KUNA baadhi ya watu wamekuwa na tabia tofauti, hususani wanaume wameonekana kuwa wahusika wakuu kwenye tabia hii ya kuweka haja ndogo kwenye chupa na kutupa barabarani au kwenye mitaa wanayokaa watu.
Ni jambo ambalo sio sahihi kijamii kiafya na mazingira, kwani katika hilo kuna baadhi ya watoto wanaokota chupa na kumwaga mikojo hiyo kisha, wanachezea au wanazisuuza na kuwapelekea wauza juisi wanaozinunua.
Kuna wakati inabaki hilo kuwa shida kidogo kwa watoto ambao hawajafikia umri unaotambulika, kwani suala la kunywa mikojo hiyo wakidhani ni juisi inaleta ukakasi, pia hatari kiafya.
Napenda katika hilo kutoa mfano hai katika eneo la Gereji, katika Barabara ya Mandela, Dar es Salaam, Manispaa ya Ubungo, ambako kunabeba sifa ya kusheheni chupa za namna hiyo zimejaa mikojo mitaani.
Nasema hali ya kuwapo chupa hizo zinazofikia kwa waokota makopo, wakisaidiana na watoto wanaotafuta ‘chochote kitu’ ni hatari.
Hata hivyo, kwa mujibu wa wakazi hao eneo la Gereji, Dar-es Salaam, Mtaa wa Mwongozo Manispaa ya Ubungo, kunakolalamikiwa ni tabia imekuwa endelevu mtaani, kukitupwa chupa za mikojo, zikiacha hatari ya afya kwa watoto wao.
Nipashe ilishawahi kudodosa kupata ushuda kupata ushahidi kwa wahusika, ambako mkazi mwenye dhamana akakubaliana na malalamiko hayo, akiwa na maelezo ya kuwapo tabia iliyokithiri watu kutupa chupa za mikojo mtaani.
Mkazi huyo akarejea mtazamo wake katika lugha ya kujitambua namna hatari inayowasogelea watoto wao mitaani, wengi wenye umri kati ya miaka minne na mitano.
Kwa mujibu wa ufafanuzi wake, kunakundi la wateja wa juisi, huku katika rika la hao ‘dogo’ kuna baadhi wanaotaka kuonja ladha ya kitu kilichopo kwenye chupa na ndipo wanaangukia janga baya.
Hapo mfafanuzi akaenda mbali akiwa na matamshi kuwa “sina hakika sana, ila nadhani ni sababu ya watoto kusumbuliwa na matumbo.
“Wengine wanaumwa UTI, ukweli wanaotupa chupa hizo ni walevi na watu wanaovuta bangi, mtu anayejielewa hawezi kufanya hivyo.”
Licha ya kuwapo nyakati chupa hizo hazionekani, bado inabaki sababu ya kuokotwa makopo, ila kuna wakati hatari zaidi baadhi ya watoto wengine kuokota na kupeleka kwao, ili waziwekea juisi za kuuza.
Mkazi mwingine wa eneo hilo, Daniel Nshoma, naye akaisumilia Nipashe, kuwa ni tabia hatari kwa afya za watoto walio katika rika la kujitambua.
Hapo ikimaanisha pale wanajamii ambao ni wadogo, wanapokunywa juisi akirejea mfano wa majumbani mwao, hata mafuta ya taa yakiwekwa vibaya, huangukia janga la watoto kuyanywa.
Niseme, hapo ingependeza kwa wananchi kwa pamoja, kushirikiana kufichua undani ulioko kwa watu hao wanasambaza makopo ya haja ndogo, wanachafua mazingira na vitendea vikopo vya maji.
Kwenu wananchi hii ni hatari, jambo la busara tunapaswa kukabliana nayo huku mamlaka za kiserikali zikifuatilia.
Hata hivyo, jema lililoko katika mwamko wa utendaji wakijitahidi kuwahi kuokota chupa hizo zenye haja ndogo zikisambazwa na watu wasiojulikana, wakiwahatarisha zaidi watoto na hata watu wazima.
Hata hivyo, gazeti letu lilifanikiwa kuongea na kiongozi katika mtaa wa serikali unaohusika, akinena si mhusika naye akanirejesha kwa idara ya afya, kisha kwa msemaji wa manispaa husika, aliyempa ofisa kata mwenye dhamana kuendeleza ufafanuzi.
Hata hivyo, mkazi mwingine wa eneo hilo kwa jina moja, Sarah, akaungana na ufafanuzi kwamba jambo linalokera na linahitaji kukomeshwa haraka kwa wahusika kukumbana na hatua kali.
Bila shaka uongozi wa mtaa una salamu, sasa ufuatilie kelele za kero na sio tofauti, kwani inachafua sura ya eneo husika.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED