Hongera Taifa Stars, mmeonesha mnaweza

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 05:33 PM Aug 04 2025
Tanzania imenza vizuri katika michuano hii
Picha: CAF
Tanzania imenza vizuri katika michuano hii

KIKOSI cha timu ya taifa ya Tanzania kimeanza kwa kishindo fainali za Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN).

Ni baada ya kuichakaza timu ya taifa, Burkina Faso, mabao 2-0, mechi ikichezwa, Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam. 

Ilikuwa ni furaha kwa mashabiki wa soka Tanzania, ambao walijitokeza kwa wingi na kuwaonesha waandaaji na wageni kuwa pia tunastahili kuwa wenyeji wa mechi ya ufunguzi wa fainali za Mataifa ya Afrika, AFCON, 2027. 

Pongezi wa wachezaji wa Stars kwa kuthamini ujio wa mashabiki wengi, walipowafurahisha kwa kucheza kandanda safi na la kuvutia, huku wakichagizwa na kelele, vifijo na ndelemo za mashabiki uwanjani. 

Mashabiki wa soka walitoka pembe zote za nchi na kukutana, Uwanja wa Mkapa, kuwashangilia mashujaa, ambao walionesha kweli na askari waliotumwa na nchi kufanya kazi kwa ajili ya taifa. 

Kazi waliofanya mashabiki ilionekana hasa, kwani waliwatia moyo wachezaji, wakawashangilia, wakawazoea wapinzani na kuwakatisha tamaa kwa miluzi na mbinja. 

Wachezaji wa Stars walipokuwa na mpira, mashabiki walizidisha kushangilia kiasi cha kuwafanya kuwa wepesi kwenda kwa wapinzani na kuwatia ndimu ili kufanya mashambulizi makali ambayo yaliwapoteza kabisa, Burkina Faso. 

Nadhani wachezaji wa Burkina Faso hawajawahi kukutana na umati kama ule, hivyo kelele na mashabiki  ziliwafanya wachanganyikiwe pale wanaposhambuliwa na kusababisha kufanya makosa mengi mara kwa mara. 

Nitoe pongezi wa Serikali Kuu chini ya Rais, Samia Suluhu Hassan, kwa kuwezesha kufanyika kwa fainali hapa nchini, lakini pia kutengeneza miundombinu ya uwanja, barabara, mahoteli, viwanja vya mazoezi, na mengine mengi yaliyowezesha CHAN kufanyika, huku mechi ya ufunguzi na sherehe zake kufana kwa kiwango cha hali ya juu. 

Pongezi pia ziende kwa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kuratibu kwa usahihi kila kilichokuwa kinahitajika kwenye michuano hiyo na kuanza kwa kishindo na ufanisi mkubwa kama ilivyopangwa. 

Baadhi ya Wakuu wa mikoa na wasaidizi wao nao wastahili sifa kwa kujitolea kusafirisha mashabiki kutoka mikoa yao na kuwapeleka Dar es Salaam kwa ajili ya kuishangilia Stars, huku malengo yakiwa yametimizwa kwa ushindi kwa kwanza mechi ya ufunguzi. 

Kama alivyosema Kocha Mkuu, Hamed Morocco kuwa safari hii Stars ina kikosi imara kuliko vyote vilivyowahi kutokea huko nyuma, hivyo Watanzania wote tuna imani kubwa na vijana wetu kuwa tunaweza kulibakisha kombe nyumbani. 

Kwa jinsi tulivyoona katika mechi ya ufunguzi, uwezo huo upo kwa asilimia kubwa, ukichanganya na ‘vibe’ la mashabiki wetu misheni ya kulibakisha kombe itafanikiwa. 

Mungu ibariki Tanzania, Mungu wabariki viongozi wetu, wachezaji wa Stars, mapambano bado yanaendelea.