacho ninadhani nacho sidhani ni sahihi.
Katika karne hii yenye kesi za tatizo la afya ya akili, inaogopesha kuona visu, mapanga na vinginevyo vinaruhusiwa kuuzwa waziwazi barabarani tena hata bila kufichwa katika mifuko yake.
Ninadhani serikali haina budi kuangalia upya mtindo huo, kwa kupiga marufuku silaha hizo kuuzwa hadharani na tena kwenye mkusanyiko wa watu mbalimbali hata wenye tatizo la afya ya akili.
Ugonjwa afya ya akili kwa dunia ya sasa unazidi kuwakabili watu wa rika mbalimbali na jinsi tofauti, lakini kuna mazingira yanayoweza kuleta madhara, hasa uuzaji wa silaha za jadi kiholela.
Inawezekana mtu akakorofishana na mwenzake kwenye maeneo yanayouzwa silaha na kuchukua na kumdhuru kirahisi, hivyo njia nzuri kudhibiti biashara hiyo isiuzwe kiholela.
Ninaelezwa hivyo, kwa sababu imekuwa ni la kawaida kukuta wamachinga wakiuza visu, mapanga na silaha nyingine za jadi kwenye mkusanyiko wa watu, kitendo ambacho kinaweza kusababisha hatari.
Wataalam wa saikolojia anasema mtu akiwa na msongo wa mawazo unaotokana na hilo tatizo la afya ya akili, anaweza kufanya tukio lolote baya wakati wowote na mahali popote na katika mazingira yoyote, hivyo, ni vyema mtindo wa kuuza vitu hatari kiholela ukadhibitiwa.
Inasikitisha kusikia kwamba nusu ya magonjwa yote ya akili duniani yanaanza katika umri wa miaka 14 na mengi ya hayabainiki wala kutibiwa, hali ambayo inatatanisha mustakabali wa vijana wengi.
Hivyo, kwa kuwa hayabainiki wala kutibiwa, suala la kuchukua tahadhari ikiwamo kuepuka mazingira hatarishi kama hayo ya kuuza silaha hilo kienyeji kama inavyofanyika sasa.
Njia salama ni kupiga marufuku uuzaji holela wa silaha hizo, vinginevyo itakuwa ni sawa na kujitengezea mazingira yanayoweza kuleta madhara makubwa hapo baadaye.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED