UMAKINI kwenye utendaji kazi ni muhimu kwa kila mmoja haijalishi anafanya jukumu gani kama mwajiriwa au kujiajiri ni wazi kwamba hali hiyo ni miongoni mwa mambo yanayochochea mafanikio, kuzuia uhalifu au kuepusha hasara.
Hivi karibuni nikiwa kwenye daladala jijini Dar es Salaam, yenye namba T988 EEK inayosafirisha abiria kutoka Mbezi hadi Makumbusho kupitia Barabara ya Morogoro hadi Manzese, Magomeni ikiingia Barabara ya Kawawa na kuendelea hadi Mwananyamala mpaka Makumbusho nilijifunza jambo ambalo nafikiri ni vyema nikitumia nafasi hii kuwashirikisha wadau na wateja wa mabasi haya ya umma .
Safari iliendelea hadi kituo cha Tip Top abiria kadhaa walishuka na wengine waliochini walianza kupanda lakini ghafla kondakta akamzuia mtu mmoja asipande akimwambia gari limejaa, binafsi pengine na abiria wenzangu tuliposikia maneno hayo tulishtuka na kushangaa .
Ni kwa sababu watu wanaotumia usafiri wa daladala wanajua jinsi ambavyo ni vigumu kusikia kauli “gari imejaa’’ ikitamkwa na kondakta kwa sababu misemo kama gari halijai inajaa ndoo ya maji.
Baada ya hapo aliruhusu gari iendelee na safari kisha akaanza kumsimulia dereva wake kwa sauti kubwa akisema” nimemkatalia yule jamaa kwa sababu kila akipanda kwenye gari, lazima kutazuka tukio la mtu kuibiwa, sasa anaibia abiria wangu hadi nauli, wakishindwa kulipa nitapata nini ? Sasa wa nini kumbeba, hawezi kupanda gari ambayo haina msongamano wa abiria. Akikuta level seat hapandi,” anasema kondakta huyo.
Hapo baadhi ya abiria walimshukuru na kumpongeza, kwangu kitendo chake kikanifanya nitafakari jinsi gani tunahitaji watu makini kwenye kazi . Mfano kondakta huyu, amekuwa makini akijua kumekuwa na vilio vya abiria kuibiwa fedha au simu za mkononi wakiwa ndani ya vyombo vya usafiri, kondakta huyu ameonesha anavyoithamini kazi yake anavyopambana kukwepa hasara kwa abiria na kwake maana wanashindwa kulipa nauli baada ya kuibiwa.
Japo nilifikiri kondakta huyu angeweza pia kuhakikisha anaweka mtego kwa kumruhusu mwizi huyo apande na kumfuatilia kwa karibu ili kumkamata akiwa anaiba, ili achukuliwe hatua za kisheria kukamatwa na kushtakiwa.
Lingekuwa jambo jingine la kumfundisha adabu ili asiendelee kuwaibia abiria kwenye mabasi mengine, lakini ndiyo hivyo naona angalau yeye ameona njia nzuri ni kumkataa asipande kwenye gari lake hivyo amezuia uovu kutendeka.
Vilio vya kuibiwa havipo kwenye vyombo vya usafiri pekee, vipo kwenye maeneo ya ofisi tofauti ikiwamo za binafsi hadi za umma, lakini kumbe matukio hayo yangeweza kuzuiliwa kwa namna nzuri iwapo kila mtu kulingana na nafasi yake angeamua kutofumbia macho uhalifu anaouona.
Kuna huduma muhimu za kijamii zinazokosekana kwa sababu ya uharibifu wa watu wachache ambao wanafumbiwa macho, kumbe kama wanajamii wasingekaa kimya wangepaza sauti au kuchukua hatua ya kuwaripoti wangesaidia kuzuia kuendelea kutendeka kwa uovu huo.
Kuzuia uovu usitendwe ni jambo jema kuna matukio mengi ya kikatili yanayoendelea kufanywa huko kwenye jamii, ikiwamo kubakwa au kulawitiwa, ukatili wa kijinsia kuna wanawake wanashambuliwa kwa vipigo na kufanyiwa unyama, pia wapo wanaume wanaofanyiwa ukatili hasa wanapopoteza kazi au wanapoyumba kiuchumi wanaishia kudhalilishwa.
Hapo kwenye ukatili wa kijinsia wapo ambao huamini kwamba ni mambo binafsi lakini ukweli ni kwamba ni masuala ambayo yamekuwa yakichangia matukio ya vifo, kuanzia kujiua au kuuawa, waathirika wanahitaji kupewa ushauri wa namna bora ya kumaliza tofauti zao, pia kwenye suala la ukatili kwa kuna baadhi ya wazazi hawapo makini kwenye malezi hivyo hutoa mwaya kwa waovu kutimiza ukatili wao.
Mzazi au mlezi hajui mwanaye yuko wapi hata giza likiwa limeingia usiku, inakuwaje unakutana na mtoto ametumwa dukani saa mbili usiku, hawa wanapaswa kuelimishwa au kuripotiwa kwa viongozi ili kuwanusuru watoto.
Kila mwanajamii aangalie namna ya kushiriki kuzuia uhalifu usitendeke kuliko kusubiri tukio litokee ili upate cha kusimulia, wakati hasara, uharibifu na hata kifo kimeshatokea.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED