Mtakaotemwa poleni nafasi ni moja pekee

By Sabato Kasika , Nipashe
Published at 02:30 PM Jul 30 2025
Bendera
Picha: Mtandao
Bendera

MAKADA 5,475 wa CCM, walijitokeza kutia nia ili wateuliwe kuwania ubunge katika majimbo 272 ya uchaguzi Bara na Visiwani, lakini bila kutaja wawakilishi na madiwani ni idadi kubwa hata kuliko majimbo yaliyopo.

Kwa wingi huo wa watiania kila mmoja wao alijua kuwa kuna mchujo utapita ili hatimaye abaki mmoja kila jimbo atakayepererusha bendera ya chama kwenye uchaguzi huo dhidi ya wagombea wa vyama vingine.

Mwisho wa hatua zote za kupata mgombea wa kila jimbo, ni kwamba watia 5,203 watakosa nafasi hiyo, kutokana na ukweli kwamba majimbo ya uchaguzi yaliyopo ni 272 pekee.

Wingi huo wa watiania ya ubunge, ni vyema wahusika wauchukulie kama kucheza bahati nasibu, ambayo ina kupata na kukosa, hivyo ninadhani hatakuwepo wa kulalamikia kukosa nafasi hiyo moja.

Kwa hali hiyo, kama wapo wanaojiandaa watakuwa na sababu ya kulaumu katika mchezo huo wa bahati nasibu walioutaka wenyewe kwa kurundikana katika jimbo moja watiania zaidi 50.

Lipo jambo ambalo wanasiasa hawana budi kulizingatia, nalo ni kwamba nafasi inayotafutwa ni moja katika jimbo, ambayo hata wakijitokeza wengi kiasi gani, mwisho wake atateuliwa mmoja.

Hivyo, suala la mchujo haliepukiki na imekuwa ni kawaida baada ya hatua hiyo, baadhi ya watiania wa vyama mbalimbali vya siasa wanaotemwa, huhama na kwenda kutafuta fursa katika vyama vingine.

Katika mazingira hayo, wapo ambao hutukana kule walikotoka ili mradi wajitengenezee mazingira ya kuaminika na kupewa nafasi na kusahau kuwa chama ni itikadi ambayo ni vyema kujua kabla kujiunga.

Mwanachama kuhama chama inaweza kuwa ni haki yao, kwa sababu mtu ana haki ya kujiunga na chama anachokipenda. Lakini swali ni kwamba; wanaofanya hivyo huwa hawajui itikadi za vyama vyao?

Kimsingi, lipo jambo ambalo wanasiasa hawana budi kulizingatia, nalo ni hili, kwamba nafasi inayotafutwa ni moja katika jimbo, ambayo hata wakijitokeza wengi kiasi gani, mwisho wake atateuliwa mmoja.

Chama cha siasa ni itikadi, itikadi ni imani, hivyo kwa kawaida huwa ni vigumu kwa watu kubadili imani, kwa sababu ya kutemwa kwenye utitiri wa watia nia ambao hawawezi kuchukuliwa wote.

Itikadi ni mwongozo wa kikanuni unaozingatia jamii au kundi fulani. Lakini pia ikumbukwe kuwa vyama hutofautiana itikadi na imani, hivyo kwa mtu aliyezama katika itikadi na imani ya chama fulani inaweza kumuwia viguumu kuhama kwa sababu ya kuachwa.

Pamoja na hayo, chama ni muungano wa watu wenye nia na malengo yanayofanana, hivyo watu hao wanaounganishwa na itikadi yao hufikia maamuzi ya pamoja kupitia vikao vyao.

Kwa utaratibu huo, hakuna mtu mmoja mwenye uwezo wa kufanya maamuzi ya chama nje ya vikao. Katika kufafanua utaratibu huo wengine huwa wanasema 'Hakuna chama bila vikao'.

Anayeamini itikadi ya chama, inaweza kuwa vigumu kwake kuchukua hatua kama hiyo. Kwa msingi huo, hata kwa wale waliotemwa kwenye ubunge wasiwe wepesi wa kukimbilia kwingine.

Hatua kama hiyo itakuwa ni sawa na kulazimisha jambo. Yaani kutaka kuwa kiongozi kwa kila njia, ikiwamo kupitia vyama vingine kwa sababu ya kuachwa katika cha awali.

Ninajadili jambo hili kwa sababu wapo wenye sababu mbalimbali kuwa 'hamahama' ya wanasiasa inatokana na kukosa msimamo, kutafuta chama kinachoridhisha nafsi za wahusika au kusaka tonge.

Wapo wanaotoka nje ya chama ili mradi wajitengenezee mazingira ya kuaminika na kupewa nafasi na kusahau kuwa chama ni itikadi ambayo ni vyema kujua kabla kujiunga.

Mtindo huo wa baadhi ya wanasiasa kuhama vyama, ni sawa na kukosa msimamo au kushindwa kuelewa itikadi za vyama walivyotoka na kusukumwa na maslahi binafsi badala ya kutumikia wananchi.