Katika hili la rushwa, CCM wekeni kando kuoneana haya au majina...

By Beatrice Moses , Nipashe
Published at 01:58 PM Jul 17 2025
Mchakato huo huishia wananchi kuchagua viongozi kwa kupiga kura Oktoba
Picha: Mtandao
Mchakato huo huishia wananchi kuchagua viongozi kwa kupiga kura Oktoba

MAJI ukiyavulia nguo huna budi kuyaoga ni msemo wa wahenga ambao naweza kuutumia kuwakumbusha viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM).

Hao ni wale mapema walijinadi kubadilisha mfumo wa mchakato wa ndani wa uteuzi wa wagombea wa nafasi za ubunge, ujumbe wa Baraza la Wawakilishi na udiwani kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu ujao mwaka huu.   

Ilibainishwa kuwa mchakato huo umeboreshwa kwa kuongeza idadi ya wajumbe wapiga kura kuanzia ngazi ya kata hadi wilaya, ikiaminika inasaidia kuzuia vitendo vya rushwa kwa namna fulani.

Rushwa ni tatizo kubwa katika maeneo kadhaa, baadhi za sekta za umma na binafsi, pia ndani ya vyama vya siasa.

Hivi karibuni imeripotiwa kuwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Kilimanjaro imewahoji wagombea 11 wakituhumiwa kujihusisha na kutoa rushwa kwa wajumbe na wapambe ili waweze kupitishwa kwenye mchakato husika.

Pia, gazeti Nipashe limeripoti kuwa mkoa fulani kuna wajumbe wanaodaiwa wameshajipangia kiwango cha fedha (rushwa) wanachopaswa kupewa, ili kumchagua mgombea kulingana na nafasi ya ubunge au udiwani anayoomba.

 Rushwa imekuwa ikipigiwa kelele za kupingwa kwa miaka mingi, lakini ni wazi inaonekana inazidi kukomaa, badala ya kutepeta, hali inayoweza kuthibitishwa na taarifa kadhaa za matukio yake.

Taasisi kadhaa, vikiwamo vyombo vya habari vimepaza sauti kukemea ama kuibua, namna rushwa inavyoathiri maendeleo ya jamii, licha ya kuwapo sheria ya zinazopaswa kutumika kuwashughulikia wahusika Bado kuna watu ni jasiri wa kutoa na kupokea rushwa.  

CCM ni chama kikongwe na tawala cha kisiasa nchini, hivyo kinapaswa kuendelea kuwa mfano bora kwa vyama vingine na wananchi kwa ujumla, kunapoibuliwa tuhuma za uwepo wa rushwa siyo sifa njema.

Licha ya TAKUKURU kutoa tahadhari bado kuna wanasiasa ambao wamejitokeza kuonesha jinsi walivyo ‘wataalami’ wa kutoa rushwa kufanikisha wanayoyakusudia.

Sijui kama hawajui uwepo wa Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11 ya 2007 (PCCA) 2. Sheria ya Uchaguzi wa Kitaifa Namba 1 ya 1985; Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Namba 4 ya 1979 (na marekebisho yake yote).

 Katika kitabu kinachoelezea kuhusu Makosa ya Rushwa Katika Chaguzi Tanzania kilichotayarishwa kwa ushirikiano kati ya POLICY FORUM na TAKUKURU, imebainisha mambo kadhaa ikiwamo  kubainisha kuhusu Sheria ya Uchaguzi wa Kitaifa Namba 1 Isemavyo Sheria ya Uchaguzi wa Kitaifa Namba 1 ya 1985, Kuhusu Makosa ya Rushwa Katika Uchaguzi 985.

Pia, kuna Makosa ya Rushwa Katika Uchaguzi Sheria inahusika na kuongoza uchaguzi wa rais, wabunge na madiwani.

Sheria inatoa taratibu na mamlaka mbalimbali, ikiwamo kuanzishwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, dhidi ya Ushawishi wa Rushwa Kujiondoa Kugombea

Ushawishi wa Rushwa Kujiondoa Kugombea kwenye Kifungu 112, mtu atakuwa ametenda vitendo vya rushwa, endapo atamshawishi au kumnunua mtu mwingine ajiondoe kugombea kwenye uchaguzi.

Inataja adhabu ya atakayepatikana na kosa hilo la kujiondoa na kumshawishi au kumnunua mwingine, akitiwa hatiani atahukumiwa kwenda kifungoni.

Kuna mengi yanayoelezwa, ikiwamo namna mtu atachukuliwa kuwa ana hatia ya hongo, kabla au wakati wa kampeni yeye au kwa kutumia mtu mwingine alitoa.

Inaweza kuwa kwa kukopesha, au kununua au kuhifadhi fedha yeyote au kitu cha thamani kwa mpiga kura au mtu yeyote kwa niaba ya mpiga kura ili apigiwe kura au kuzuia kupiga kura.

Hayo ni baadhi ya yanayotajwa katika sheria. Jambo la ajabu ni kwamba wagombea licha ya kuwa wanaosaka nafasi za kuwa wawakilishi wa wananchi.

Pia, kuna nafasi nyingine nyeti ikiwamo uwaziri ‘uspika’ au ‘umeya’ wanaweza kuteuliwa baada ya  kushinda kwenye uchaguzi.

Hao hawapaswi kufumbiwa macho kwa kuwa hawa ni miongoni mwa vinara wanaoeneza rushwa katika taasisi mbalimbali hivyo kusababisha huduma kadhaa ambazo zinapaswa kutolewa bure kwa wananchi kutolewa kwa upendeleo, hali ambayo huzusha manung’uniko.

Hivyo viongozi waadilifu ndani ya CCM, wanapaswa kuhakikisha wanasimama kidete bila kuangalia jina wala sura ya mhusika.

Wahakikishe walaji na watoa rushwa wote wanashughulikiwa, kama hotuba ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere inavyotukumbusha, ili kukomesha tabia hiyo ndani ya tetesi hizo zinazowanyima haki sahihi wengine.